Wednesday, November 27, 2013

Sio sahihi kumuhurumia Zitto kwa sababu tu ni Zitto. Sio sahihi kumuhukumu Zitto kwa sababu tu ni Zitto.


Kipimo hicho hakijafikiwa popote. Wapo wengi ambao hawataki kufikiria tofauti zaidi ya kwamba Zitto ni msaliti na adui namba moja wa Chadema. Kwamba Zitto anatumika kukidhoofisha chama na ni tatizo kubwa sana zaidi ya Shibuda au Selasini au Lema au Lissu.

Wapo ambao wanaamini bila sababu zozote za msingi kwamba Zitto ni malaika, anakijenga chama na kukisaidia chama chake kufikia malengo.

Pia wapo ambao wanazo sababu za kumuamini Zitto. Hawa wanamuamini na pia wanakubali kwamba ana mapungufu yake. Haya ni mawazo yaliyomo kwenye waraka wa Mwigamba. Na haya ni mawazo ambayo mimi binafsi ninayo.

Katika mambo ambayo yamesemwa sana kwa ufupi ni haya;

1. Zitto ni mdini. Ana tabia ya kuendekeza Uislamu.

2. Zitto anaisaidia CCM kwa kuihujumu Chadema. Kwa kufanya haya;

2.1 aliuza baadhi ya majimbo

2.2 hakumpigia Dr Slaa kampeni

2.3 hakupigia wagombea udiwani kwenye jimbo lake kampeni

2.4 anamsifia Raisi Kikwete

2.5 ana marafiki wana CCM

2.6 wakati wabunge wenzake wanatoka Bungeni yeye hakwenda kabisa.

2.7 hashiriki kwenye maandamano yanayoandaliwa na chama

3. Kwamba hashiriki vikao makao makuu

4. Sio muadilifu anapokea rushwa na malipo yasiyo halali kutoka CCM na Usalama wa taifa.

5. Anatengeneza makundi ya uasi ndani ya chama.

Hayo ni baadhi ya yake ambayo mimi nasikia yakisemwa. Sijawahi kuona au kupewa ushahidi wowote. Yote ni ya kusikia tu. KUSIKIA.

Inawezekana yote hayo anasababisha Zitto mwenyewe kwa sababu ya tabia yake ya kujiamini na kutokujipendekeza kwa watu fulani fulani kama ilivyo tabia ya wanasiasa wengi.

Sioni kama ni kosa yeye kuwa na misimamo tofauti na wengine ili mradi tu ndicho anachokiamini na umma kwa kiasi kikubwa unaona ni sawa.

Kwa mfano, Zitto alikuwa wa kwanza kukubali kwamba uchaguzi Mkuu umeisha na JK ni Raisi. Hili kwa juu juu ni kosa kwa sababu Katibu Mkuu alitoa kauli kwamba Chadema haimtambui Raisi. Na tukasusia sherehe za kuapishwa. Lakini Bungeni tukaenda!! Mkakati ulikuwa wabunge watoke nje akianza kuhutubia...

Mpaka leo JK ni Raisi na yeye ndie tumeenda Ikulu kumuona....

Zitto aliona hilo akaamua kutokwenda kabisa bungeni. Kwa wengi watasema alisaliti! Siamini hivyo.

Au suala la posho. Yeye binafsi amekataa kuchukua posho. Anaitwa mnafiki. Kwa sababu wengine wanazitaka.

Hili suala ambalo sio la chama. Chama kilishasema posho zifutwe. Na ilani ya uchaguzi ilisema tutafuta posho ila baada ya kupata madaraka. Zitto anakosea kukataa posho kabla ya kushika dola!! Hapa ni Zitto dhidi ya wabunge wenzake wanaopokea posho pamoja na madiwani.

Hiyo ni mifano tu ya tabia na misimamo ya Zitto inayotafsiriwa tofauti na wale waliomkamia au ambao basi tu hawampendi. Pia misimamo ambayo yeye ameshindwa kuona au ameona ni jinsi gani itamfanya awe adui namba moja.

Posho: wabunge wote na madiwani pamoja na wajumbe wa baadhi za Halmashauri za vijiji na Kamati mbali mbali tunapokea posho. Zitto ni nani zaidi ya mnafiki na msaliti kukataa posho na kusema ifutwe? Tule wapi?

Huyu ni mtu anayechukiwa na asilimia 90 ya wabunge, madiwani, wenyeviti wa vijiji na wajumbe wa halmashauri na kamati mbali mbali nchini ambao posho sio jambo la kugusa kwanza wanataka ziongezwe.

Sasa anataka uenyekiti wa chama kikuu cha upinzani nchini. Chama ambacho kuna watu 'wamekifadhili' na kukaribia 'kufilisika' kwa ajili ya kukijenga kichukue dola (sio lazima iwe kwa ajili ya wananchi)....kwa sababu ingekuwa hivyo basi isingekuwa shida kumuachia mwingine.....

Mawazo yangu. Yasihusishwe na mtu yeyote. Ukweli au uongo wake ni wangu. Na wangu pekee.

Msando Albert-Wakili na Diwani wa Chadema

No comments:

Post a Comment