Thursday, November 7, 2013

Alama mpya sekondari ‘madudu’ yaibuliwa


0
Share


Kwa kutumia mfumo mpya ufaulu wa Kidato cha Nne mwaka jana ungekuwa asilimia 94
Dar es Salaam.Wakati Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne nchi nzima ukiendelea, imebainika kuwa madaraja na alama mpya za ufaulu kwa shule za sekondari zilizotangazwa na Serikali hivi karibuni ni tofauti na zile zilizopendekezwa na Kamati Maalumu iliyoundwa kuchunguza suala hilo pamoja na zile zilizotolewa na makundi mbalimbali yaliyoshiriki kuandaa mfumo huo mpya.
Mbali na kwenda kinyume na maoni hayo, alama hizo zinaifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza duniani kuwa na viwango vya chini vya ufaulu.
Alama hizo zilizotangazwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome zinaonyesha kwamba: A=75-100, B+=60-74, B=50-59, C=40-49, D=30-39, E=20-29 na F=0-19, huku alama endelevu za upimaji wa mwanafunzi shuleni (Continuous Assessment-CA) ikiwa ni 40 na mtihani wa mwisho ukichangia alama 60.
Kabla ya Serikali kutangaza alama hizo mpya, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi iliunda Kamati Maalumu iliyopewa jukumu la kufanya uchunguzi na kuja na mapendekezo ya viwango vipya vya ufaulu na utaratibu wa CA.
Kamati hiyo ilifanya kazi hiyo na kukabidhi ripoti yake wizarani Septemba mwaka huu na mapendekezo yake kwenye upangaji wa alama hizo ilikuwa ni A= 80-100, B= 70-79, C= 50-59 D= 40- 49, E= 35- 39 na F= 0-34 huku wakitaka CA iwe alama 25.
Baada ya kuandaliwa kwa ripoti hiyo, Serikali ilitafuta maoni zaidi kutoka kwa wadau wengine kupitia makundi mbalimbali ambayo nayo yalitoa mapendekezo.
Kundi la kwanza lililotoa mapendekezo yake ni Jukwaa la Taasisi za Elimu za Serikali ambalo lilitaka ufaulu uanzie alama 40, kundi jingine ni Vyuo vya Watu Binafsi ambalo lilipendekeza ufaulu uanze alama 35 huku Wakuu wa Vyuo vya Serikali na Wakaguzi Wakuu wa Kanda wakitaka ufaulu uanzie alama 40 na CA iwe 30.
Ofisa mwandamizi kutoka Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), ambaye aliomba jina lake lisitajwe gazetini alisema kitaalamu CA hutakiwa kuwa chini ya alama ambayo inahesabika kuwa ndiyo ufaulu.
Alisema baada ya Serikali kupitisha mfumo ambao ufaulu unaanzia 20, ilitarajiwa CA kuwa chini ya 19 badala ya 40 iliyopitishwa na wizara.
Ufaulu wa chini
Kwa mujibu wa kitabu kinachoonyesha viwango vya ufaulu duniani kila mwaka cha International Qualification, baada ya Tanzania kutangaza alama hizo mpya, sasa inakuwa nchi inayoongoza duniani kwa kuwa na alama za chini za ufaulu.

No comments:

Post a Comment