Tuesday, November 12, 2013

Tume ya Katiba TZ yapata pigo

Marehemu Dkt. Sengondo Mvungi aliyekuwa Mjumbe wa Mabadiliko ya Katiba nchini Tanzania
Tume ya Mabadiliko ya Katiba nchini Tanzania imepata pigo baada ya mmoja wa wajumbe wake Dr. Sengondo Mvungi kufariki dunia nchini Afrika Kusini, ambako alikuwa akitibiwa.
Dr. Mvungi, alipelekwa Afrika Kusini kwa matibabu zaidi baada ya kuvamiwa na watu wanaoaminika kuwa majambazi nyumbani kwake mjini Dar, es Salaam, wiki iliyopita.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Bw. Assaa Rashid Dkt. Mvungi alifariki majira ya saa 8:30 mchana kwa saa za Afrika ya Kusini akiwa katika Hospitali ya Milpark.
"Kwa masikitiko makubwa, Tume inawafahamisha wananchi kuwa Mjumbe wake, Dkt. Sengondo Mvungi aliyekuwa akipata matibabu katika Hospital ya Milpark iliyopo jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini amefariki dunia leo Jumanne, Novemba 12, 2013 saa 8:30 mchana kwa saa za Afrika ya Kusini," amesema Bwana Rashid katika taarifa yake fupi.
Amesema taratibu za kuusafirisha mwili wa marehemu kutoka nchini Afrika Kusini kuja nchini Tanzania kwa mazishi zinaendelea.
Marehemu Dkt. Mvungi alisafirishwa siku ya Alhamisi, Novemba 7, 2013 kwenda nchini Afrika Kusini kwa uchunguzi na matibabu zaidi akitokea Kitengo cha Mifupa Muhimbili (MOI) alipokuwa amelazwa baada ya kuvamiwa nyumbani kwake.
Dkt. Mvungi pamoja na kuwa ni mwanasheria aliyebobea katika fani ya Katiba, pia ni mwanasiasa ambaye aliwahi kugombea urais mwaka 2005 kupitia chama cha NCCR Mageuzi.

No comments:

Post a Comment