Friday, November 15, 2013

Sehemu ya hotuba ya mh. Zitto Kabwe. (Verbatim)-Kaliua, Tabora 9/11/2013


".......Kwa hiyo tunahitaji nguvu kazi kubwa sana. Siyo kazi ndogo na ndiyo maana kwa kufanya kazi kubwa kama hii, na ninapokuwa na ajenda kubwa, ni mtaji sana kuwa na support ya Watanzania wa ndani ya chama changu na nje ya chama changu.

Kinachonisikitisha ni kwamba wakati niko nafanya kazi kubwa kama hii, kazi ambayo ina hatari kwa maisha yangu, kwa sababu watu wana nguvu sana. Mimi mtoto wa masikini tu na ninatoka Kigoma. Sina nguvu yoyote. Ndugu yangu ni mwenyezi Mungu (Allah Subhanahu Wa Ta'Ala). Basi nguvu yangu ni ninyi watu kuwategemea.

Kwamba unapokuwa unafanya kazi hii ya kupambana na watu wa namna hii upate nguvu. Bahati mbaya sana, tena sana, sana. Navunjwa nguvu na watu wengine wanaonivunja nguvu ni watu ambao mko chama kimoja ambapo kwa hali ya kawaida walipaswa kutia nguvu.

Inasikitisha kwa sababu unapokuwa mwanasiasa lazima kuwe na mashambulizi ili yakukomaze. Nani huyo mwanasiasa asiyepata mashambuzi haiwezekani au siyo.

Lakini unapokuwa una ajenda ambayo unaisukuma halafu unapigwa mishale na watu wako, si utaanza kwanza kujilinda na ile mishale halafu hiyo ajenda unaisahau. Anayefaidika ni nani?. Ni adui.

Na huu ndiyo ujumbe ambao nataka hasa watu wa CHADEMA wajue. Tuna kazi kubwa. Kazi ya kupambana na dude CCM siyo mchezo. CCM ni kama lipweza hivi lina miguu mingi. Ili uliue lazima upige miguu mingi karibari mpaka afe na wakati anapotaka kufa lazima atetereke, lazima atumie watu kuwavuluga, lazima. Huwezi kuwa na chama ambacho kimekaa madarakani kama CCM kwa muda mrefu sana, halafu kinaona wananchi wamekichoka, halafu eti kikae kimya kikubali kutoa madarakani. Kinachokifanya ni kuonyesha kwamba, aah, watu wote ni walewale. Bora zimwi likujualo. Ndiyo kazi inayofanyika.

Ninataka niwahakikishie wanaCHADEMA kwamba hakuna mgogoro wowote CHADEMA. Kuna watu wachache, wachache sana ambao hawana kazi isipokuwa kazi ni kugonganisha viongozi ili viongozi wasielewane, ili viongozi wasipoelewana ndiyo faida kwao, ndiyo wanakula, ndiyo wanaonekana wanafanya kazi.

Na kuna uwezekano mkubwa sana watu hao wanatumika na watu wa nje ya chama ili kuvuluga.

Nataka niwaonye kwamba hatuwezi hata kidogo kushika dola kama ninyi wenyewe wananchi mnatuona hatuko wamoja. Mtatupa dola mkituona siyo wamoja? (Hapana-Sauti ya wananchi). Si mtatuona kama CCM tu.

Kwa hiyo siyo ufahari hata kidogo kwa CHADEMA kuonekana na yenyewe ina migogoro kama CCM. Siyo fahari. Inawavunja moyo nyie, nyie mnatuamini kwamba sisi tutaleta mabadiliko.

Ngojeni niwaambie. Historia ya chama chetu ni historia ya kidemokrasia. Chama hiki kimeanza mwaka 92. Mwenyekiti wetu wa kwanza Mzee Mtei. Mwaka 95, Mzee Mtei na Marehemu Bob Makani walisimama kugombea Urais ndani ya chama, na Urais ulikuwa na nguvu kweli kweli. Baadaye chama kikaamua kwamba, aah, CHADEMA itamsapoti Mrema wakati huo. Je, mliwahi kusikia hadharani Bob Makani na Mzee Mtei wanagombana. Mwaka 1998, Marehemu Mzee Bob Makani na Mzee Ndesamburo waligombea uenyekiti wa Taifa wa chama, kina Mbaruko hawa ni mashahidi. Mwaka 98, Marehemu Mzee Bob Makani akashinda. mlisikia migogoro? (Hapana-sauti ya wananchi).

Mwaka 2009, kwa kufuata misingi hiyo hiyo ya demokrasia, mimi niligombea uenyekiti.

Kwa nini uwe nongwa, si ndiyo demokrasia tu. Si ndiyo demokrasia tu na mkimaliza mnaenda kujenga chama.

Na tumeenda kujenga chama na tumeibua mambo ndani ya bunge dhidi ya CCM. Tumeibua hoja zenye nguvu ndani ya bunge dhidi ya Chama Cha Mapinduzi. Tumeibua hoja za kumpiga chini Waziri Mkuu na Mawaziri wanane wakafukuzwa kazi ili kumuokoa Waziri Mkuu. Haya yamefanyika baada ya 2009.

Sasa watu wanaona uchaguzi unakaribia, halafu sijatangaza. Vulugu zinaanza, maneno yanaanza, uzushi unaanza ili kutugawa bila sababu, bila sababu yoyote, bila sababu yoyote ile.

Kwa kweli kwa mtu kama mimi ambaye nimeingia kwenye siasa mdogo sana. Kigoma wamenichagua na miaka 29, na kubeba majukumu makubwa sana kisiasa, makubwa kwa maendeleo ya Mkoa wangu.

Sasa hivi tunafanya kazi ya kanda ya jimbo letu hili la kanda ya Magharibi. Tumeibua hoja nzito nzito bungeni. Kwa umri mdogo sana.

Kwa mishale ya kisiasa ninayopigwa, nadhani Mwenyezi Mungu amenipa sifa ya ziada ya uvumilivu (Makofi-kutoka kwa wananchi), lakini mimi ni binadamu, msisahau hilo. Mimi ni binadamu, mkinifinya ninaumia (Kicheko-kutoka kwa wananchi). Ninatoka damu kama mwingine yoyote. Nimechoka kupigwa mishale, nimechoka (Kicheko-kutoka kwa wananchi).

Kwa hiyo ni lazima tuambizane kuwa turudi kwenye reli ya kujenga misingi ya chama hiki ili tuwakomboe wanyonge. Tuhakikishe hatuwaangushi wananchi.

Hivi mnakumbuka kulikuwa na chama chenye nguvu kama NCCR-Mageuzi. Mnakumbuka kulikuwa kuna mtu mwenye nguvu kama Augustino Mrema. Lakini walifanyaje?. Walianza kusema Marando msaliti. Mabere Marando alachafuka, akawa ananuka.

Leo Marando yuko wapi?. Siyo Kamanda wetu?. Siyo mwanasheria wetu?. Halafu Mrema yuko wapi?. Amebaki na Mbunge mmoja, yeye mwenyewe. Lazima tujifunze.

Lazima tujifunze kuruka viunzi vya CCM kutaka kambi ya upinzani igawanyike. Kutaka vyama vya upinzani vipasuke. Lazima mjifunze kuruka viunzi.

Na ninyi ndiyo mnapaswa kuwa nguzo yetu. Ninyi mnapaswa kutuambia kwamba tunataka muwe wamoja. Na sisi tumeamua kanda yetu hii na sasa tunazunguka. Kwenye ziara tumebakiza Urambo. Tulikuwa tumebakiza Kariua, lakini bado kwa sababu jimbo hili ni kubwa na ninakubaliana na risala ya viongozi lazima turudi twende kwenye kata za kutosha.

Tunataka tuihamishe Tabora. Kigoma irejee heshima yake. Mpanda iamuke zaidi ili kanda yetu iongoze katika siasa za mageuzi na kuhakikisha kwamba CHADEMA inatoa wabunge wengi zaidi. (makofi-Kutoka kwa wananchi).

Ni lazima wanachama na uongozi ambao badala ya kufanya kazi ya kumshughurikia adui wanaanza kuleta chokochoko ndani ya chama wachukuliwe hatua za kinidhamu bila upendeleo. Bila upendeleo wowote (Makofi-kutoka kwa wananchi).

Sababu mkishaanza kuwa na upendeleo ndiyo mnaenda kuwa kwenye maneno ya CCM. Kila siku CCM wanasema CHADEMA, aaah, CHADEMA yao ni chama cha kidini. Chama cha Wakristo hicho, lakini tunasema, kama ni chama cha Wakristo, Arfi wa Mpanda ni Mkristo?. Hapana. Zitto Mkristo?. Hapana.

Lakini leo ukiona kundi la watu fulani wanamshambulia Arfi, wanamshambulia tu. Watu watafikiria.

Kila siku CCM wanashambulia wanasema CHADEMA chama cha Wachaga. Upuuzi mtupu. Tunasema hapana.

Viongozi wetu angalieni. CHADEMA ni kiti tu. Kwa nini msisimamie?.

Lakini wapumbavu wanaoenda kutumiwa na CCM bila kujiangalia wamejikuta wanawashambulia watu ambao ndiyo ngao ya kuonyesha umoja ndani ya chama.

Lazima tukatae hayo mambo na lazima viongozi tuhoji haya mambo na tusipoonya tutaonekana tutaonekana tunashiriki au siyo?. (Ndiyo-sauti ya wananchi). Tutaonekana tunafanyaje?.

Tunaonekana tunashiriki na sisi.
Waha tuna msemo, tunasema hivi, UKIMUONA KIFARANGA YUKO JUU YA CHUNGU UJUE CHINI KUNA MAMA YAKE.
by- Zitto Kabwe
 

No comments:

Post a Comment