Tuesday, November 26, 2013

CHADEMA KUTOKA 1995 KUELEKEA 2015- Na Chambi Chachage



Wale wanaosahau yaliyopita wamehukumiwa kuyarudia. Hayo si maneno yangu, ni ya mchambuzi mmoja mahiri. Japo aliyasema zamani bado yanatulenga sisi leo.

Yaliyotokea kati ya mwaka 1993 na 1995 yanafanana na yanayotokea sasa kati ya 2013 na 2015. Hebu tujikumbushe. Baada ya Tanzania kuurejesha mfumo wa vyama vingi, nyota ya kisiasa ya Augustine Lyatonga Mrema ilianza kung’aa kwa kasi ya ajabu. Wivu ulitanda ndani ya chama tawala. Wananchi walionekana kumkubali sana hasa alipokua akitoa siku 7 za utekelezaji wa maazimio yake dhidi ya uhalifu na wahalifu.

Rais Ali Hassan Mwinyi alimpa rungu pale alipounda nafasi ambayo haikuwepo kabla, yaani Unaibu Waziri Mkuu. Mrema akapachikwa jina la ‘Fagio la Chuma’, la kufagia takataka zote za ufisadi nchini. Wapinzani wake wakadai yote ni kiini macho, wengine wakadiriki kusema hata anatumia hizo siku 7 za vitisho kudai rushwa.

Hakika Mrema alibobea katika kile ambacho wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanakiita ‘populism’, wakimaanisha siasa ya kukong’a nyoyo za watu kiasi kwamba hata wengine wanakuwa wafuasi wako tu bila kutafakari wewe ni nani na unasimamia nini hasa.

Nakumbuka enzi hizo nikiwa mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Azania kuna siku tuliambiwa twende kwenye viwanja vya Jangwani kuhudhuria tukio kubwa la Kiserikali. Wakati viongozi wengine wakiwa ndani ya magari yao yaliyojulikana kama 'mashangingi' wakikodoa macho nje, Mrema alikuwa akitembea kwa miguu huku amezungukwa na watu wa kawaida na wanafunzi.

Huyo ndiye alikuwa Mrema wa kuelekea 1995. Alipotofautiana na wenzake kwenye serikali ya chama tawala, akalazimika kutoka na kuingia kwenye upinzani. Japo wapo waliodai kuwa alitumwa kwenda kuvunja upinzani, tulichokiona ni hali ya kuweweseka ambapo ilibidi muasisi wa chama tawala, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aingie dimbani kujaribu kutafuta ‘mgombea safi’ ambaye angalau ataweza kuikoa nchi kutoka katika janga la kitaifa la ufisadi na kukabiliana na mpinzani wao mkuu. Kwa taabu sana Benjamin William Mkapa akamshinda Mrema.
Kilichofuata baada ya 1995 ni kudidimia kwa kilichokuwa chama kikuu cha upinzani. Hali ilikuwa tate na tete kwenye mkutano wa chama hicho mjini Tanga ambapo taa zilipozimwa, vurugu kubwa ilitokea. Mtafaruku huo ulisababisha na kupelekea uwepo wa kambi ya Mrema na ya Mabere Marando. Mwisho wa siku wote waliondoka chamani.

Wapo wachambuzi wa mambo ya kisiasa wanaodai kuwa kila uchaguzi mkuu unapokaribia chama kilicho kikuu cha upinzani kinahujumiwa na chama kingine kinapandishwa. Kwa mantiki yao, 1995 chama cha upinzani kilichokuwa kwenye chati ni NCCR-Mageuzi ila ilipofika 2000 ikawa ni CUF. Mantiki hiyo inaendelea kudai hicho nacho kikahujumiwa 2005 na hivyo kupelekea kupanda kwa CHADEMA mwaka 2010.

Mgogoro unaondelea sasa ndani ya CHADEMA unaonekana, kwa mantiki, hiyo kuwa ni sehemu ya kutekeleza mlolongo huo wa kuhujumu chama kikuu cha upinzani kabla ya uchaguzi mkuu ujao. Safari hii shutuma hizo zimelengwa kwa mwanasiasa machachari mwenye mvuto na ushawishi mkubwa, Zitto Zuberi Kabwe. Sasa glovu zimevuliwa na pambano kati ya wapinzani wa "mwanasiasa huyu nguli", kama rafiki yake Dakta Kitila Mkumbo anavyomtambulisha, liko wazi baada ya kufichwafichwa kwa maneno ya kisiasa kuwa ‘Hakuna Mgogoro wowote CHADEMA’.

Mijadala inayoendelea kwenye mitandao ya Jamii – Twitter, Facebook, Jamii Forum, Mwananchi News n.k. – inadhihirisha kuwa Zitto anakubalika sana miongoni mwa vijana na wanaharakati walioko kwenye asasi huru za kiraia (NGOs/CSOs). Kwa wengi wao anaonekana ni mkweli na mzalendo anayeweka maslahi ya taifa mbele kuliko maslahi yake binafsi na ya chama chake. Pia kuna makundi ya vijana wasomi, wakiwemo wale waliopoteza na walioanza kupoteza imani naye kutokana na sakata la DOWANS na suala la Kamati ya Madini aliyounda Rais Jakaya Mrisho Kikwete (Kamati ya BOMANI), ambayo sasa yemerudisha/yanarudisha imani yao kwa mwanasiasa huyu hasa baada ya kukataa posho na kuanza kuongoza vita dhidi ya posho pamoja na kusimamia kidete harakati za kurejesha mabilioni ya fedha zilizofichwa Uswizi na kwingineko.

Tatizo kubwa ni kuwa makundi yaliyopo CHADEMA nayo kwa kiasi kikubwa yanaakisiwa katika makundi haya ambayo yanajumuisha vijana ambao wanadai hawana chama ila ni wazalendo. Kwa kiasi fulani hali ya zile siasa za ‘populism’ inajionyesha ndani na nje ya chama kikuu cha upinzani hivyo hata kusababisha iwe vigumu kupata uchambuzi ambao ni huru.

Jambo hili linasikitisha hasa ukizingatia kuwa jamii yetu inawategemea vijana walio kwenye asasi huru za kiraia na vyuo vikuu pamoja na wahitimu wake walio kwenye sekta binafsi, wewe tayari kuweka pembeni siasa za kishabiki/kinazi na kuchambua masuala haya kwa uwazi na uhuru bili kujali kama mtu au watu wao ndio wanahusika.

Inasikitisha pale unapoona vijana wasomi/wanazuoni wakitoa misimamo na maneno ya kishabiki hata kabla ya kusoma kwa undani tamko la Zitto na la Kitila, kuyalinganisha na tamko la Kamati Kuu ya CHADEMA kama lilivyosomwa na mwanasheria mkuu wa chama hicho, Tundu Antiphas Lissu. Vijana hao, wakiwemo wale walio kwenye yale yanayoitwa ‘Think Tanks’ (Taasisi za Tafakuri), watatusaidia sana kama watafanya uchambuzi wa kina wa matamko kama hayo na kuyalinganisha, kwa mfano, na makala/maelezo/matamko mbalimbali ya zamani pamoja na mahojiano ya zaidi ya masaa 7 ambayo Zitto aliyafanya na Jamii Forum. Kwa kuwa Zitto na Kitila wamehusishwa na wamekiri/wamedhihirisha kuhusiana, ingekuwa vyema pia kama watalaamau wetu wangefanya uchambuzi wa maandishi ya Kitila katika mtandao wa Mabadiliko na wa Jamii Forum na kutusaidia kuelewa kwa upana huo unaoitwa Mkakati wa Mabadiliko 2013 na hata ile iitwayo Ripoti ya Siri Juu ya Zitto Kabwe ambao nao unalitaja jina la Kitila.

Mpaka dakika hii pia sijaona vijana hao waliobobea, walau kishahada, katika tasnia ya uchambuzi wa kisiasa, wakichambua kwa kina, kwa mfano, kuingia ulingoni kwa mwanasheria aliyebobea, Lissu, kwenye pambano hilo dhidi ya Zitto, jambo ambalo halijawahi kutokea waziwazi. Hata kitendo cha Kitila kuipiga dongo Kamati Kuu ya CHADEMA kuhusu kile ambacho anakiita ni (pengine) kupitiwa kwa kamati hiyo kinastahili uchambuzi wa kisiasa na si wa kisheria tu.

Kwa kudai kuwa Kamati hiyo ambayo ina wanasheria nguli imemvua ujumbe wa Kamati Kuu ya Chama ilhali haina mamlaka hayo ambayo ni ya Baraza Kuu, moja kwa moja Kitila anaigeuzia kibao kile kile ilichokitumia kuwapiga wao, yaani kuvunja Katiba ya chama. Lakini pia inaonyesha utayari wa kupambana na mwanasheria Lissu ambayo kwa wale tunaomjua, inahitaji kazi ya ziada hasa kama amejipanga na ushahidi.

Pia suala la kuingia ulingoni kwa Mwanasheria Alberto Msando ambaye naye ni mwana-CHADEMA tena ni kiongozi katika ngazi ya udiwani tena huko huko kwenye kanda ambayo inadaiwa kuhodhi uongozi wa CHADEMA nalo linastahili uchambuzi yakinifu (rejea hizi salamu zake kwa Zitto na Godbless Lema). Je, huu ndio mwanzo wa kujitokeza waziwazi kwa kundi ambalo mwanasheria Nyaronyo Mwita Kicheere analiita “chadema yenye watu wenye fikra pevu”? Na, je, wachambuzi wetu waliochukua upande nao ni miongoni mwao? Kama ndio, wanaweza/wataweza kweli kufanya uchambuzi mpevu au watabakia kuwa wanatimu/mashabiki ambao msimamo wao unatabirika hata kabla hawajafungua mdomo kuongea au kuchukua kalamu kuandika?

Mimi binafsi uwezo wangu wa kuchambua masuala haya unafungwa kwa kiasi kikubwa na mgogoro wa maslahi (conflict of interest) n.k. Pengine wachambuzi wetu mahiri nao wana migogoro hiyo na labda ndio maana wengine wameamua kuwa waumini wa ushabiki tu wa kisiasa (populism) au/na wajumbe wa timu za wahusika. Kama ni hivyo, basi makala haya hayawahusu.
Ila kwa wale ambao hawana mgogoro na wasiofungamana na upande wowote, jamii iliyowalea na kuwasomesha inawadai wairudishie walau kitu kimoja – uchambuzi huru wa hali ya kisiasa na wanasiasa Tanzania kutoka 1995 kuelekea 2015 kwa maana safari hii wananchi tunahitaji kufanya uchaguzi sahihi.

No comments:

Post a Comment