Nape alifafanua kwamba hesabu za 2011/2012 bado ziko kwa
wakaguzi wa nje, wakishakamilisha nazo zitawasilishwa kwenye vikao vya
chama na hatimaye kwa CAG.
“Hesabu hizi zikikaguliwa kwa mujibu wa utaratibu,
anapelekewa CAG ambaye ndiye anazipeleka kwa Msajili wa Vyama vya Siasa
na sio vinginevyo,” alisema.
Alidai kuwa Zitto anapaswa kuanza kutoa ‘boriti
kwenye jicho lake ndipo aone kibanzi kwenye jicho la mwenzake’ kwa
sababu chama chake ndicho kimekuwa na matumizi mabaya ya ruzuku. Alisema
Zitto kama Naibu Katibu Mkuu wa Chadema ni vyema akawajibika ndani ya
chama chake ili kuonyesha mfano kwa wengine.
“Wote tunakumbuka kelele zilizopo mtaani kuhusu
matumizi mabaya ya ruzuku zinazoelekezwa na Chadema na viongozi wake
kutoka kwa wanachama wao, hivyo si ajabu wakawa wanakiuka sheria hii na
ndiyo chanzo cha kelele hizo za wanachama wao,”alisema.
Vyama vingine
Kwa upande wake, Chadema kilieleza kwamba
hakijapata barua inayowaarifu kuhusu kutaka kufungiwa ruzuku kutokana na
kutowasilisha taarifa ya ukaguzi.
Ofisa Habari Mwandamizi wa Chadema, Tumaini Makene
ilisema hata barua ya kuitwa kwenye Kamati ya PAC, iliwafikia kwa
kuchelewa. “Tunasubiri barua rasmi ya suala hili ndio mamlaka
zinazohusika na masuala ya fedha ndani ya chama, hususan, Baraza la
Wadhamini wa Chama kuweza kutafakari hatua,” alisema Makene.
Hata hivyo, alisema angependa umma utambue kwamba
“Chadema ndicho kilichokuwa mstari wa mbele tangu kabla na baada ya
mwaka 2009 kutaka ukaguzi na wazi katika mapato na matumizi ya vyama vya
siasa.”
Alifafanua kuwa msimamo wa Chadema kwenye
mkakakati huo ulikuwa ni kuibana CCM kutokana na madai ya baadhi ya
vigogo wake “kukwapua fedha Benki Kuu ( Akaunti ya Madeni ya Nje – EPA)
na kuzitumia kwenye uchaguzi wa mwaka 2005.”
Alijigamba kuwa hesabu za chama chake zimekuwa
zikikaguliwa kila mwaka na kwamba wanasubiri maelezo ya barua kuhusu
kile kinacholalamikiwa.
Kwa upande wa Chama cha Wananchi (CUF) kimesema
hesabu zake ziko safi, ila imeshindikana kukaguliwa kwa vile Serikali
haijatoa fedha za kugharimia ukaguzi huo.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Tanzania Bara, Julius Mtatiro alisema hesabu zao zimekwishakaguliwa na wakaguzi wa ndani.
No comments:
Post a Comment