Friday, October 4, 2013

Fastjet yabaki njia panda

KAMPUNI ya Ndege ya Fastjet imekuwa katika sintofahamu baada ya serikali ya Afrika Kusini kuendelea kuwa kimya na kushindwa kutoa kibali cha kuwaruhusu kutoa huduma ya usafiri kwenda nchini humo.
Septemba 27, mwaka huu, kampuni hiyo ilikuwa ianze safari za kwenda nchini humo lakini ilishindwa baada ya mkuu wa idara ya usafirishaji wa Pretoria kushindwa kuweka saini ili kuruhusu kampuni hiyo kuanza safari zake.
Akizungumza na Tanzania Daima jana, Meneja Biashara wa kampuni hiyo nchini, Jean Uku, alisema kuwa kampuni yake ilifuata utaratibu katika kuomba kibali cha kutoa huduma nchini humo lakini walishangazwa na idara ya usafirishaji kushindwa kuweka saini katika nyaraka hizo.
Uku alifafanua kuwa idara hiyo ilituma barua pepe kwa mamlaka ya viwanja vya ndege nchini humo na kuhitaji kutumiwa nyaraka nyingine muhimu ambazo zilishatumwa awali na kuhakikiwa.
Aliongeza kuwa Fastjet ilianza kuomba kibali cha kutoa huduma tangu Januari mwaka huu, hata ilipofika Septemba 25, mwaka huu, walizuru idara hiyo nchini humo na kuelezwa kuwa maombi yao yangeweza kushughulikiwa kwa siku 5 hadi 7.
“Tulipofika katika idara hiyo tulielezwa kuwa maombi yetu yanapitiwa na yanaweza kushughulikiwa kwa wiki moja, jambo ambalo lilivuruga utaratibu wa kuruka kwa ndege zetu kuingia nchini humo,” alisema.
Alisema kuwa hakuna sababu zilizotolewa na Afrika Kusini juu ya kuahirishwa bali ucheleweshaji umetokea baada ya idara ya usafirishaji kuomba nyaraka za ziada kutoka Fastjet.
Meneja huyo alisema kuwa pamoja na kuwepo kwa usumbufu kwa wateja, kampuni ililazimika kurudisha nauli zao na kwamba watafanya maandalizi ya safari na kukatiwa tiketi ya bure ya kwenda na kurudi ambayo itatumika kwa mwezi ujao.
Alisema kuwa safari za Fastjet kwenda Afrika Kusini zilipangwa kufanyika mara tatu kwa wiki na zilitarajiwa ziongezeke kutokana na mwitikio wa wateja wake.
chanzo-Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment