Dar es Salaam. Serikali inatarajia kuandaa hati ya dharura ili
kuwezesha kufanyika kwa maboresho ya Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya
Mabadiliko ya Katiba ambayo yatajadiliwa upya katika Mkutano wa Bunge
unaoanza Oktoba 29 mjini Dodoma.
Tayari vyama vya upinzani na chama tawala
vimekubaliana taratibu muhimu za kufuata ili maboresho hayo yaweze
kupita ndani ya Bunge. Muswada huo haukuwa umepangwa kujadiliwa katika
mkutano ujao wa Bunge ndio maana itabidi iombwe hati hiyo ya dharura.
Hatua hiyo ni ushindi kwa vyama vitatu vya upinzani vya Chadema, CUF na
NCCR- Mageuzi, ambavyo vilipinga muswada huo wakati wa mkutano uliopita
wa Bunge Septemba, mwaka huu.
Muswada wa sheria hiyo uliopitishwa Septemba na
Bunge ulisusiwa na wabunge wa vyama hivyo wa upinzani kwa maelezo kuwa
una kasoro kwenye baadhi ya vipengele.
Hata hivyo, wabunge wa CCM waliamua kuendelea na
mjadala na kupitisha muswada huo kitendo ambacho kilisababisha mvutano
mkubwa uliomfanya Rais Jakaya Kikwete kukutana na viongozi wa vyama vya
siasa vyenye wabunge kumaliza tofauti zao.
Mbatia asoma tamko la vyama
Akisoma tamko la vyama vya siasa mbele ya
waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia
alisema hatua ya Serikali itakuja baada ya vyama vya siasa kufikia
mwafaka wa vipengele vinavyotakiwa kufanyiwa marekebisho kwenye muswada
huo. Mbatia alisema kuwa tayari kazi hiyo imefanyika na mapendekezo yao
yameshapelekwa serikalini ingawa hakutaka kuingia kwa undani
walichopendekeza katika marekebisho hayo.
Vyama vilivyokutana ni pamoja na CCM, Chadema,
CUF, NCCR -Mageuzi, TLP. Pia vyama vya UDP na UPDP vilishiriki kwa niaba
ya vyama visivyo na wabunge.
Mbatia alisema hatua inayofuata ni vyama kuunda
kamati yao na Serikali kuunda yake ili kukubaliana kwa pamoja maeneo
muhimu ya marekebisho.
Alisema lengo la hatua hiyo ni kuufanya mchakato wa Katiba kuwa shirikishi baada ya kamati hizo kumaliza kazi yake.
“Baada ya hapo, Serikali itaandaa hati ya dharura
ili marekebisho yapelekwe haraka katika Mkutano wa Bunge unaoanza Oktoba
29, “ aliongeza Mbatia.
Mbatia alisema wanataka kabla ya Bunge la Katiba
halijaanza basi sheria husika ifanyiwe marekebisho. “Tunawaomba
Watanzania hasa wabunge waunge mkono juhudi hizi za vyama na Serikali
ili kuhakikisha mchakato wa Katiba Mpya unakuwa shirikishi. Wabunge
waridhie marekebisho haya na kuyapitisha,” alisema mbunge huyo wa
kuteuliwa na Rais.
No comments:
Post a Comment