Dar es Salaam. Sakata la vigogo kuficha mabilioni ya shilingi
katika benki za Uswisi, limechukua sura mpya baada ya Serikali ya nchi
hiyo kutunga sheria inayowabana walioweka fedha kwenye benki zake
kuzithibitisha, la sivyo zitarejeshwa katika nchi husika.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe alifanya
mazungumzo na Serikali ya nchi hiyo ambayo imemweleza kuwa imebadili
sheria zake ili kuwadhibiti wageni wanaoficha fedha nchini humo.
Akizungumza na gazeti hili, Zitto alisema amepata
taarifa hizo juzi baada ya kukutana na Waziri wa Fedha wa nchi hiyo
ambaye alimwandalia mazungumzo na watalaamu wake.
Alibainisha kuwa tangu kuibuka kwa sakata hilo
mwaka 2012 na Bunge kuiagiza Serikali kufuatilia, Serikali haijaomba
taarifa yeyote kutoka Uswisi kuhusu Watanzania waliohifadhi fedha nchini
humo.
“Jana nilikutana na Waziri wa Fedha na akatuacha
na mazungumzo na wataalamu wake. Wamesema hadi sasa, Tanzania haijasaini
mkataba wa kubadilishana taarifa za kikodi (Multilateral convention on
administrative assistance in tax matters),” alisema Zitto na kuongeza;
“Kwa kutosaini, Tanzania inajinyima haki ya kupata
taarifa hizi na kutoza kodi kwa watu walioficha fedha huku (Uswisi),
maana Sheria ya Kodi ya Tanzania inataka kila Mtanzania popote anapopata
kipato halali lazima alipe kodi.”
Zitto alieleza kuwa kitendo cha Serikali ya Uswisi
kubadili sheria zake, kinaiwezesha nchi hiyo kutoa taarifa za benki za
watu walioweka fedha nchini humo wakiwamo Watanzania, ambao sasa
watatakiwa kuthibitisha kama fedha hizo ni safi au la.
“Kiufupi, Tanzania haijaomba taarifa yeyote kutoka
Uswisi. Ila Uswisi wamebadili sheria yao na sasa mmiliki wa fedha ndiyo
anapaswa kuthibitisha kwamba ni safi, na ikithibitika kuwa hazina
mwenyewe wala maelezo, zitarudishwa nchi husika,” alisema.
Zitto alisema mbali na kukutana na watendaji hao
wa Serikali amezungumza na Umoja wa Mabenki wa nchi hiyo uliobainisha
kuwa Uswisi ina Watanzania wachache wenye fedha.
“Wamesema Watanzania wengi wana fedha Uingereza,
Jersey, Cayman Islands na Mauritius. Dubai pia imetajwa sana,” alisema
Zitto. Zitto alielezea kuwa umoja huo wa benki za Uswisi umeanzisha
mkakati wa kusafisha fedha uitwao ‘clean money strategy’, na wamegundua
watu wengi ambao ni wanasiasa, wamezuia akaunti zao na kupeleka majina
kwenye Serikali zao.
“Tanzania haijafanya maombi rasmi hapa Uswisi na
hivyo wao kama benki hawawezi tu kutoa taarifa bila kuombwa. Sheria yao
imerekebishwa ambapo sasa ni wajibu wa mwenye akaunti kusema kama fedha
zake ni halali au hapana,” alisema Zitto na kuongeza.
Hivi sasa hawapokei pesa kutoka nchi za Afrika au
wanapokea kwa tahadhari sana, maana kuna reputational risk (kupoteza
heshima),” alisema.
No comments:
Post a Comment