Rais Kikwete alisema kuwa Serikali yake itaendelea
kulinda amani ya nchi na maadui wote wanaohusika na kutaka kuvuruga
nchi watachukuliwa hatua kali za kisheria. “Kulikuwapo na upepo mbaya,
lakini kwa sasa Tanzania ni shwari na tumemshinda adui,” alisema Rais
Kikwete jana kwenye Maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Kifo cha Baba
wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere yaliyoandamana na sherehe za kuzima
Mwenge wa Uhuru, mkoani Iringa.
Alisema katika siku za hivi karibuni, maadui
wasioitakia mema Tanzania walikuwa na mkakati wa kuvuruga amani ya nchi,
lakini Serikali kwa kushirikiana na vyombo vya dola vimewadhibiti na
nchi iko salama.
Rais Kikwete alisema kuwa Serikali haiwezi
kuvumilia vitendo vya uvunjifu wa amani kwa sababu inajua wazi kwamba
nchi ikiingia kwenye mgawanyiko, mshikamano utavurugika na shughuli za
maendeleo zitasimama.
Katiba Mpya
Rais Kikwete alisema mwaka 2014 ni mwaka wa kipekee kwa nchi kwa kuwa utakuwa na mambo makubwa matatu yatakayofanywa.
Rais Kikwete alisisitiza kwamba Katiba Mpya ni lazima ikamilike mwakani kama mambo yatakwenda kama ilivyopangwa.
Vilevile, alisema mwakani Tanzania itasherehekea
miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyoondoa udhalimu na kuwarudishia
Wazanzibari heshima ya mwanadamu na utu wake.
“Pia tutasherehekea miaka 50 ya Muungano wetu.
Nawaomba Watanzania wajiandae kuyafanikisha vizuri mambo hayo ili
historia mpya ifunguliwe nchini.
“Wazanzibari waanze miaka mingine baada ya miaka
hamsini ya uhuru wao, muungano uanze miaka mingine baada ya miaka
hamsini na Katiba Mpya itupeleke miaka mingine tukiwa wamoja,” alisema
Kikwete.
Rais Kikwete alionya kuwa asingependa mchakato wa
kupata Katiba Mpya uligawe taifa na kuleta mfarakano utakaovunja umoja
wa kitaifa badala ya kuuimarisha.
“Tunataka tuwe na Katiba itakayojenga, siyo kubomoa, kutugawa kwa misingi ya kiitikadi,” alionya Rais Kikwete.
Chanzo-Mwananchi
Chanzo-Mwananchi
No comments:
Post a Comment