Friday, October 4, 2013

Jide, Diamond ndani ya Coke Studio

COCA-Cola Afrika Mashariki, Kati na Magharibi wanatarajiwa kuanzisha kipindi cha muziki kwenye runinga kinachoitwa ‘Coke Studio Afrika’ kikishirikisha nyota kibao wakiwamo Nasib Abdul ‘Diamond’ na Judith Wambura ‘Jide’.
Kipindi hicho, kitawahusisha wanamuziki wa miondoko ya aina tofauti kutoka sehemu mbalimbali ili kupata mchanyato wa kisasa wenye asili ya Afrika.
Meneja Bidhaa wa Coca-Cola Tanzania, Maurice Njowoka, alisema jijini Dar es Salaam juzi kwamba msimu wa kwanza Coke Studio Afrika itawahusisha wasanii nyota wa Afrika ambapo mbali ya Diamond Platinumz na Lady Jaydee pia watakuwepo Salif Keita wa Mali, King Sunny Ade, MI, Waje, Jimmy Jatt na Bez kutoka Nigeria.
Wengine ni Octopizzo, Miss Karun na Just a Band kutoka Kenya, Boddhi Satva, Tumi wa Afrika Kusini, Joel Sebunjo, Qwela, Lilian Mbabazi, Hip hop Panstula wa Uganda na Culture Music ya Zanzibar.
Njowoka alisema kipindi kitawahusisha pia wasanii walioshirikiana ikiwa ni pamoja na Bamboo wa Kenya, Sage na Dela pamoja na Kassongo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Temi Dollface wa Nigeria.
“Coca-Coca tunathamini nguvu ya muziki katika kuwaleta watu pamoja bila kujali jinsia, lugha, dini na nchi.
Kupitia Coke Studio, tunapata fursa adimu siyo tu kuwaleta wasanii wa Afrika pamoja, bali kuuboresha muziki wa Afrika uwe wa kisasa na unaowalenga vijana,” alisema Njowoka na kuongeza:
“Tuna imani tutawapa mchanganyiko wa muziki usiosahaulika katika kuimarisha mahusiano na wateja.
Coke Studio itakuwa inarushwa Kenya, Uganda, Tanzania na Nigeria, ikienda hewani kwa vipindi vinane vya dakika 45 kila kimoja pamoja na saa mbili za kipindi maalumu cha mwaka mpya.
Chanzo-Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment