Tuesday, October 15, 2013

Mawaidha ya Shk. Bombo katika Ibada ya Idi iliyoadhimiwa leo na Answar Sunna

 Picture
Kutoka kwenye blogu ya Mwanafasihi Mahiri, Mkwinda — Waumini wa dini ya Kiislamu mkoani Mbeya wameungana na Waislamu wenzao duniani katika kusherehekea ibada ya Eid na kutoa ujumbe wa kuzitaka nchi za Magharibi ziache uvamizi katika nchi za Kiislamu ambazo zina maslahi ya kiuchumi.

Akizungumza katika Ibada ya Swala ya Eid katika viwanja vya Kiwanja Ngoma, Sokomatola Jijini Mbeya, kiongozi wa Ibada hiyo ambaye ni Imamu katika msikiti wa Baraa Bin Azb Isanga, Shekhe Ibrahim Bombo alisema kuwa uvamizi unaofanywa na nchi za Magharibi umelenga kupora mali za wananchi wa nchi hizo.

Shekhe Bombo alisema kuwa limekuwa ni jambo la kawaida kwa nchi za Magharibi kudondoka mate kwa mali zilizopo katika
nchi za Kiislamu, hivyo njia pekee inayofanywa na nchi hizo ni kuzichonganisha ili machafuko yaibuke na wao kutumia fursa hiyo kuhujuma mali zilizopo katika nchi hizo.

Alisema kuwa ipo mifano mingi katika nchi zenye utajiri mkubwa duniani ambazo zimevamiwa na mali zake kuporwa na wageni kutoka nchi za Magharibi. Alizitaja nchi hizo kuwa ni pamoja na Libya, Afghanistan, Misri, Syria, Yemen, Iran na Pakistan ambako kumekuwa kukiibuka mapigano ya mara kwa mara huku wageni wakiingia katika nchi hizo wakijifanya wanasuluhisha migogoro ilhali wakiingilia utawala wa ndani na kujinufaisha kwa mali zilizomo: ''Tunalaani vitendo vya nchi za Magharibi kufanya uchonganishi kwa nchi zenye utajiri wa mafuta, itafika mahala dunia nzima haitakubali kwa dhuluma hii, tunaungana na wenzetu duniani kulaani dhuluma hii.''alisema Shekhe Bombo.

Shekhe Bombo alidai kuwa katika uvamizi huo yanafanyika mauaji ya kikatili kwa raia wasio na hatia ilhali akina mama na watoto wakidhalilishwa na kubakwa jambo ambalo halipaswi kuvumilika na kwamba itafika wakati Waislamu wote wataungana kupinga ukatili huo.

Aidha aliwataka waumini wa dini ya Kiislamu kutokubali kutenganishwa kwa imani zao moja na kwamba Waislamu wote wanaongozwa na Kitabu kimoja na Mtume mmoja na kwamba miongozo ya Uislamu inafuata taratibu za kitabu cha Koran na Hadith za Mtume Muhammad (SAW): ''Sisi sote ni Waislamu! inakuwaje  tukubali kutofautiana na wenzetu walioko Mecca Saudi Arabia ambao wanatekeleza ibada hii ya Hijja leo nasi tukiadhimisha kwa kufanya ibada ya Swala ya Eid el Haj?" alihoji Shekhe Bombo.

Wakati Waislamu wengine wameswali leo, kesho Waislamu wengine wanatarajia kuswali swala ya Eid kutokana na matangazo yatakayotolewa na viongozi wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA).

No comments:

Post a Comment