Friday, October 18, 2013

CHADEMA wamkana Zitto • Yeye asema anawangoja makatibu wakuu Oktoba 25

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema kuwa kimewasilisha taarifa zake za fedha kwa Msajili wa Vyama vya Siasa na zilizokaguliwa kwa mwaka wa fedha 2010/11 na 2011/12.
Kwamba, hilo linathibitishwa na barua ya Msajili wa Vyama yenye kumb. Na CDA.112/123/01a/37 ya Septemba 4, 2012, iliyopelekwa kwa makatibu wakuu wa vyama vyote vya siasa.
Uthibitisho huo umetolewa kukanusha taarifa ya Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe, iliyosema kuwa vyama vya siasa vinavyopata ruzuku kutoka serikalini havijawasilisha taarifa yake ya mapato na matumizi kwa ajili ya kufanyiwa ukaguzi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kwa kipindi cha miaka minne mfululizo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana huku akionesha nyaraka za vielelezo, Katibu wa Baraza la Wadhamini wa CHADEMA, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, Anthony Komu, alisema wamesikitishwa na taarifa ya PAC.
Alisema kuwa wameamua kuchukua jukumu la kuufahamisha umma kuwa wapo tayari kutoa ushirikiano wa dhati ili sheria hiyo ifanye kazi yake kwani tangu itungwe mwaka 1992 na kufanyiwa marekebisho mwaka 2009, CHADEMA kimekuwa kikifuata utaratibu kama ulivyoelekeza.
Komu alisisitiza kuwa taarifa za PAC si sahihi na hazina ukweli wowote kuhusiana na CHADEMA labda kwa vyama vingine.
Alifafanua kuwa hesabu za mwaka wa fedha zilizokaguliwa za 2009/2010, CHADEMA kiliwasilisha kwa msajili kwa barua yenye kumb. C/HQ/ADM/MSJ/04/71 ya Oktoba 2011.
Komu alionesha barua ya Msajili wa Vyama ya Septemba 4, 2012, ambayo ilionesha vyama vilivyowasilisha hesabu zilizokaguliwa kwake kuwa ni CHADEMA na NCCR-Mageuzi tu.
Kwa mujibu wa barua hiyo, CUF waliwasilisha hesabu kwa msajili bila kukaguliwa. Vyama ambavyo havikuwasilisha hesabu zao kabisa ni CCM, TLP, APPT- Maendeleo, UDP na DP.
Komu alifafanua kuwa taarifa ya fedha iliyokaguliwa kwa mwaka huu 2012/2013 bado hawajaiwasilisha kwenye ofisi ya msajili.
Alisema hatua hiyo ni baada ya ofisi ya msajili yenyewe kutoa maelekezo kwa barua yenye kumb. Na. DA.112/123/16A/97 ya Novemba 26, 2012.
“Tumefanya mawasiliano na CAG kwa ufafanuzi wa jambo hili na tutawafahamisha ipasavyo kuhusu malipo/gharama mliyotakiwa kulipa katika ukaguzi wa mahesabu hayo,” ilisomeka barua hiyo ya msajili.
Hadi jana wakati CHADEMA wanatoa utetezi huo, Komu alisema ofisi ya msajili ilikuwa haijatuma hata mkaguzi au maelekezo yoyote kama walivyoelekezwa walipe kiasi gani na wapi kwa kazi ya ukaguzi wa hesabu za mwaka 2012/2013.
Komu aliilaumu PAC kujitokeza hadharani kuzungumza mambo mazito pasipokuwa na ushahidi wala kuwashirikisha wahusika ambavyo ni vyama vya siasa, badala yake ikajumuishwa na CHADEMA katika kapu hilo.
“CHADEMA tuna hadhi yetu, ni chama makini, hatuachi mambo yaende yalivyo, ndiyo maana kuliko kuanza kujibizana na mtu mmoja mmoja katika simu, tumewaita waandishi ili kutoa taarifa hii kwa umma kuwa taarifa ya PAC si sahihi,” alisema.
Alisisitiza kuwa kama kweli tangu mwaka 2009 hesabu hazijakaguliwa, basi aulizwe CAG, ofisi yake inafanya nini ikiwa fedha zinatolewa mwaka wa kwanza hazikaguliwi hadi mwaka wa nne.
“Ofisi ya CAG ituambie wanafanya kazi gani, kwanini wanaendelea kutoa ruzuku kama hesabu hazikaguliwi?
“Sisi CHADEMA tuko wazi, tunapopata hata misaada kutoka nje huwa tunamuarifu msajili, maana yake ni hatari kama chama kinapokea misaada hakisemi kwa msajili,” alisema.
Komu aliongeza kuwa chama kinaweza kupokea hata misaada ya Al- Shabaab au mambo mengine kama ya EPA, ndiyo maana wanawataka PAC waende mbele zaidi ili utaratibu wa uwazi uende kwenye vyama vyote kama wanavyofanya CHADEMA.
“Tulipata fedha kutoka Denmark ukiwa msaada kwa ajili ya kujenga uwezo, tulimwandikia msajili, naye akatujibu kwa barua Na. DA/112/123/16a/10 ya tarehe 19, Agosti 2013.
“Tunashukuru kwa taarifa hii ambayo ni sehemu ya utekelezaji wa Sheria ya Vyama vya Siasa,” ilisomeka barua hiyo.
Juzi, vyama vya CCM, CUF na NCCR-Mageuzi navyo vilimjia juu Zitto vikidai anatafuta umaarufu, kwani hesabu zao zimekaguliwa.
Zitto azidi kukomaa
Alipotafutwa kujibu ufafanuzi huo wa vyama, Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini na Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, alisema vinapoteza muda kuongea na waandishi, badala yake viongozi wao wajiandae kujieleza mbele ya kamati yake.
“Wanapoteza muda tu. Badala ya kufanya mikutano na waandishi, wajiandae kujieleza mbele ya kamati, niweke wazi utaratibu wa kisheria.
“Vyama vinapewa ruzuku, vinafunga mahesabu ya mwaka, vinawasilisha mahesabu kwa mkaguzi. Akishakagua vyama vinawasilisha hesabu zilizokaguliwa kwa msajili, naye anachapisha mahesabu kwenye gazeti la Serikali (GN),” alisema.
Zitto alisisitiza kuwa hadi kufikia juzi, hakuna chama ambacho kilikuwa kimepeleka mahesabu yaliyokaguliwa kwa msajili.
Alisema kuwa PAC inasimamia sheria, hivyo kumuonya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, aliyemshambulia, akisema aache kelele wakati kamati hiyo ikiwa inamsubiri Katibu Mkuu wake, Abdulrahaman Kinana kuhojiwa.
Zitto alisema yupo tayari kunyongwa akitetea masilahi ya umma, huku akiwataka viongozi wa CHADEMA na CCM kutoendeleza malumbano kuhusiana na hoja ya zuio la ruzuku, la sivyo atawafunga.
Akizungumza na waandishi, alisema vyama hivyo vinatakiwa kufika mbele ya kamati yake Oktoba 25, mwaka huu.
Zitto alisema anayo mamlaka kama mwenyekiti wa kamati hiyo kuwafunga jela wote wanaoendeleza malumbano hayo ilhali agizo lilishatolewa, na kusema kuwa hilo ni onyo kwa CHADEMA na CCM, aliodai ni vinara wa malumbano.
“Mimi sifanyi siasa hapa, natekeleza jukumu langu kama mwenyekiti wa kamati, kwa hiyo hili ni onyo kwao, nipo tayari kunyongwa nikitetea masilahi ya umma,” alisema.
Alieleza kuwa ni vema vyama hivyo vikapeleka ripoti kwa msajili na kuachana na malumbano yasiyo na tija, huku akiwashukia waliokuwa wakidai kuwa anatafuta umaarufu kwa maelezo kuwa tayari ni maarufu.
Alisema vyama hivyo vinavyotakiwa kufika kwenye kamati yake ni CCM, TLP, CHADEMA, NCCR-Mageuzi, UDP, CUF, APPT-Maendeleo, UPDP na Chausta.
Aliwataka wanasiasa kutochukulia suala hilo kama ni la Zitto binafsi bali limeamuliwa na Kamati ya Bunge.
Alifafanua kuwa anafahamu fika kuwa ana masilahi katika hilo, kwa kuwa ni Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, lakini uamuzi alioutoa ni kwa niaba ya kamati na si binafsi.
Zitto alisisitiza kuwa katika kipindi cha miaka minne iliyopita, ofisi ya msajili pamoja na waliokuwa wajumbe wa kamati hiyo kabla yake, walikuwa wakiogopa kuviwajibisha vyama hivyo.
Alisema inashangaza kuona katika hicho, msajili hakuwahi kuitwa katika kamati wala suala la ruzuku za vyama kuzungumziwa.
Vyama hivyo vinadaiwa kutowasilisha ripoti hiyo kwa miaka minne kuanzia mwaka 2009, ambapo tayari serikali imeishavilipa jumla ya sh bilioni 67.7 kama ruzuku.
Ruzuku hiyo imelipwa kwa CCM sh bilioni 50.9, CHADEMA sh bilioni 9.2, CUF sh bilioni 6.3 na NCCR-Mageuzi sh milioni 637.
Vingine ni UDP sh milioni 333, TLP sh milioni 217, DP sh milioni 3.3, APPT-Maendeleo sh milioni 1.1 na Chausta sh milioni 2.4.

No comments:

Post a Comment