Tuesday, October 15, 2013

Tuzo ya Mo Ibrahim yakosa mshindi tena

Mo
Wakfu wa Mo Ibrahim ambao humzawidi Rais mstaafu aliyeonyesha uongozi mzuri umesema hakuna kiongozi wa Afrika aliyetosha kutuzwa mwaka huu.
Hata hivyo utafiti wa wakfu wa Mo umeonyesha kuwa Afrika imepiga hatua pakubwa tangu mwanzoni mwa karne hii katika maswala ya uongozi.
Tuzo hiyo haijapata mshindi kwa miaka minne mfululizo tangu kuzinduliwa kwake miaka saba iliyopita.
Katika mkutano na waandishi wa habari mjini London, wakfu wa Mo umesema kuwa baada ya ukaguzi kufanyika hakuna hata kiongozi mmoja alistahili kutuzwa.
Tuzo hiyo ambayo hutolewa na mfanyabiashara bilionea mzaliwa wa Sudan na raia wa Uingereza, Mo Ibrahim hutoa dola milioni 5 kwa kipindi cha miaka kumi na dola laki mbili kila mwaka hadi kiongozi huyo atakapofariki. Na pia dola laki zingine mbili hutolewa kwa mradi wowote unaoungwa mkono na mshindi wa tuzo hiyo kwa kipindi cha miaka kumi.
Hata hivyo, kwa mujibu wa takwimu za wakfu huo, kuna baadhi ya sehemu ambapo hali bado ni mbaya ikiwemo kutii sheria.
Wakfu huo wake Mo Ibrahim tajiri mkubwa sana mwenye uraia wa Sudan ulianza kutoa takwimu zake kuhusu utawala barani Afrika mwaka 2007.
Katika mwaka ambapo Afrika ilisherehekea miaka hamsini tangu kuzinduliwa kwa muungano wa nchi za Afrika, AU. Kwa mujibu wa utafiti wa wakfu wa Mo Ibrahim, mustakabali wa Afrika sio mbaya.

Washindi wa tuzo ya Mo

2005 Joaquim Chissano: Msumbiji
2008 Festus Mogae : Botswana
2011 Pedro Pires : Cape Verde
Asilimia tisini na nne ya waafrika sasa wanaishi katika nchi ambayo angalau imeonyesha uongozi umeimarika tangu mwaka 2000.
Nchi 18 kati ya hamsini na mbili, zilionekana kupata alama nzuri tangu mwaka 2007.
Utafiti huu unaanganzia mambo kadha kwa kadha kama vigezo vya utawala mzuri ikiwemo, ukuwaji wa uchumi , afya na sheria.
Taifa lililopata alam,a nzuri kuliko zote ni Mauritius,ikifuatiwa na Botswana na Cape Verde.
Mataifa yaliyoshika mkia ni pamoja na Eritrea, DRC na Somalia. Nchi zenye uchumi mkubwa barani Afrika,ikiwemo Afrika Kusini na Nigeria zilishika nambariya sita na 45 mtawalia.
Ripoti ya Mo inaonyesha kuwa mizozo sasa imepungua barani humo kuliko ilivyokuwa mwongo mmoja uliopita.
Hata hivyo, bado kuna tatizo la pengo kubwa kati ya masikini na matajiri na ripoti hiuyo inaonya kuwa ikiwa tatizo hili litapuuzwa huenda mizozo zaidi ikaibuka.

No comments:

Post a Comment