Ikiwa yamebaki majuma machache wanafunzi wa kidato cha nne
waanze mtihani wa wa taifa, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi iko
kwenye mchakato wa kubadilisha mfumo wa upangaji za mitihani ya
sekondari na matumizi wa alama za maendeleo ya mwanafunzi (Continuous
Assessment (CA).
Mfumo huo ambao unatarajiwa kuanza kutumika kwenye
Mtihani wa taifa wa kidato cha nne mwaka huu, unakuja ikiwa ni miezi
michache tangu Tume ya Waziri Mkuu iliyoundwa kuchunguza chanzo cha
kufeli kwa maelfu ya wanafunzi waliofanya mtihani wa kidato cha nne
mwaka 2012.
Akizungumzia mchakato huo, Kamishna wa Elimu
Profesa Eustella Bhalalusesa alisema kwamba hatua hiyo imechukuliwa
ikiwa ni sehemu ya kuboresha elimu na kuwa haina uhusiano na taarifa ya
tume iliyoundwa na Waziri Mkuu ambayo mpaka sasa haijawekwa hadharani.
“Mambo yanakwenda yanabadilika hata binadamu
yeyote anabadilika kila siku, mfumo unaotumika sasa hivi ni wa siku
nyingi,” alisema.
Alisema kuwa, ili kuweza kuboresha vyema mfumo huo wameshirikisha wadau mbalimbali zikiwamo shule za sekondari.
“Kama unataka kuboresha lazima upate maoni, lengo
letu ni kushirikisha shule zote za sekondari za Tanzania, ila siwezi
kukuhakikishia kama zote zitashiriki kwa kuwa tunawatumia zaidi maofisa
elimu mkoa na wilaya. Tumeweka pia dodoso kwenye mdandao ili watu zaidi
washiriki.
Kuhusu tume ya Pinda hapa haihusiki kabisa, ile
ilikuwa na mambo yake, hata bila ile tume sisi hii tungefanya tu,”
alisema Profesa Bhalalusesa.
Alisema kuwa, mpaka sasa wameshapokea zaidi ya asilimia 60 ya maoni hayo kutokana na lengo walilo jiwekea.
Dodoso hilo ambalo pia Mwananchi imefanikiwa
kuliona, linasema kuwa serikali inakusanya maoni ya wadau wa elimu
kuhusu Upangaji wa Viwango vya Alama (Grade Ranges) katika mitihani ya
kuhitimu kidato cha nne na cha sita pamoja na matumizi ya ‘Alama
Endelevu ya Mwanafunzi [Continuous Assessment (CA)].
“Serikali imeamua kukusanya maoni haya kwa sababu
kwa muda mrefu sasa upangaji wa viwango vya alama vinavyotumika katika
mitihani ya kuhitimu kidato cha nne na kidato cha sita havifanani pamoja
na kwamba mitihani hiyo yote ni ya elimu ya sekondari.
Pia mfumo wa elimu ya sekondari umekuwa na miundo
tofauti ikiwemo ule unaotumika shuleni na ule wa Baraza la Mitihani la
Taifa (Necta),” sehemu ya dodoso inasema.
Dodoso hilo linafafanua kuwa, muundo wa kwanza ni
ule wa shule ambao alama mgando (Fixed Grade Ranges) ambao alama
zinazotumika kupanga madaraja: A = 81 – 100; B = 61 – 80; C = 41 – 60; D = 21 – 40 na F = 0 – 20.
Muundo wa pili ulioidhinishwa kutumiwa na Necta kuanzia mwaka 2012 ni Upangaji wa Alama Mgando usiobadilika (Fixed Grade Range).
Kwa kidato cha nne alama zilizotumika ni A = 80 – 100, B = 65 – 79, C = 50 – 64, D = 35 – 49 na F = 0 – 34.
Kwa upande wa kidato cha sita alama zilizotumika
ni A = 80 – 100; B = 75 - 79; C = 65 – 74; D = 55 – 64; E = 45 – 54; S =
40 – 44 na F = 0 – 39.
Kwa mujibu wa dodoso hilo, alama zinazopendekezwa ni A = 81 – 100, B = 61 – 80, C = 41 – 60, D = 21 – 40 naF = 0 - 20.
Utaratibu mwingine ambao washiriki wanapaswa
kuchagua ni A = 80 – 100, B = 65 – 79, C = 50 – 64, D = 35 – 49 na F = 0
– 34 huku utaratibu wa tatu ukiwa A+ = 91 – 100, A = 81 – 90, B+ = 71 -
80, B = 61 - 70, C+ = 51 – 60, C = 41 – 50, D+= 31 – 40, D = 21 – 30, E
= 11 – 20 na U = 0 – 10.
Akisoma Kauli ya Serikali Bungeni kuhusu Taarifa
ya Awali ya Tume ya Taifa ya Kuchunguza Matokeo ya Mtihani wa Taifa wa
Kidato cha Nne mwaka 2012, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Wiliam
Lukuvi alisema kuwa matokeo yaliyotangazwa awali na Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi yafutwe na yapangwe tena kwa kutumia mfumo
uliobadilika mwaka 2011 kama ilivyopendekeza tume ya Waziri Mkuu Mizengo
Pinda.
Hata hivyo, baada ya kufutwa kwa matokeo hayo na
kupangwa upya, Waziri wa Elimu Dk Shukuru Kawambwa alisema kuwa
utaratibu uliotumika kupanga matokeo hayo mapya ni uleule uliotumika
kuandaa matokeo yaliyofutwa wa Fixed Grade Ranges.
“Kuanzia sasa matokeo ya mtihani ya kidato cha nne
na sita yatachakatwa kwa kutumia Fixed Grade Ranges na Standardization
(alama zisizobadilika na kuuwisha alama za mitihani),” alisema Kawambwa.