KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk.
Willibrod Slaa, amesema anamvutia pumzi Spika mstaafu wa Bunge, Samuel
Sitta, juu ya kauli yake kuwa chama hicho hakina viongozi wa kutosha
kufanya kazi ya serikali.
Sitta ambaye pia ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki na
mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, alitoa kauli hiyo juzi wilayani
Karagwe, Mkoa wa Kagera, alipotembelea ofisi za chama chake, akisema
CHADEMA haina kiongozi zaidi ya Dk. Slaa.
Sitta alikwenda mbali zaidi akisema kuwa CHADEMA ina viongozi wenye
uzoefu wa kuongoza kumbi za muziki na kwamba Mwenyekiti wa chama hicho,
Freeman Mbowe, ni mjuzi wa disko za usiku.
Akizungumza na Tanzania Daima mjini Iringa jana, akiwa katika
mwendelezo wa Operesheni ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C), Dk. Slaa,
alisema tuhuma hizo ni nzito na lazima azipitie kwa umakini ili aweze
kuzitolea maelezo.
“Nimesoma juu ya hizo taarifa na kama Sitta ninayemheshimu, amefikia
kumuita mwenyekiti wetu mtaalamu wa kuongoza disko, si kauli nyepesi,
hiyo ngoja tuichambue na leo au kesho tutatoa tamko zito juu ya hilo,”
alisema Dk. Slaa.
Aliongeza kuwa Sitta ambaye ni Mbunge wa Urambo Mashariki alitoa kauli
hiyo akiwa katika jukwaa la siasa, hivyo naye anatafakari kama amjibu
akiwa jukwaani au aitishe mkutano na waandishi wa habari.
No comments:
Post a Comment