Thursday, February 28, 2013

Mkondo wa lala samala nchini Kenya

Kinyang'anyiro, cha uchaguzi utakaofanyika Jumatatu kinaingia mkondo wa lala salama hii leo, na Ijumaa huku wagombea wakienda kwenye majimbo kuwaomba watu kura.
Kura za maoni zinaonyesha ushindani mkali kati ya mgombea Uhuru Kenyatta wa Jubilee na Raila odinga wa CORD.
Mshindani anayewafuata ni Musalia Mudavadi wa muungano wa Amani na anashikilia nafasi ya tatu nyuma ya wawili hao kulingana na kura za maoni.
Kwa mgombea kushinda uchaguzi lazima apate zaidi ya asilimia hamsini na takriban asilimia 25 ya kura katika nusu ya majimbo 47.
Miungano ambayo inaongoza kwenye kura zamani inatumia mbinu mbali mbali kuwashawishi wapiga kura kujitokeza siku ya kupiga kura.
Muungano wa Cord wake, Raila Ofinga, ulisema kuwa unawataka watu 330,000 kuwaombea kura kwa wapiga kura kote nchini.
Bwana Kenyatta amekuwa akiwashawishi wapiga kura kupiga kura mapema kabla ya kuelekea kazini na makwao wakati mgombea mwenza wake William Ruto,amewataka vijana kuhakikisha kuwa marafiki zao na jamaa zao wameweza kupiga kura.
Jimbo la Rift Valley, moja ya majimbo makubwa, ina kauti 14 ikiwa na wapiga kura milioni 3,373,853. Eneo hilo linatazamiwa kama ngome ya William Ruto.
Utafiti wa mwisho uliofanywa kuhusu maoni ya watu kuwahusu wagombea wakuu, ulionyesha kuwa Kenyatta angemshinda Raila asilimia 60 kwa asilimia 23.
Pande hizo mbili hata hivyo zina matumaini ya kuibuka mshindi.
Kwa upande wake, Muungano wa Jubilee wake Kenyatta umeelezea matumaini makubwa, ukitaka kushinda kiwango kikubwa cha kura.
Mkoa wa kati ndio wa pili wenye idadi kubwa zaidi ya wapiga kura na eneo hilo ni ngome ya Uhuru Kenyatta.
Kura zote za maoni, zinawaweka zinaonyesha kuwa Kenyatta anaweza kushinda asilimia tisini ya kura katika eneo hilo.

Kamanda Mbowe ndani ya Mbeya maandalizi ya uzinduzi Kanda ya Nyanda za Juu Kusini

MWENYEKITI wa Taifa, Freeman Mbowe leo ameingia Jijini Mbeya, kwa ajili ya vikao vya ndani kwa ajili ya maandalizi ya uzinduzi wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (Ruvuma, Njombe, Iringa na Mbeya) utakaofanyika kesho kwenye Viwanja vya Dkt. Slaa (zamani Mama John), ikiwa ni mwendelezo wa mikutano ya ndani na hadhara kutekeleza maamuzi ya Baraza Kuu la CHADEMA, kuielezea dhana ya uendeshaji wa chama kupitia kanda ambayo lengo lake kuu ni kushusha mamlaka ya uendeshaji wa chama katika ngazi ya chini, simply decentralization of powers from the centre.

Papa wawili katika mgongano wa kimadaraka

 
YAMETIMIA. Safari ya miaka saba ya Baba Mtakatifu Benedict XVI inakamilika leo pale atakapong’atuka rasmi katika uongozi wa Kanisa Katoliki, ifikapo saa 2:00 usiku kwa saa za Italia (saa 4:00 usiku kwa saa za Tanzania).

Kwa siku mbili, Papa amekuwa na shughuli nyingi katika makao yake, Gandolfo Castel, Vatican akijiandaa kimwili kuondoka, akiweka sawa nyaraka zake binafsi na zile za kanisa ambazo zitawekwa katika kumbukumbu.

Kwa upande mwingine Vatican, nchi ambayo ipo ndani ya Jiji la Rome iliyozungukwa na ukuta, ikiwa na ukubwa wa hekta 44 na wakazi 832 pekee, imekuwa katika hekaheka nyingi.
Jana, waumini zaidi ya 50,000 na wengine wengi kutoka sehemu mbalimbali duniani wakiwamo makardinali, maaskofu, mapadri na walei walialikwa kwa shughuli rasmi ya kumuaga kiongozi huyo.

Tofauti na kanuni yake, leo Benedict hatavaa viatu vyekundu kama ilivyozoeleka na badala yake amechagua viatu rahisi vya ngozi vilivyobuniwa Mexico. Alipewa viatu hivyo ikiwa ni zawadi wakati wa ziara nchini humo 2012.

Tangu alipotangaza uamuzi wake wa kung’atuka Februari 11, mwaka huu, utata umegubika nafasi yake katika maisha mapya ndani ya Vatican, akiitwa Papa Mstaafu.

Waumini, wataalamu na hata viongozi mbalimbali wa Kikatoliki wameanza kuhoji ni jinsi gani viongozi wawili (Papa) wataishi, huku wote wakivaa mavazi meupe wakiitwa Papa, wakiishi umbali mdogo kati yao, wakiwa na wasaidizi wengi wanaowahudumia.

Vatican
Nje ya Gandolfo Castel, ulinzi umeimarishwa na vibali vya kuingia Vatican vimesitishwa.
Juzi, Vatican ilitangaza kwamba Papa Benedict XVI atajulikana kama ‘Emeritus Pope’, yaani Papa Mstaafu mwenye cheo cha heshima, akiendelea kuitwa, ‘mtakatifu’ na ambaye ataendelea kuvaa nguo nyeupe.

Mavazi na hata jina lake jipya ni masuala ambayo yamezua uvumi mwingi, huku suala la mrithi wake mpya pia likiwa gumzo, kwani tukio kama hilo lilitokea miaka 600 iliyopita.
Ni uamuzi uliolishtua kanisa hilo lenye waumini 1.2 bilioni duniani na wengi wanasema awali, haikushauriwa Papa kustaafu kwani kwa kufanya hivyo kunaacha mizozo na minong’ono ya kuwania madaraka.

Hata hivyo, uongozi wa Vatican umesisitiza kuwa uamuzi huo wa Papa Benedict XVI ni wa kipekee na hakuna mzozo ambao utatokea baina yake na mrithi wake ambaye mchakato wa kumpata unatarajiwa kuanza ndani ya wiki mbili zijazo.

“Kulingana na mabadiliko katika kanisa letu, kuna Papa mmoja. Ni dhahiri kwamba katika hali ya sasa hakutakuwa na tatizo,” anasema Mhariri wa Gazeti la L’Oservatore Romano linalomilikiwa na Vatican, Giovanni Maria Vian.

Hofu iliyopo
Hata hivyo, wakosoaji wa mambo hawakubaliani na hoja hiyo na baadhi ya makardinali walioko Vatican kwa usiri mwingi, wanazungumzia suala hilo wakieleza kwamba litazua tatizo kubwa kwa Papa ajaye, hasa ikiwa mtangulizi wake, Benedict akiwa bado hai.

Mtaalamu wa tauhidi (theolojia), raia wa Uswisi, Hans Kueng ambaye amekuwa mtu wa karibu wa Papa Benedict XVI, ingawa kwa sasa ni mkosoaji wake amesema:
“Kwa sasa, Benedict XVI akiwa bado hai, kuna hatari ya kuwa na Papa kivuli, mwenye mamlaka kamili ambaye kwa chinichini anaweza kumshinikiza mrithi wake kufikia uamuzi.”
Hans Kueng alisema hayo alipozungumza na Gazeti la Der Spiegel la Ujerumani.

Msemaji wa Vatican, Padri Federico Lombardi alisema Papa Benedict XVI kwa upande wake aliamua aitwe Papa Mstaafu au ‘kiongozi mstaafu wa Roma.’ Anasema haelewi ni kwa nini ameamua kuacha jina lake la sasa la Askofu wa Rome.

Kwa wiki mbili zilizopita, maofisa mbalimbali wa Vatican wamekuwa wakifikiri kwamba Papa angeanza kuvaa mavazi meusi na kutumia jina la Askofu Mstaafu wa Rome ili kuepuka mkanganyiko na mrithi wake.

Mtanzania apewa uwaziri Rwanda

 
RAIS Paul Kagame wa Rwanda amemteua Mtanzania, Profesa Silas Rwakabamba kuwa Waziri wa Miundombinu wa nchi hiyo katika mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yaliyofanyika Jumatatu iliyopita.

Kabla ya uteuzi huo, Profesa Rwakabamba alikuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Rwanda. Ni mmoja wa mawaziri wanaoingiza sura mpya katika Baraza la Rais Kagame ambalo amelifanyia mabadiliko kwa kuunda wizara nyingine mpya.

Sura nyingine mpya katika Baraza hilo ambalo liliapishwa juzi Ikulu ya Rwanda ni pamoja na Seraphine Mukantabana (Wakimbizi na Menejimenti ya Maafa) na Oda Gasinzigwa (Ofisi ya Waziri Mkuu- Familia na Jinsia).

Akizungumza kwa simu na mwandishi wetu jana, mdogo wa Profesa Rwakabamba, Timothy Rwamushaija anayeishi Dar es Salaam, alisema ndugu yake alizaliwa katika Kijiji cha Bushagara, Wilaya ya Muleba mkoani Kagera.

Alisema Profesa Rwakabamba alikuwa Mtanzania aliyeamua kuchukua uraia wa Rwanda na wote baba yao ni Mzee Titus Rwamushaija... “Huyu ni kaka yangu wa tumbo moja na kwa kweli tumefurahi sana kwa mafanikio yake sisi kama wanafamilia.”

Naibu Makamu Mkuu - Taaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM), Profesa Makenya Maboko alisema Profesa Rwakabamba alifanya kazi katika chuo hicho na aliondoka akiwa Mkuu wa Kitivo cha Uhandisi.

“Aliondoka wakati Kagame alipoingia madarakani na alikwenda kuongoza Taasisi ya Teknolojia ya Kigali (KIST) kabla ya kwenda katika Chuo Kikuu cha Kigali,” alisema Profesa Maboko.

Msomi huyo alikwenda Rwanda mwaka 1997, baada ya kuombwa na Rais Kagame ambaye alikwenda UDSM kuwaomba baadhi ya wahadhiri kwenda Kigali kufungua chuo kikuu katika taifa lake baada ya kumalizika vita ya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1994.

Profesa Rwakabamba alikuwa Mkuu wa kwanza wa KIST na kukifanya kuwa miongoni mwa vyuo bora barani Afrika kwa masuala ya teknolojia jambo lililomfurahisha Rais Kagame.

Baada ya mafanikio hayo, Rais Kagame alimteua kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Rwanda, Butare ambako pia alijizolea sifa baada ya kusimamia vyema ujenzi wa mabweni kwa wingi na kiongozi huyo alimtunukia uraia wa nchi hiyo kama zawadi.

Hata hivyo, Profesa Rwakabamba atakuwa amelazimika kuukana uraia wa Tanzania kwa kuwa katiba ya nchi hairuhusu uraia wa nchi mbili.
Profesa Rwakabamba alipata elimu ya msingi huko Muleba na akajiunga na Shule ya Sekondari ya Ihungo.

Baada ya hapo, alijiunga na Chuo Kikuu cha Leeds, Uingereza na kupata Shahada ya Uhandisi mwaka 1971 na 1975 alipata Shahada ya Uzamivu katika fani hiyohiyo.

Zaidi ya 1000 wajiunga CHADEMA

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kupitia kikosi kazi chake cha Vuguvugu la Mabadiliko (M4C), Kanda ya Ziwa, kimefanikiwa kuzoa zaidi ya wanachama wapya 1,000, wengi wakitokea Chama cha Mapinduzi (CCM).

Wakizungumza na Tanzania Daima jana wilayani hapa, viongozi waandamizi wa M4C Kanda ya Ziwa, Husina Amri Saidi, na Alfonce Mawazo, walisema M4C imedhamiria kujikita zaidi maeneo ya vijijini.

Walisema baadhi ya wananchi hao walipatikana katika mikutano yao iliyofanyika kisiwa cha Bumbile, kata ya Bumbile, jimbo hilo la Muleba Kaskazini ambao ni zaidi ya 200 waliojiunga na CHADEMA.

Mbali na hilo alisema zaidi ya wanachama 100 wa CCM walilazimika kurudisha kadi zao na kujiunga CHADEMA.

“Kwa kweli CHADEMA kupitia M4C tumeweza kuzoa wanachama wengi katika visiwa vya Muleba Kaskazini.

“Kisiwa cha Bumbile, kata ya Bumbile, zaidi ya wananchi 200 wamejiunga na CHADEMA kwa kununua kadi kwa hela zao.

“Lakini, wapo zaidi ya wana CCM 100 wamerudisha kadi za ‘magamba’ kisha kuvaa ‘kombati’,” alisema Husina.

Walisema wakiwa katika visiwa vya Lushonga na Mchangani zaidi ya wananchi 438 walijiunga na CHADEMA.

Akizungumzia harakati za CHADEMA katika kuelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2014 na uchaguzi mkuu ujao mwaka 2015, Kamanda wa M4C Kanda ya Ziwa, Mawazo, aliwasihi wananchi wote wa Kanda ya Ziwa na Tanzania kwa jumla kutumia nguvu ya umma kuiondoa CCM madarakani kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Mwanafunzi Mbeya anaswa mtandao wizi wa Benki NMB

 
POLISI wilayani Rungwe, mkoani Mbeya, limewanasa watu wanne akiwamo mwanafunzi aliyemaliza kidato cha nne mwaka jana, wilayani Bunda, mkoani Mara, baada ya kukutwa wakiiba fedha Benki ya NMB tawi la Tukuyu kupitia mashine za kutolea fedha (ATM).
Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Chrispin Meela alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 2:30 usiku.
Meela aliwataja watuhumiwa  hao kuwa ni mkazi wa mjini Tukuyu,  Mfanyabishara wa Mbozi, mwanafunzi aliyemaliza kidato cha nne mwaka jana wilayani Bunda na mkazi wa Msasani Tukuyu.
Alisema akiwa nyumbani kwake usiku, alipigiwa simu na msamaria mwema na kuambiwa taarifa za kuwapo watu  wakiwa kwenye mashine hizo za kutolea fedha, huku wakiwa wanatoa fedha mfululizo na aliwatilia shaka.
“Jana  usiku saa 2:30 nilipigiwa simu na msamaria mwema na kuniambia kuwa,  kuna watu wapo Benki ya NMB wanatoa fedha ATM tena mfululilo huko wakiwa na kadi nyingi za ATM,” alisema Meela na kuongeza:“Baada ya kuambiwa hivyo nilimpigia simu OCD (Mkuu wa polisi wilaya), akatuma timu ya makachero eneo ta tukio na wakabahatika kuwakuta na kuwatia nguvuni.”
Meela alisema watuhumiwa  walikutwa wakiwa na kadi bandia za ATM 150 za watu tofautitofauti  na kwamba, hadi wanatiwa mbaroni tayari walikuwa na Sh20.5 milioni mkononi. Alisema kadi zote ni za NMB na kwamba, zilikuwa zinaonyesha  wateja wote ni walimu kutoka wilayani Mbozi.
Alisema baada ya watuhumiwa kuhojiwa  walidai ni wafanyabiashara wanajihusisha na kukopesha fedha walimu, hivyo  katika kuzirejea fedha hizo walimu waliwapatia kadi zao ili waende kutoa  benki.
“Kinachotupa hofu  hapa ni kwamba, kadi zote hizi zinaonyesha wateja kutoka wilayani Mbozi, sasa swali kwa nini waje kutolea fedha hizo wilayani kwetu?” alihoji Meela.
Alisema watuhumiwa wote wapo Kituo cha Polisi Tukuyu kwa mahojiano zaidi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Diwani Athumani alikiri kupata taarifa hizo, lakini alikataa  kulitolea ufafanuzi kwa sababu  wanaendelea na uchunguzi.

Tuesday, February 26, 2013

Utafiti: Dk Slaa aongoza vinara tisa urais 2015

 
WAKATI baadhi ya wanasiasa wakiwa wameanza kujiwinda kwa ajili ya kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, Shirika la Utafiti la Synovate limetoa matokeo ya utafiti wake ambao unaonyesha vigogo tisa kuwamo katika mchuano huo.
Utafiti huo umeonyesha kuwa endapo uchaguzi huo ungefanyika sasa, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Willibrod Slaa angeibuka mshindi baada ya kuongoza orodha hiyo akipata asilimia 17.

Katika matokeo ya utafiti huo uliofanywa Desemba mwaka jana, Dk Slaa anafuatiwa kwa mbali na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambaye amefungana na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe kila mmoja akipata asilimia tisa.

Hata hivyo, licha ya kuongoza, Dk Slaa ameporomoka kwa asilimia 25 ikilinganishwa na matokeo ya utafiti kama huo uliofanywa na taasisi hiyo mwaka 2011 ambapo alipata asilimia 42.

Kadhalika, umaarufu wa Pinda ambaye anaongoza miongoni mwa wagombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), umeshuka kwa asilimia tatu kutoka 12 za mwaka juzi, wakati Zitto ameendelea na kiwango kilekile cha asilimia tisa alizopata katika utafiti uliotangulia.
Wengine wanaofuata na asilimia walizopata kwenye mabano ni Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli (8), Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa (7) na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba (5).

Pia wamo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe (4) ambaye amefungana na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe (4) na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta (2).
Ikilinganishwa na utafiti wa 2011, Lipumba ameporomoka kwa asilimia tisa.
Lowassa amepanda kwa asilimia sita, Dk Magufuli asilimia nne, Mbowe na Membe wamepanda kwa asilimia mbili kila mmoja, wakati Sitta amebaki katika kiwango kilekile cha asilimia mbili.

Hata hivyo, utafiti huo umeonyesha kuwa wananchi ambao hawana uamuzi wa kuchagua mtu yeyote kati ya hao kwa sasa ni asilimia 18, likiwa ni ongezeko la asilimia 12 ikilinganishwa na utafiti uliotangulia.

CCM yatamba
Katika utafiti huo, CCM kimeonyesha kuwa ni chama ambacho asilimia 52 ya wananchi wangependa kujiunga nacho, kikiwa kimepanda chati kwa asilimia moja kutoka asilimia 51 mwaka jana.

Kwa upande wa Chadema, wananchi ambao wanapenda kujiunga nacho imeshuka kutoka asilimia 35 mwaka 2011 hadi 31 mwaka jana.

Uwezekano mkubwa wa CCM kupanda chati ni kutokana na ukweli kuwa mwaka jana kilikuwa na uchaguzi ulioanzia ngazi ya mashina hadi taifa na kuibua vuguvugu kubwa masikioni mwa wananchi.

Chadema hakikuwa na harakati kubwa za kisiasa ukiacha kampeni ya Movement For Change (M4C), ambayo kwa kiasi haikuwa na pilika kama uchaguzi wa CCM.
Chama kingine ni CUF ambacho kimeporomoka kwa kupata asilimia 10 mwaka 2011 hadi nne mwaka 2012.

Hata hivyo, asilimia ya wananchi kutokutaka kujihusisha na chama chochote imepanda kutoka asilimia mbili mwaka 2011 hadi 12 mwaka 2012.

Rushwa
Katika suala la rushwa nchini, utafiti huo umeonyesha kuwa kati ya watu 10 waliohojiwa, wanne walikuwa na maoni kuwa rushwa imeongezeka kufikia asilimia 41, asilimia 30 walisema iko palepale, asilimia 23 walisema imepungua na asilimia tano hawajui.