Friday, April 22, 2016

JPM TUPIA JICHO MFUMO WA ELIMU NCHINI, NI "JIPU" KUBWA ZAIDI YA UDHANIAVYO.!-By Malisa GJ,

Kati ya vitu navyotamani sana kuona vikifanyika ni marekebisho makubwa ya mfumo wa Elimu Nchini. Natamani kuona shule za sekondari za serikali zikirudishwa ktk hadhi yake. "Special schools" ziwe "Special" kweli. Tuone watoto wetu wakipambana kwenda Ilboru, Kibaha, Tabora boys, Mzumbe etc. Sio kupambana kwenda St.Marry's au St.Francis.

Nakumbuka miaka 21 iliyopita kaka yetu alifaulu darasa la 7 kwenda sekondari ya Iyunga (Mbeya) akitokea kule kijijini Old Moshi. Wakati tunamsindikiza kupanda basi alikua anatupa hamasa ya kusoma ili tufanye vizuri zaidi yake. Kipimo kilikua kwenda "special school".
Nakumbuka matokeo ya darasa la 7 au kidato cha 4 yalikua yakitoka tunaenda kujazana ofisi za Halmashauri ya wilaya kuangalia umepangwa wapi. Ruvu, Kigonsera, Kantalamba, Ndanda, Pugu, Magamba, Mwenge, Same, Mazengo au Mzumbe?
KWA WAVULANA: Tabora boys, Songea Boys, Bwiru boys, Nsumba, Lyamungo, Umbwe etc.
KWA WASICHANA: Weruweru, Ashira, Songea girls, Nganza, Loleza, Iringa girls etc.
Zilikuwepo shule za ufundi ambazo zilichukua watu wa daraja la pili la Ufaulu. Yani shule za vipaji ndio zilichukua wale "bright" waliofuata wakaenda shule za Ufundi kama Tanga Tech, Iyunga Tech, Mtwara Tech... Waliofuata wakaenda shule za kawaida za Boarding kama Pugu, Ruvu, Galanos etc.
Waliofuata wakaenda shule za kutwa (day school), ambazo nazo hazikuwa mchezo kupata nafasi. Nakumbuka mdogo wangu alipata alama 120 kati ya 150 yani wastani wa daraja A ya asilimia 81% lakini alipangwa day school (Mawenzi).
Zilikuwepo pia shule maalumu kwa ajili mchepuo wa biashara. Yani ukipita huko unajiandaa kuja kusomea Uhasibu, Masoko, au biashara kwa siku za baadae. Shule kama Umbwe na Shycom zilikua maalumu kwa michepuo ya ECA, EGM etc.
Kwa ujumla serikali ilikua imejipanga vizuri sana ktk sekta ya Elimu. Kuanzia ngazi ya chini kabisa kwa shule za msingi hadi Elimu ya juu.
Na ilitumia mfumo mzuri wa kuhakikisha wanafunzi wanafanya vizuri katika masomo yao. Kwa mfano mashindano ya UMITASHUMTA na UMISETA yalisaidia sana kuinua kiwango cha Taaluma na michezo. Wanafunzi walishindanishwa ktk michezo na taaluma pia.
Nakumbuka nikiwa darasa la 6 nilishiriki mashindano ya somo la HISABATI na nikafanikiwa kufika hadi ngazi ya wilaya. Pale ninakutana na vichwa vya "number" nikachujwa japo nilipata 45 ya 50. Waliofanya vizuri wakaendelea ngazi ya mkoa na hatimaye taifa. Na mwishoni alipatikana bingwa wa Hisabati kitaifa.
Mashindano ya sanaa (uchoraji, uchongaji, kusuka etc). Mashibdano ya Insha (darasa la 4), mashindano ya Umahiri ktk lugha ya kiingereza (darasa la 5) ni moja ya mambo yaliyofanya wanafunzi kusoma kwa bidii na kuibua vipaji vyao.
Wengine kwenye michezo kama Riadha, Soka, kuruka viunzi, kukimbia na magunia.. Wenye ktk uimbaji.. kulikuwa na Mashindano ya kuimba (kwaya ya shule) mnatunga nyimbo za kutunza mazingira, kusifia Tanzania au kupiga vita magonjwa kama Ukimwi halafu mnapimwa kwa maudhui ya wimbo na mpangilio wa uimbaji wenu (tone, melody, rythim etc).
Unamaliza shule unakuwa "multi-purpose".. unajua vitu vingi kwa wakati mmoja. Darasani unajua, michezo unajua, sanaa unajua.. yani unaimarika afya ya mwili na akili.
Kila nikitafakari haya yote nawaonea huruma sana wadogo zetu waliopo shuleni. Hawajui zaidi ya wanavyosoma kwenye vitabu.. Na bahati mbaya vitabu vyenyewe vinaandikwa vikiwa na makosa mengi.
Mwamko wa elimu hakuna tena na taaluma imedumaa. Watoto hawaandaliwi kuzikabili changamoto za maisha. Watoto hawaandaliwi kupambana ktk kusaka maarifa. Wanaandaliwa kuona elimu ni kitu cha kawaida na yeyote anaweza kuipata.
Wakati nikiwa darasa la 5 nilikua nimekariri miji mikuu yote duniani, Marais wote wa Afrika (kwa wakati ule), sarafu za nchi zote za Afrika, Marais wa kwanza wa nchi zote za Afrika, vyama tawala vya nchi zote za Afrika, Baraza la Mawaziri lote la Tanzania nikiwa kinda wa miaka 11 tu, lakini nimepigwa na butwaa juzi kuona kupitia EATV (kipindi cha Skonga) mtoto wa kidato cha 4 anaulizwa mji mkuu wa Somalia akajibu 'Al Shabab'
Nikajiuliza huyu amefikaje form four? Tena shule ya serikali. Nikagundua Mfumo wetu wa Elimu uko "loose" na umeruhusu kila mtu kupita tu hata kufika chuo kikuu hata kama hajui kitu.
Hujiulizi inakuaje darasa lina nwanafunzi 70 halafu 69 wanafaulu kwenda sekondari anafeli mmoja tu. How comes? Wakati mimi namaliza darasa la 7 tulikua wanafunzi 97 darasani. Tuliofaulu kwenda sekondari ni 6 tu. Yani wavulana watano na msichana mmoja. Ikawa gumzo kijijini kwamba tumefaulu wengi maana ilikua imezoeleka ni wawili au watatu.
Lakini leo hata asiyejua kusoma yupo sekondari. Na akitaka anafika hadi chuo kikuu. Unabisha?? Nenda UDSM, Mzumbe, SAUT au UDOM fanya "rundom sampling" upate mwanafunzi mmoja kisha mwambie akutajie jina la sarafu ya Zambia, Rwanda, Namibia, au Congo. Kama asiposaidiwa na "Google" nakuhakikishia atapata sifuri.
Au muulize akutajie marais wa kwanza wa nchi 5 za Afrika Mashariki.. Yani Rwanda, Kenya, Uganda, TZ na Burundi. Akijitahidi sana atakutajia Nyerere na Mzee Kenyatta. Wengine hadi asaidiwe na "google".. wadogo zetu hawasumbui tena vichwa kusaka maarifa.. wao busy "instagram, facebook na whatsapp" kila saa wanatupia picha.
Hizi simu wa gezitumia vzr zingewasaidia sana kusaka maarifa lakini hawana muda huo. Wanataka kuona "mastaa" wa bongo movie wanasema nini Insta. Wako busy kufuatilia maisha ya Diamond na Zari kuliko kufuatilia masomo.
Elimu yetu imefubaa... Elimu yetu imedumaa.. Elimu yetu inaugua kiharusi.. Tunahitaji kuchukua hatua madhubuti kuiokoa ili irudi ktk hali yake ya awali.
Bahati mbaya Viongozi wetu wamerahisisha sana elimu na ikaonekana ni kitu "cheap". yani elimu ni haki ya la kila mtu anayetaka.. Hata kama huna uwezo lakini ukitaka degree unaipata tu.. ili mradi uwe na fedha..
Ndio maana leo kuna vyuo vinatoa degree vipo jirani na garage, au stand za mabasi.. Unasikia chuo kinatangazwa kwenye vyombo vya habari kwamba kinatoa degree au diploma lakini kipo karibu na soko la Mitumba, au jirani na kituo cha daladala, mkabala na gereji au nyumba ya kulala wageni.
Na wanaotoka hapo wanaitwa wasomi. Wana vyeti vinavyopendeza sana. Wana GPA nzuri sana. Lakini wape kazi wafanye au wapime katika maarifa waliyonayo. Utajiuliza hivyo vyeti walisomea au wameviokota?
Mfumo wa Elimu duniani kote unapaswa kuwa pembetatu.. Yani wanaoanza ni wengi lakini kadri wanavyoenda juu idadi inapaswa kupungua. Kama shule za msingi wanafunzi ni laki 5 basi sio wote watakaoenda sekondari. Kama mwanafunzi hana uwezo wa kwenda sekondari atafutiwe shughuli nyingine ya kufanya. Sekondari waende wenye sifa na uwezo tu.
Na watakaoenda sekondari si wote watahitimu.. wengine watachujwa kidato cha pili wakatafute shughuli za kufanya.. wengine wataendelea lakini wakifika kidato cha 4 si wote watakaoenda kidato cha 5. Hivyohivyo hadi chuo kikuu.
Chuo kikuu sio haki ya kila mtu na haipaswi kuwa haki ya kila mtu. Ni kwa "wateule" wachache tu. Vyuo vya kati (Polytechnic) vinapaswa kuwa vingi maana ndio vinatoa watendaji lakini vyuo vikuu vinapaswa kuwa vichache maana vinatoa wasimamizi (managers). Na hivi ndivyo Mwalimu Nyerere alivyofanya.
Kwa mfano vyuo vya Ufundi vilikua vingi lakini chuo kikuu kimoja. Kwahiyo kama kuna kampuni ya Ufundi umeme unakuta Kuna Electrical Engineer mmoja mwenye degree huyu anakuwa Meneja. Halafu chini yake kuna mafundi sanifu (Technicians wa level za diploma), halafu chini kabisa kuna mafundi mchundo (Artisan) wa level za certifice kutoka VETA au vyuo vingine vya ufundi.
Kimsingi "mafundi sanifu" na "mafundi mchundo" ndio watenda kazi. Hawa ndio wanaingia "field". Kwahiyo "degree holder" yeye anawasimamia tu ili wafanye kazi inavyotakiwa.
Kwa kawaida "degree holders" wengi wanajifunza kwa nadharia zaidi si vitendo (isipokuwa kwa baadhi ya course kama MD, Law, Journalism etc). Kwa hiyo ukiwa degree holder wewe ni msimamizi (manager). Unajua kitu kinatakiwa kifanyikeje lakini hufanyi wewe. Kwa hiyo unawekwa msimamizi kusimamia wengine wafanye.
Lakini siku hizi imekuwa vice-versa. Unakuta kampuni ya umeme ina degree holder 18 wa Electrical Engineering na Diploma holder wawili. Sasa hapo nani anaingia "field?", nani anamsimamia, nani anasimamiwa?
Na tatizo lilianza baada ya serikali kurahisisha elimu na kuona ni haki ya kila mtu. Vyuo vyote vya ufundi daraja la kati vilivyokuwa vikitoa Technician wazuri kama Mbeya Tech, DIT na Arusha Tech vikageuzwa kisiasa na kuanza kutoa degree. Kwahiyo wahitimu wa DIT wakimaliza hawashiki tena spanner maana wao sio "Technicians" tena. Wana degree kwahiyo nao wanataka kuvaa tai au suti wakae kwenye viyoyozi.
Mfumo wetu wa Elimu umepinduka miguu juu kichwa chini. Wanaojiita wasomi wa "Degree" (managers) wamekuwa wengi kuliko wasomi wa taaluma za kati (implementers). Na hii ni tatizo kubwa. Huwezi kuwa na Managers wengi kuliko watendaji. Wanam-manage nani sasa?
Ukiona taifa lina wasomi wengi wa vyuo vikuu na upungufu wa wasomi wa vyuo vya kati ujue taifa hilo halizalishi. Limedumaa kwa sababu Wanaofanya uzalishaji ni wataalamu wa ngazi za kati. Wasomi wa vyuo vikuu ni wasimamizi tu. Sasa tumefanya kila mtu kuwa msimamizi, je nani awe mzalishaji?
Ndio maana Wachina wakija kujenga barabara wanakuja na mafundi sanifu (Technicians) kutoka kwao halafu tunaanza kulalamika kuwa ajira zetu wanapewa wageni. Mnalalamika nini wakati mafundi sanifu hakuna? Vyuo vya kutengeneza mafundi sanifu mmevigeuza vyuo vikuu, sasa hivi vinazalisha wasimamizi (managers) badala ua kuzalisha watendaji?
Nchi hii ina vyuo vikuu kama utitiri. Ukipitia taarifa ya TCU na ukapitia ya NACTE utagundua nchi hii ina vyuo 64 vinavyotoa elimu ya juu kwa ngazi za "degree" na kuendelea. Vingine ni "Universities" vingine ni "Non university institutions".
Hivi vyuo vyote hivi vinatoa elimu kwa ubora unaotakiwa? Sina shida na idadi ya vyuo ila standard ya elimu inayotolewa huko. Tunazalisha wasomi wa viwango vya kukubalika kimataifa? Au tumetanua goli kila mtu apite.?
Nilienda Songea nikakuta Chuo kikuu kinaitwa St.Joseph (nashukuru serikali imeshakifunga) yani nikasikitika sn. Chuo kikuu kinazidiwa majengo na shule ya msingi Vingunguti A??
Chuo hakina maabara, hakina maktaba, hakina hostels, hakina sifa hata ya kuwa shule ya sekondari. Labda shule ya msingi kwa shida. Lakini ni chuo kikuu na wadogo zetu walipelekwa huko na TCU.
Vipo vyuo vingi vya aina hii. Serikali ifanye ukaguzi upya ivifunge. Heri tuwe na vyuo vichache vyenye "standard" ya kueleweka kuliko kuwa na mavyuo mengi yasiyo na tija. Kuna haja gani ya mwanafunzi kujiita ana degree wakati hata CV hawezi kuandika?
Juzi nilikuwa kwny pannel ya usaili wa nafasi fulani za kazi nikamwambia mmoja wa wadahiliwa ajieleze kwa dakika mbili lakini akaishia kutaja jina lake na umri wake tu. Mwingine akataja degree yake (Business Information System) tukamuuliza hiyo degree ni ya Social science, Pure Science au Business afiliated? Akashindwa kujibu akaomba kuangalia kwenye cheti chake imeandikwaje. Nikashangaa lakini nikamuonea huruma. Ina maana miaka mitatu alisoma kitu asichokijua vzr? Kwa hali hii ni ngumu kushindana kimataifa.
Nina mengi ya kusema lakini ukurasa huu hautoshi kuandika yote.. Itoshe tu kusema Mfumo wa Elimu nchi hii unahitaji marekebisho makubwa sana ya kimfumo. Natamani kuona Magufuli akiumizwa na hili la elimu kama anavyoumizwa na "majipu". Mfumo wa elimu wa nchi hii ndio jipu kubwa zaidi. Tumshauri Rais alitumbue kwa gharama yoyote ile.!
Malisa GJ.!

No comments:

Post a Comment