MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo ( CHADEMA ), Freeman
Mbowe, amepata mapokezi hafifu mjini Mpanda, baada ya kuwasili mjini
hapa. Mapokezi hayo hafifu yamedaiwa kuwa yalisababishwa na mgogoro
uliopo ndani ya chama hicho katika Mkoa wa Katavi.
Kutokana na hali hiyo, Mbowe ambaye aliwasili mjini Mpanda akitokea
Sumbawanga, Mkoa wa Rukwa, alilazimika kuahirisha mkutano wa hadhara
aliopanga kuufanya juzi mjini hapa katika Uwanja wa Kashaulili.
Baada ya kuahirisha mkutano huo, alikutana na viongozi wa Chadema, Mkoa
wa Katavi katika kikao cha ndani kilichokaa kwa saa 11 katika ukumbi
wa Kanisa Katoliki, Jimbo la Mpanda.
Taarifa zilizopatikana kutoka ndani ya kikao hicho zinasema kwamba,
katika kikao hicho, baadhi ya wajumbe walionekana kuwa na hasira kwa
kile walichodai ni kutotendewa haki na baadhi ya viongozi wa chama
hicho, Mkoa wa Katavi.
Taarifa hizo zilisema kuwa, baadhi ya wajumbe hao, walisema kuna kundi
la watu linafanya kila mbinu ili wenzao wafukuzwe uanachama kutokana na
chuki binafsi.
Baada ya Mbowe kuelezwa hayo na mengine, taarifa zinasema alilazimika
kutumia busara zaidi kwa kuwa alijua kama ataamua kukubali uamuzi wa
kuwafukuza baadhi ya viongozi, mgogoro utazidi kukua.
Kutokana na hali hiyo, Mbowe alisema hayuko mkoani Mpanda kwa ajili ya
kuwafukuza viongozi wa chama bali anachokitaka ni kutatua mgogoro
uliopo.
Kuhusu suala la Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ambaye pia ni Mbunge wa
Mlele kupita bila kupigwa wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2010,
alisema uamuzi huo ulifanyika kwa kuwa ulipendekezwa na wazee wa Mkoa
wa Katavi.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, Mbowe alisema lengo la Chadema ni kuweka
mgombea kila panapotakiwa lakini chama hicho kinaweza kisiweke mgombea
kutokana na sababu za msingi zinazojitokeza.
Kwa upande wa chama hicho kutokuwa na ofisi mkoani Katavi, inadaiwa mbowe alisema hilo ni jukumu la wanachama wa mkoa huo.
Pamoja na hayo, Mbowe alizungumzia kikao cha chama hicho cha Kamati ya
Ushauri cha Mikoa ya Katavi na Rukwa kilichokaa mwaka jana wilayani
Nkasi na kumsimamisha uanachama Katibu wa BAVICHA wa mikoa hiyo,
Laurent Mangweshi.
Juu ya kikao hicho, taarifa hizo zinasema Mbowe alisema kikao hicho
hakikuwa na mamlaka kikatiba kutoa uamuzi huo na kwamba Mangweshi bado
ni mwanachama wa chama hicho.
Kutokana na kauli hiyo, Mangweshi alilazimika kuwaomba radhi wajumbe wa kikao na kuwataka wamsamehe popote alipowakosea.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Chadema ambaye pia ni Mbunge wa Mpanda Mjini,
Said Amour Arfi ambaye alitishia kutupa kadi ya Chadema mwishoni mwa
mwaka jana baada ya kutuhumiwa na Mangweshi, kwamba aliwahi kupokea
rushwa kutoka kwa Waziri Mkuu Pinda, alisema amemsamehe kiongozi huyo
wa BAVICHA kwa kuwa ameomba msamaha.
Akizungumza katika mkutano huo, Arfi alisema pamoja na kumsamehe kijana huyo, naye anastahili kusamehewa na yeyote aliyemkwaza.
Mgogoro wa Chadema Mkoa wa Katavi, ulianza mwaka jana baada ya
Mangweshi kumshutumu Arfi, kwamba alipokea rushwa kutoka kwa Waziri
Mkuu Pinda ili apite bila kupingwa. Suala jingine lililosababisha
mgogoro lilikuwa ni juu ya chama hicho kushindwa kujenga ofisi katika
Mkoa wa Katavi.
Chanzo: Gazeti la Mtanzania, Machi 4, 2013
No comments:
Post a Comment