Thursday, March 14, 2013

Kim aanika risasi za kuwakabili Morocco

KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars, Kim Poulsen, jana alitaja kikosi cha nyota 23 kitakachokwaana na Morocco kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Machi 24.
Timu hizo zitakumbana katika mfululizo wa mechi za kuwania nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwakani nchini Brazil.
Kikosi hicho ambacho kimeendelea kumweka kando mshambuliaji Jerry Tegete wa Yanga, kitaingia kambini Jumamosi kusaka makali kuelekea mechi hiyo.
“Wachezaji wanatakiwa kuripoti kambini Jumamosi kwenye Hoteli ya Tansoma kujiandaa na mechi hiyo muhimu kwetu, naufahamu uwezo wa wapinzani wetu,” alisema Kim aliyerejea hivi karibuni akitoka kuwasoma.
Nyota waliomo ni makipa: Juma Kaseja (Simba), Aishi Manula na Mwadini Ally (Azam) na Hussein Shariff (Mtibwa Sugar) aliyeitwa kwa mara ya kwanza.
Mabeki: Aggrey Morris, Erasto Nyoni (Azam), Issa Rashid (Mtibwa Sugar), Kelvin Yondani, Nadir Haroub ‘Canavaro’ (Yanga), Nassoro Masoud Cholo na Shomari Kapombe (Simba).
Viungo: Salum Abubakar na Khamis Mcha (Azam), Athuman Idd na Frank Domayo (Yanga), Amri Kiemba na Mwinyi Kazimoto (Simba) na Shabani  Nditi (Mtibwa Sugar).
Washambuliaji: John Bocco (Azam), Mbwana Samata, Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo - DRC), Mrisho Ngasa (Simba), na Simon Msuva (Yanga).
Mbali ya Kim, benchi la ufundi la Taifa Stars inayodhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia kinywaji chake cha Kilimanjaro linaundwa na Marsh Sylvester (Kocha Msaidizi).
Wengine ni Juma Pondamali (Kocha wa makipa), Leopold Tasso Mukebezi (Meneja), Dk. Mwanandi Mwankemwa (Daktari), Frank Mhonda (Kocha wa viungo) na Alfred Chimela ambaye ni mtunza vifaa.
Kuhusu mechi hiyo, Kim alisema wana uwezo wa kushinda licha ya rekodi ya wapinzani wao ya kuwahi kutwaa ubingwa wa Afrika mwaka 1976 na kucheza Kombe la Dunia.
“Morocco ina wachezaji wengi wanaocheza soka ya  kulipwa Ulaya ila hawanitishi, kwani timu yangu iko vizuri, nimewasoma uwezo wao kwenye Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika, Afrika Kusini, kitu muhimu ni kushikamana,” alisema.
Stars iliyo kundi la tatu, inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi tatu nyuma ya kinara Ivory Coast yenye pointi nne, huku Morocco ikiwa ya tatu kwa pointi mbili na Gambia ni ya mwisho ikiwa na pointi moja.
Chini ya udhamini wa TBL kupitia bia ya Kilimanjaro Premium lager, Stars imekuwa ikipata matunzo na maandalizi ya uhakika, ambapo hivi karibuni ilicheza mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Zambia na kuwafunga bao 1-0.

No comments:

Post a Comment