Monday, March 4, 2013

Jaji Mkuu afanya mabadiliko ya majaji nchini

 
JAJI Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman amefanya mabadiliko makubwa ya majaji katika kanda mbalimbali nchini, huku akiwahamisha wengine na kuwapandisha baadhi kuwa Majaji Wafawidhi.
Habari kutoka kwa vyanzo mbalimbali ndani ya Mahakama Kuu, zinaeleza kwamba Majaji wote watatu waliokuwa wa Kanda ya Moshi wamehamishwa huku aliyekuwa Jaji Mfawidhi, Stella Mugasha akihamishiwa Kanda ya Arusha kuendelea na wadhifa wake.
Majaji wengine waliokuwa chini yake, Crecensia Makuru amehamishiwa Kanda ya Dodoma kuwa Jaji Mfawidhi na Jaji Moses Mzuna naye amepandishwa cheo na kuhamishiwa Kanda ya Mtwara kushika nafasi hiyo.
Habari za uhakika zimeeleza kuwa katika mabadiliko hayo, Jaji Aisha Nyerere aliyekuwa Mfawidhi Kituo cha Arusha amehamishiwa Moshi kuendelea na wadhifa huo.
Hata hivyo, bado majaji watakaosaidiana na Jaji Nyerere katika Kituo cha Moshi hawajatajwa.
Kabla ya kuteuliwa kuwa Jaji na kuhamishiwa jijini Dar es Salaam,  Nyerere aliwahi kuwa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mkoa wa Kilimanjaro.
Katika mabadiliko hayo, Jaji Shaban Lila aliyekuwa Jaji Mfawidhi Mtwara sasa anahamia Dar es Salaam kuwa Jaji Mfawidhi wa Kanda Maalumu ya Ilala ambayo inaanzishwa.
Wengine walioguswa na mabadiliko hayo ni Jaji Maryam Shangali anayetoka Dodoma kwenda Iringa kuendelea na wadhifa wake na Jaji Sekieti Kihiyo anatoka Iringa kwenda Kanda ya Dar es Salaam kuwa Mfawidhi.
Pia Jaji Kakusulo Sambo aliyekuwa Kanda ya Arusha chini ya Jaji Nyerere, amehamishiwa Sumbawanga kuwa Jaji Mfawidhi na Jaji Mwanaisha Kwariko akihamishwa kutoka Dodoma kwenda Songea kuwa Jaji Mfawidhi.
Haikuweza kufahamika mara moja sababu za kufanyika kwa mabadiliko hayo, lakini wafuatiliaji wa medani ya sheria nchini wanaamini uteuzi huo una lengo la kuongeza ufanisi katika idara hiyo ambayo katika siku za karibuni ilitajwa na Taasisi ya Utafiti ya Synovate kuwa miongoni mwa asasi zinazolalamikiwa kwa rushwa.

No comments:

Post a Comment