MKAKATI
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kugatua madaraka kwa
kutafsiri sera yake ya majimbo, umeanza kazi rasmi katika kanda zake 10,
na sasa Kanda ya Ziwa Magharibi imetangaza kikosi kazi kilichosheni
wataalamu wa fani mbalimbali.
Kanda hiyo inayohusisha mikoa ya Geita, Kagera na Mwanza, ilizinduliwa
wiki iliyopita mkoani Mwanza, mbele ya Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa,
Freeman Mbowe.
Mkutano wa uzinduzi wa kanda hiyo uliohudhuriwa na wajumbe wa mabaraza
ya uongozi, wabunge na madiwani kutoka mikoa hiyo, uliwachagua watu sita
kuunda timu ya muda ya uratibu wa kanda kwa miezi mitatu.
Waliochaguliwa kuongoza kanda hiyo ni Peter Mekere (Mwenyekiti), Dk.
Rodrick Kabangila (Makamu Mwenyekiti), Renatus Bujiku (Katibu), Cecilia
Odemba (Mhazini) na Tungaraza Njugu.
Mekere ni mtaalamu mshauri wa biashara na utawala na mafunzo ya
biashara. Ana shahada ya biashara na uongozi na stashahada ya ualimu. Ni
mwenyekiti wa kamati ya fedha na mipango ya Shirika la nyumba la Taifa
(NHC), Kanda ya Ziwa.
Kabangila ni Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Afya, Bugando,
daktari bingwa wa magonjwa ya binadamu na Makamu wa Rais wa Chama cha
Madaktari Tanzania (MAT).
Ana shahada ya uzamili ya magonjwa ya wanadamu, shahada ya udaktari,
shahada ya uzamili, epidemilojia na utafiti wa huduma za afya.
Bujiku ni mwalimu, mtaalamu mshauri, ofisa wa kanda ya ziwa wa shirika
la ACORD kwa muda sasa. Ana shahada ya uzamili, uongozi na mipango,
shahada ya Elimu, Stashahada ya Maendeleo na misaada ya kiutu.
Njugu amekuwa Meneja wa shirika la kijamii (CACT-Mwanza 2008-2010),
meneja wa Chama cha Akiba na Mikopo (MWAUWASA SACCOS 2007 hadi sasa) ana
cheti cha uhasibu kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT) na
cheti cha sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Odemba ni Meneja masoko katika usafiri wa anga, mkurugenzi wa kampuni ya
uwakala ya usafiri wa anga, na amewahi kuwa katibu wa kamati ya
uhamasishaji ya vuguvugu la mabadiliko (M4C) kanda ya Ziwa.
Akizungumza na gazeti hili, Mekere alisema: “Timu yetu imetokana na watu
wenye taaluma mbalimbali ambao wamekuwa wakitafuta nafasi kukisaidia
chama kupitia taaluma zao. Tunaipongeza CHADEMA kwa kuanzisha sera ya
majimbo kuandaa Watanzania kupata maendeleo kwa haraka kwani utaratibu
huu wa majimbo ya chama unarudisha mamlaka kwa wananchi, na ni
maandalizi ya kuongoza nchi.
“Kwa utaratibu huu wananchi wamerudishiwa madaraka yao, wana nafasi ya
kuamua kuhusu rasilimali zao na kupanga namna ya kuzitumia. Utaratibu
huu unaharakisha maendeleo tofauti na mfumo wa kimikoa uliowekwa na
CCM.” |
|
No comments:
Post a Comment