Sunday, October 21, 2012

ni kweli watendaji wa wizara ya nishati na madini hawatuambii ukweli juu ya Tatizo la umeme-Mnyika aweka bayana

 Tunaambiwa hakuna mgao wala tatizo ila wakazi wa moshi na maeneo ya jirani umeme unakata zaidi ya mara5 kwa siku bila taarifa yoyote.

WAZIRI Kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika, ameeleza kusikitishwa na kauli za viongozi na watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini na Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kuhusu hali ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme nchini sanjari na uboreshaji wa utendaji TANESCO.
Amesema kauli hizo zinatoa matumaini potofu kwa wananchi na kuwasihi kuzipokea kwa tahadhari kwa kuwa hazielezi ukweli kuhusu tatizo la umeme nchini.
Mnyika ambaye pia ni mbunge wa Ubungo, alitoa kauli hiyo jana katika taarifa yake kwa vyombo vya habari na kusema kulingana na nyaraka alizonazo za ndani ya wizara hiyo na TANESCO kuanzia Septemba hadi Oktoba mwaka huu, hali ya uzalishaji na usafirishaji na usambazaji wa umeme imekuwa tete kwa sababu mbalimbali ikiwemo upungufu wa upatikanaji wa mafuta na gesi asili kwa ajili ya uendeshaji wa mitambo ya kufua umeme na kasi ndogo ya uwekezaji kwa ajili ya kupata ufumbuzi wa kudumu.
Mnyika pia alisema amemwandikia barua Spika wa Bunge, Anne Makinda, ili Wizara ya Nishati na Madini iwajibike kueleza hali halisi katika mikutano ya kamati za Bunge inayoendelea.
“Katika barua hiyo nimependekeza pamoja na mambo mengine suala la kupokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa mpango wa dharura wa umeme na utekelezaji wa mpango wa uboreshaji wa utendaji wa TANESCO lishughulikiwe na kamati nyingine kwa haraka kwa kuzingatia maelezo na maelekezo ya Spika aliyoyatoa bungeni wakati wa kuahirisha mkutano wa nane wa Bunge,” alisema.
Aidha alisema mapitio ya utekelezaji wa mpango wa uboreshaji wa utendaji wa shirika hilo yahusishe kamati ya kudumu ya Bunge na itakayoeleza hatua iliyofikiwa katika uchunguzi wa tuhuma za ufisadi kwa kuzingatia kuwa siku 60 za uchunguzi zimepita.

No comments:

Post a Comment