Wednesday, October 24, 2012

Matokeo ya uchaguzi wa uvccm yalikuwa hivi na jua watuhumiwa walichokisema

Lukuvi alimtangaza Mbunge wa Donge, Sadifa Juma Khamisi kuwa Mwenyekiti wa UVCCM baada ya kupata kura 483.
Sadifa alimshinda Rashid Simai Msaraka aliyepata kura 263, wakati mgombea mwingine Lulu Msham Abdallah licha ya kujitoa katika kinyang’anyiro hicho muda mfupi kabla ya kura kupigwa, alipata kura nane.
Katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti Mboni Muhita alishinda katika duru ya pili baada ya kupata kura 489 na kumshinda, Paul Makonda aliyepata kura 241.
Katika duru ya kwanza, Mboni alikuwa amepata kura 361 na Makonda kura 206, huku mgombea mwingine Ally Salum Hapi akipata kura 179. Uchaguzi huo ulirudiwa baada ya wagombea wote kutofikisha nusu ya kura kama kanuni zinavyotaka.
“Sheria kushindwa kwa heshima kuliko kushinda kwa fedheha.”
Makonda aliyekuwa akizungumza kwa hisia jukwaani alisema ikiwa UVCCM wanataka kujenga taasisi yenye nguvu na inayoaminika, lazima wahakikishe wanajiepusha na vitendo vya rushwa ambavyo vinaua demokrasia.
“Uchaguzi tulioufanya hatukumchagua Sadifa wala Mboni, bali tumechagua uongozi wa aina ya jumuiya tunayoitaka, sasa tutarajie jumuiya hiyo…. kama sikueleweka historia itakuja kutuambia maana ya maneno haya,” alisema Makonda na kuongeza:
“Kama kuna mtoto wa maskini, mtoto wa mkulima kama mimi amechagua au kupiga kura yake kwa sababu ya rushwa, basi ajue amepanda mbegu maishani mwake.”
Baada ya Makonda kutoa kauli hizo alishuka jukwaani na kwenda moja kwa moja nje ya ukumbi ambako baadhi ya wapambe wake walimfuata na kuanza kulia machozi.
Baadhi yao walisikika wakisema kwamba UVCCM wameisaliti demokrasia kutokana na nguvu ya fedha. Hata hivyo, Makonda alikuwa akiwafariji kwa kuwaambia wasife moyo.
  WATUHUMIWA WAJITETEA HIVII
Kwa nyakati tofauti, wakijibu tuhuma hizo watuhumiwa wote walikanusha kuhusika kutoa rushwa na kuwataka wanaolalamika kupeleka ushahidi wao Takukuru na kufikisha malalamiko hayo katika vikao vya ulinzi na maadili vya CCM.
Shigela kwa upande wake, akizungumza na waandishi wa habari alisema kinachotokea sasa kuhusu tuhuma hizo kilitarajiwa kwani ni kawaida watu wanaposhindwa katika uchaguzi kutoa malalamiko hata kama hawana ushahidi wa tuhuma husika.
Shigela alikanusha yeye na Malisa kutoa fedha kwa viongozi wa mikoa akisema kwa nafasi yake asingeweza kupata fursa ya kufanya hivyo kwani alikuwa mratibu mkuu wa uchaguzi kuhakikisha kila jambo linakwenda sawa.
“Kama kuna watu hawakuridhika kuna taratibu za chama inabidi zifuatwe, kwa mujibu wa taratibu zetu kuna siku 14 za malalamiko na hizo mtu anaweza kuzitumia kuandika malalamiko yake na yapelekwe kwa viongozi wahusika ili wachuke hatua,” alisema Shigela na kuongeza:
“Vinginevyo taratibu za chama haziruhusu kutoa au kupokea rushwa kwa namna yeyote, kwa hiyo kama mtu anadhani ana uwezo aitumikie jumuiya popote pale alipo kwa sababu wote hatuwezi kuwa viongozi kwa pamoja.”
Kwa upande wake, Malisa alisema: “Nimefanya kazi yangu na kutekeleza wajibu wangu kwa ukamilifu, kama kuna jambo lolote ambalo linahusu UVCCM, basi kamuulizeni mwenyekiti wa jumuiya maana yupo.”
Bashe alikanusha kuhusika na vitendo vya rushwa na kuwataka wanaotoa madai hayo, kama wana ushahidi waupeleke Takukuru au kufikisha suala hilo katika vikao vya chama hicho.
“Waambieni kwamba wasilete siasa za shule za sekondari UVCCM, maana kama wangeshinda ni dhahiri kwamba wasingelalamika. Ninawapa ushauri wa bure, kwanza kama wana ushahidi wa madai hayo kwamba mimi Hussein nimetoa rushwa, basi wapeleke ushahidi wao Takukuru lakini pia ndani ya chama tunayo Kamati ya Maadili na Usalama wapeleke malalamiko yao huko ili yafanyiwe kazi.”
Alisema hawezi kujihusisha na rushwa kwani hata Rais Kikwete katika hotuba ya ufunguzi alikemea vitendo hivyo.
Fredy akizungumza kwa simu alisema: “Tuhuma hizo siyo za kweli kwani mimi licha ya kwamba nilipata barua ya mwaliko wa kuhudhuria mkutano huo sikuenda Dodoma kutokana na kubanwa na kazi.
“Kwanza mimi si mjumbe wa mkutano mkuu japokuwa ni Katibu wa Uhamasishaji wa Mkoa wa Arusha. Nilipata mwaliko lakini sikuweza kufika huko (Dodoma) nimetingwa na kazi nyingi,” alisema.

No comments:

Post a Comment