Zanzibar hali tete
Wakati Ponda kafikishwa mahakamani, visiwani Zanzibar hali bado ni 
tete kutokana na wafuasi wa jumuiya ya Uamsho kutanda mitaani na kufanya
 vitendo mbalimbali vya kutia wananchi hofu.
  Ni katika vurugu hizo, askari polisi ameuawa kinyama kwa kupigwa 
mapanga kichwani na mikononi juzi  wakati akirudi nyumbani kutoka kazini
 usiku wa saa 6 .30 eneo la Bububu Zanzibar.
  Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamishna wa Polisi Zanzibar, Musa
 Ali Mussa,  kwa waandishi wa habari, askari aliyeuawa ni F.2105 CPL 
Saidi Abdulrahman wa kikosi cha FFU Mkoa Mjini Magharibi.
  Alisema kuwa inasadikiwa kuwa tukio hilo lilifanywa na wafuasi wa 
jumuiaya ya Uamsho ambayo imekuwa ikifanya vurugu mitaani tangu jana 
ikidai  
  kuwa kiongozi wao Sheikh Faridi Ahmed Hadi ametekwa tangu Oktoba 16, 
mwaka huu.
  Polisi walisema kuwa uchunguzi umeanza kumsaka kiongozi huyo ambapo 
ndugu yake mmoja, Saidi Omar Saidi, anahojiwa kwa vile ndiye aliyekuwa 
naye majira ya jioni wakati walipokwenda eneo la Mazizini kununua umeme.
  Kwamba Sheikh Farid alimuamuru Saidi amuache katika eneo hilo aende 
nyumbani kupeleka umeme wakati akizungumza na watu aliowaita aliokuwa 
nao ndani ya gari aina ya Noah.
  Aliongeza kuwa Saidi alikwenda na aliporudi tena, huo ukawa ndiyo 
mwanzo wa wafuasi wa Shekh Faridi kuanzisha vurugu wakitaka serikali 
imtafute.
  Fujo hizo zilileta hasira ya kuchomwa na kuharibu miundombinu ya 
barabara, kuharibu maskani za chama tawala (CCM) za Kisonge na Muembe 
Ladu kwa kuzichoma moto.
  Pia gari la zimamoto lilivunjwa kioo cha mbele, gari lingine la 
serikali lilivunjwa kioo cha pembeni, huku duka la pombe nalo likivunjwa
 na kuiba mali zilizokuwemo ndani.
  Hadi muda huu watu kumi wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma ya makosa 
mbalimbali yaliyotokana na vurugu hizo. Upelezi wa kujua ukweli juu ya 
uvumi wa kutekwa Sheikh Faridi bado unaendelea.
  Kwa siku nzima ya jana, hali ilikuwa si shwari visiwani hapa, askari 
walikuwa wakiranda katika maeneo yote ya mjini na kutupa mabomu ya 
machozi kwa lengo la  kuwatawanya wafuasi wa uamsho.
  Katika maeneo mengi shughuli nyingi za kibishara zilisitishwa na maduka kufungwa na wanafunzi kutolewa mapema shuleni.
 
 
 
 

 
No comments:
Post a Comment