Saturday, June 7, 2014

Silinde apigania Tunduma kuwa na mamlaka kamili

MBUNGE wa Mbozi Magharibi, David Silinde (CHADEMA), ameitaka serikali ieleze ni lini mji mdogo wa Tunduma utakuwa na mamlaka kamili kabla ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Silinde alisema kuwa mwaka 2011 serikali ilikubali kuwepo kwa kata 14 katika mji ndogo na kwa sasa kuna Mkurugenzi, lakini bado haijawa na mamlaka kamili.
“Naomba serikali ieleze ni lini mji wa Tunduma utakuwa na Mamlaka kamili kwa kuwa tayari zimeishatengwa kata 14 na kuna Mkurugenzi,” alihoji Silinde.
Katika swali la msingi, mbunge wa Karagwe, Gosbert Blandes (CCM), alitaka kujua ni lini kata za Kiruruma na Nyakahanga zitagawanywa kwa kuwa ni kubwa ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa sera ya serikali ya kupunguza ukubwa wa kata na vijiji, ili kurahisisha maendeleo.
Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na  Serikali za Mitaa (Tamisemi), Kasim Majaliwa, alisema ili mji huo uwe na mamlaka kamili ni lazima kuwepo na madiwani katika kata zote 14 tofauti na sasa ambapo yupo diwani mmoja.
Akizungumzia kuhusu kugawa kata na vijiji katika wilaya ya Karagwe ambavyo ni Karuruma na Nyakahanga, alisema vijiji hivyo vinatakiwa kugawiwa kwa mujibu wa sheria husika.
Alisema kata ya Nyakahanga ina wakazi 20,284 na Kata ya Kiruruma inakadiliwa kuwa na wakazi 34,945 kwa mujibu wa sensa na makazi ya mwaka 2012.
Majaliwa alisema kuhusu kugawa kata hizo, Waziri mwenye dhamana na serikali za Mitaa atazigawa kata hizo sambamba na maombi kutoka katika halmashauri nyingine kabla ya uchaguzi wa serikali za mitaa kufanyika.

No comments:

Post a Comment