Saturday, June 7, 2014

Panone FC na safari ya mafanikio ya soka

TIMU ya soka ya Panone FC ‘Matajiri wa Moshi’, ndio mabingwa wa Mkoa wa Kilimanjaro msimu wa 2013/2014, wakipokea kijiti kutoka kwa Machava FC.
Tangu Panone wajitwalie taji Machi 30 kwa kuwafunga Machava bao 1-0 katika mechi ya aina yake iliyochezwa Uwanja wa Ushirika, wamekuwa gumzo kubwa kwa wapenzi na mashabiki wa soka.
Lakini, wengi wamekuwa wakijiuliza timu hii imetokea wapi. Ni timu iliyoanzishwa mwaka 2011, ikiundwa na mafundi wa mradi wa ujenzi wa kituo cha mafuta cha Kampuni ya Panone Co. Ltd, kilichopo Weruweru, wilayani Hai.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Klabu hiyo, Simon Kajaus, ilianzishwa na mafundi wajenzi yeye akiwa ndiye fundi mkuu kwa wakati huo, kwa lengo la kujiepusha kufanya mambo yasiyofaa baada ya saa za kazi.
“Klabu hii ilianza kama utani tu mwaka 2011, tulikuwa ni mafundi katika kituo cha mafuta pale Weruweru, mimi na wasaidizi wangu tuliona badala ya kutumia muda mwingi kufanya mambo yasiyofaa baada ya kazi, ni bora tufanye mazoezi,” anasema Kajaus.
Anasema wakati huo wakiwa wachache, waliamua kutumia boya la tenki ya maji kama mpira ambapo baada ya wiki moja, wakaamua kuchangishana na kununua mpira wa miguu wa watoto.
“Tulianza kwa kutumia boya kama mpira, baada ya wiki moja lile boya lilipasuka, ndipo tukaamua kuchangishana shilingi elfu moja kila mmoja kupata fedha ya kununulia mpira, tulinunua mpira wa watoto,” anasema.
Kuhama uwanja/kupata uongozi
Kajaus anasema baada ya timu kukua waliamua kuchangishana na kupata kiasi cha shilingi 35,000 za kununua mpira wa wakubwa pamoja na kuhamia uwanja mkubwa wa Kimashuku Mnadani, kutokana na wingi wa wachezaji na ubovu wa eneo la awali.
“Baadae timu ilianza kukua kutokana na kuongezeka kwa wachezaji kwani hata vijana wa mitaani, waliamua kujiunga nasi,” anasema.
Baada ya kuhama, wakapata wazo la kuweka uongozi wa muda ambapo Kajaus akateuliwa kuwa mwenyekiti, kocha wa timu akawa Ayubu Joel chini ya unahodha wa Bahati Naligiga akisaidiwa na Michael Stewart.
Mechi ya kwanza
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Panone, Augustino Hess, ambaye pia ni mmoja wa wachezaji waanzilishi, baada ya kuona kikosi kimekamilika, waliamua kutafuta mechi ya kwanza ya majaribio kujua uwezo wao halisi dimbani.
Anakumbuka kuwa mechi yao ya kwanza ilikuwa dhidi ya Kimashuko FC ya kijijini hapo na kufungwa 7-3.
Anakiri kuwa pamoja na kipigio hicho, hawakuweza kukata tamaa ya kusonga mbele katika kupigania mafanikio wakitambua mwanzo ni mgumu.
“Kipigo hicho hakitukatisha tamaa, tulicheza mechi nyingine ambayo tulishinda 4-0, baadae tukapata moyo wa kuendelea mbele kwa kuomba kucheza na timu zenye uwezo zaidi ikiwemo dhidi ya Lambo FC, bingwa wa Wilaya ya Hai wakati huo, lakini tulifungwa, tulifungwa 6-4,” anasema Hess.
Walianza kufanya usajili kuimarisha kikosi baada ya kipigo hicho wakichukua vijana mitaani na kuwapa ajira, na katika usajili huo waliwanasa nyota kama Elia Massawe, Ali Muya na Omari Miraji.
“Desemba 2011 tulifanya usajili na tukaomba mechi na Deca Flower na tukashinda 3-1, yakifungwa na Simon Kajaus na Elia Massawe aliyefunga mawili,” anasema Hess na kuongeza: “Tukaomba mechi dhidi ya Machame United ambayo tulichezea eneo la Mkomwasi, tukashinda 4-2.”
Baada ya hapo, Panone ilicheza mechi nyingine za kirafiki ndani na nje ya Mkoa wa Kilimanjaro chini ya kocha mpya Vitalis Shamuhelo kutoka Lambo FC.
Hess anakumbuka mechi ya kwanza kwao wakiwa katika jezi rasmi za kuuzia mafuta, ilikuwa dhidi ya Selian FC ya Arusha walipofungwa mabao 3-2.
Safari ya ubingwa
Meneja wa Kanda wa Kampuni ya Panome, Gido Marando, anasema baada ya uongozi wa kampuni kupata taarifa za timu hiyo, Mkurugenzi wake Patrick Ngiloi, aliongeza nguvu kwa kumwajiri kocha Atuga Manyundo akitokea AFC ya Arusha akisaidiwa na Shamuhelo.
Marando anasema waliweka timu kambini pamoja na kuendesha mchakato wa kupata uongozi mpya kwa lengo la kusuka kikosi hicho tayari kwa Ligi Daraja la Nne msimu wa 2012/2013.
Katika  uchaguzi huo, Kajaus aliendekea kuwa mwenyekiti wa klabu hiyo hadi sasa huku makamu wake akiwa Habibu Ali, Katibu Mkuu Hess, Katibu Msaidizi ni Ramadhani Hussein na Mhazini ni Carolyn James.
“Baada ya mafanikio kuwafikia mabosi wetu, Mkurugenzi na Meneja wa Kanda, walifurahia na kuanza kutusapoti ambapo mwanzoni mwa mwaka 2013, Mkurugenzi alimuajiri Kocha Atuga Manyundo kutoka AFC ya Arusha akisaidiwa na Vitalis Shamuhelo,” anasema Hess.
Walipoingia Ligi Daraja la Nne Wilaya ya Hai, wakajitwalia tiketi ya kucheza Ligi Daraja la Tatu ngazi ya mkoa, lakini wakitolewa katika hatua ya awali baada ya kumaliza katika nafasi ya tatu kwenye kundi lao; nyuma ya Polisi Kilimanjaro na Kitayosce SC.
Mwaka huo walishiriki mashindano mengine kadhaa ikiwemo Bonanza ya Elimu ya Watu Wazima mkoani Arusha na kutwaa ubingwa kabla ya kumaliza nafasi ya tatu kati ya timu 20 katika michuano ya UVCCM.
Ubingwa wa Mkoa
Msimu huu ndipo wamefanya makubwa katika historia yao wakifanikiwa kutwaa ubingwa wa mkoa dhidi ya Machava FC.
Katika mechi ya kwanza, Panone walifungwa 2-1, lakini kwa kanuni za usajili za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Panone walimkatia rufaa mchezaji Tony Kingunda wa Machava FC na kufanikiwa kupewa ushindi wa pointi tatu na mabao mawili.
Katika mechi ya pili, walikutana na Lang’ata bora, mechi iliyopigwa katika uwanja wa Cleopa Msuya, Mwanga, wakatoka sare ya bao 1-1 kabla ya kuibamiza Kilototoni FC 5-1; wakimalizia safari hiyo kwa sare ya bila kufungana dhidi ya Kitayosce SC.
Katika raundi ya timu 10 za mwisho, Panone FC ilipangwa katika kundi la kifo dhidi ya Machava FC, Kilimanjaro FC, New Generation na Forest FC ya Siha.
Kwenye mechi ya kwanza, walicheza na New Generation na kushinda 1-0 kabla ya kuichakaza Kilimanjaro FC 4-0.
Mchezo wa tatu katika hatua hiyo, Panone ilicheza na Machava na kushinda 1-0 kabla ya kumalizia hasira zao kwa Forest kwa kuichakaza 3-0 na kufanikiwa kuongoza kundi wakiwa na pointi 9.
Panone ilianza mzunguko wa kwanza wa hatua ya lala salama hatua ya sita bora ilikokuwa na timu za Machava, New Generation, Afro Boys, Agip Kahe, Polisi Kilimanjaro kwa kishindo, baada ya kuitandika Agip Kahe bao 1-0.
Mechi ya pili, Panone ilikutana na Afro Boys ikashinda 3-0 kabla ya kutoka sare ya bila kufungana na Polisi Kilimanjaro na baadae kutoa kipigo cha bao 1-0 kwa New Generation; mechi ambayo ilivunjika kutokana na vurugu, hivyo wao kuzawadiwa ushindi.
Katika mechi ya mwisho mzunguko wa kwanza, Panone FC iliwafunga Machava FC 1-0 katika dimba la Ushirika, hivyo kumaliza na pointi 13.
Kwenye raundi ya pili ya hatua hiyo, Panone FC ilikutana na Agip Kahe wakishinda 2-0 na kutoka sare ya 2-2 dhidi ya Afro Boys kabla ya kuvunja rekodi ya mkoa kwa kubeba ubingwa wakiwa na pointi 20, baada ya kuifunga Polisi Kilimanjaro bao 1-0.
Mechi mbili zilizofuata, Panone ilipoteza kwa kipigo cha 1-0 dhidi ya New Generation na kushinda nyingine dhidi ya Machava ambapo ilishinda 1-0 katika mechi kali iliyochezwa Uwanja wa Ushirika

No comments:

Post a Comment