Wednesday, September 4, 2013

Zitto alipua tuhuma nzito

MWENYEKITI wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe, amedai kuwa kuna wimbi la utoroshaji mkubwa wa fedha haramu nje ya nchi kuliko fedha za msaada na uwekezaji kutoka kwa wafadhili.
Aidha, Zitto amedai kuwa makampuni makubwa saba kati ya kumi yanayoongoza kwa kutorosha fedha na kuzificha katika nchi ambazo zimeweka sera za unafuu wa kodi na zisizokuwa na sheria za udhibiti wa uingizaji na upatikanaji wa mapato.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini hapa, Zitto alisema kati ya makampuni makubwa matatu ya simu hapa nchini, mawili yanahusika na ukwepaji mkubwa wa kodi kwa kujisajili katika nchi za Uholanzi na Ubelgiji, hivyo kuepuka kulipa kodi walizotakiwa.
Zitto alizidi kufichua kuwa moja ya kampuni kubwa za madini iliyoko hapa nchini imesajili makampuni mengine tisa katika nchi hizo, huku moja ya kampuni kubwa ya madini ikihusishwa na utoroshaji huo mkubwa.
Alisema nchi wahisani hutoa misaada inayokadiriwa kufikia kiasi cha dola za Marekani bilioni 37 huku uwekezaji kutoka nje ukiwa ni dola za Marekani bilioni 40 kwa mwaka.
Akizungumza juu ya mkutano wa 10 wa umoja wa kamati za mabunge za hesabu za serikali kutoka nchi wanachama wa SADC, (SADCOPAC), unaofanyika jijini hapa, alisema kumekuwa na matukio mengi ya kutorosha fedha na rasilimali za taifa katika nchi nyingi, na kuitolea mfano Tanzania ambayo imekumbwa na matukio hayo kwa kiwango kikubwa.
Alisema kumekuwa na utoroshaji wa fedha za taifa kupitia uuzaji wa mazao ya biashara, huku watendaji wa serikali wakionekana kuzidiwa ujanja.
“Mwaka 2011 Tanzania iliuza nje ya nchi tani 80,000 za korosho ambapo soko letu kuu ni India.
“Lakini utashangaa kuwa India wenyewe walisema kwa mwaka huo walipokea tani 120,000 kutoka kwetu, na hii inaonesha kuwa tani 40,000 zilitoroshwa bila kulipiwa kodi wala Benki Kuu (BoT) haina taarifa nazo, hivyo hawawezi kuzirudisha nchini kwa kuhofia kubainika,” alisema.
Aliongeza kuwa Tanzania inapoteza asimilia tano ya pato la ndani la taifa (GDP) kwa usafirishwaji wa fedha haramu zinazotokana na ukwepaji wa kodi na rushwa ambayo ni sawa na zaidi ya dola za Marekani bilioni 1.25 kila mwaka.
Aidha, amesema kuwa  kiasi cha zaidi ya dola za Marekani bilioni 844  zimekuwa zikitoroshwa nje ya Bara la Afrika kila mwaka kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2000 mpaka 2010  wakati misaada kutoka nchi wahisani na uwekezaji kutoka nje (FDI) zikikadiriwa kufikia kiasi cha dola za Marekani bilioni 80 kwa mwaka.
“Theluthi mbili ya fedha haramu hutoroshwa kwa kughushi nyaraka za malipo kwa kuongeza au kupunguza gharama halisi ya bidhaa wanazosafirisha nje au kuingiza barani Afrika ambapo kila dola moja inayokuja Afrika kama msaada dola saba hutoroshwa kwa njia haramu,” alisema.
Alifafanua kuwa sheria za nchi hizo, hazimlazimishi mtu ama kampuni kutoa maelezo ya namna alivyopata fedha hizo, na kama analipa kodi sahihi, jambo linalowavutia watu na makampuni yasiyo na uaminifu kuficha fedha hizo huko.
Zitto alisema kwa kuwa matukio ya aina hiyo yamesababisha athari kubwa za kiuchumi, hivyo ni jukumu la kamati za mahesabu ya umma kwenye kila nchi kufanya kazi ya kudhibiti utoroshwaji wa fedha haramu huku akiainisha changamoto iliyopo kwenye baadhi ya nchi za Afrika ambazo hazina kamati hizo, na zile zilizonazo za muda tu, kama Zambia na Swaziland.
Kutokana na hujuma hizo, wajumbe wa mkutano huo wanaokadiriwa kufikia 300 wamewasukumia lawama wabunge wa nchi nyingi za Afrika kwa kuweka mbele masilahi ya vyama vyao vya siasa  badala ya masilahi ya wananchi.
Mbunge wa Afrika Kusini, Nikiwe Num, wakati akichangia mada kwenye mkutano huo wa kamati za usimamizi wa hesabu za serikali za nchi za Kusini mwa Afrika (SADCOPAC), alisema lazima wabunge wazibane serikali zao kikamilifu, vinginevyo wimbi la hujuma litaongezeka.
Ameongeza kuwa kama wabunge hawatabadilika, wataendelea kulalamika tu, badala ya kuchukua hatua dhidi ya watawala na kuweka kando tofauti zao za kiitikadi.
“Mataifa ya Afrika yana katiba nzuri sana, tatizo hazifuatwi na tukiendelea kuweka mbele masilahi ya vyama hatutaweza kuzisimamia serikali kwani wabunge wengi wanatoka kwenye vyama tawala kila mara tutakuja hapa tukilialia kuwa mambo hayaendi lazima tubadilike,” alisema Num.
Awali Mwenyekiti wa SADCOPAC, Sipho Makama, kutoka nchini Afrika Kusini alisema kuwa mkutano huo unazikutanisha nchi zote za SADC isipokuwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambayo kwa sasa hali si shwari nchini humo kutokana na vita inayoendelea kati ya serikali na waasi wa M23.
Zaidi ya wajumbe 300 wanahudhuria mkutano huo ambao ni wabunge wa kamati za hesabu za serikali, wakaguzi na wadhibiti wa hesabu za serikali, wahasibu wakuu wa serikali, makatibu wa kamati za PAC, maspika wa mabunge ya SADC pamoja na wahisani kutoka taasisi mbalimbali za kimataifa.
chanzo-Tanzania daima

No comments:

Post a Comment