Singida. Polisi wametanda eneo la mkutano wa Baraza la Katiba lililoandaliwa na Chadema, Wilaya ya Iramba.
Mkutano huo ulifanyika juzi katika Uwanja wa Soko
la Zamani, ambako ni nyumbani kwa Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu
Nchemba. Baada ya kuwasili kwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod
Slaa, askari walionekana kutanda kila kona ya uwanja huo.
Baadhi ya askari walikuwa wameshikilia mabomu ya
machozi na marungu huku wakiwa wamevalia kofia ngumu, lakini muda mfupi
gari lililosheheni Polisi wa Kutuliza Ghasia (FFU) liliwasili wanjani
hapo na kuegeshwa pembeni mwa mkutano.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Mabere Marando, alikuwa wa kwanza kupanda jukwaani na kukemea kitendo hicho.
“Ndugu zangu polisi mnatumika vibaya jinsi
mlivyokaa hapa mkiwa mmevalia kofia zenu na mabomu kama vile mnataka
kupambana na wahalifu, ni kitendo kibaya,” alisema Marando na kuongeza:
“Huu mkutano umeruhusiwa kisheria na Tume na nyie
hamna mamlaka ya kuuzuia, ila nadhani haya ni maagizo kutoka kwa
Mbunge Mwigulu Nchemba kama tulivyokuwa tumeelewa kabla ya kufika. “Naye
Dk Slaa aliwataadharisha polisi kuacha tabia ya kufanya kazi zao kwa
maelekezo ya watu, bila kufuata taaluma zao.
“Kila siku tunawalalamikia polisi kuwa chanzo cha
vurugu, huu ni ushahidi tosha mmezunguka jukwaa langu lote huku wananchi
ambao ni walengwa mmewasogeza mbali,” alisema Dk Slaa na kuongeza:
“Sikuja hapa kuongea na nyie, nimewafuata wananchi naomba mtoke mkae mbali ili watu wangu wasogee karibu na hiyo ni amri.”
Kitendo ambacho kilipokelewa kwa shangwe na wananchi kwa kushangilia na kuweza kusogea karibu ya jukwaa.
No comments:
Post a Comment