Tanga. Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Joseph Butiku
amesema asingekubali kushiriki katika Tume hiyo laiti kama angejua CCM
ingeingilia mchakato huo.
Butiku ambaye alitoa kauli hizo kwa nyakati
tofauti, wikiendi iliyopita kwenye Mabaraza ya Katiba ya Halmashauri ya
Mji wa Soni, Lushoto na Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, alieleza
kutokufurahishwa kwake na kitendo cha CCM kushinikiza maoni yake mbele
ya mabaraza hayo.
Alilalamika kuwa kitabu cha mwongozo wa utoaji
maoni kilichotolewa na CCM kinatumiwa vibaya kushinikiza maoni kwenye
Rasimu ya Katiba Mpya.
“CCM imeandaa kitabu kizuri kweli kusaidia
wanachama wake, tuliwaambia (Tume) hatukitaki; ni mwongozo kusaidia
wanachama wake namna ya kutoa maoni, lakini kimekuwa kinatumika vibaya.
Kinatumika kushinikiza maoni,” alisema Butiku.
Butiku ambaye ni mwanachama wa Tanu tangu mwaka
1958 na CCM kuanzia 1977 alisema: “Ningejua itatokea chama kitafanya
hivyo, nisingekula kiapo nilichokula kufanya kazi hii katika Tume ya
Marekebisho ya Katiba. Kundi moja lisigeuke Tanzania. Mimi ni mzee
nasema kitu kikubwa nataka Mwenyekiti (wa CCM) asikie, Halmashauri Kuu
yangu (ya CCM) isikie. Mchakato huu usiingiliwe, madiwani saidieni
wananchi wenu kujielewa. Muungano hautaponywa kwa helikopta zinazoruka
au vitabu vinavyosambazwa.”
Muungano
Kuhusu Muungano, Butiku aliyewahi kushika nyadhifa
mbalimbali serikalini alisema: “Mimi ni mzee sasa, sitaki kwenda
kaburini bila kuwaambia ukweli. Endeleeni kuujadili, msifanye jambo la
kutaka asali bila kujua madhara yake,” alisema.
Kauli hiyo ya Butiku ambaye pia ni Mkurugenzi wa
Taasisi ya Mfuko wa Mwalimu Nyerere ilitokana na wajumbe kuonyesha
mvutano kuhusu muundo wa Serikali katika Muungano na wengi walionekana
kuelemea upande wa Serikali mbili uliopo sasa, baadhi kuunga mkono
Rasimu ya Katiba inayopendekeza Serikali tatu, huku wachache wakitaka
Serikali moja.
Butiku aliwataka wajumbe wa Mabaraza ya Katiba
kutoa maoni yanayolenga kulinda na siyo kuvunja Muungano na kwamba Tume
ya Marekebisho ya Katiba imepewa kazi ya kuulinda akisisitiza kwamba
haikuwa, wala haina ajenda ya kuvunja.
“Wapo pia viongozi wakubwa ndani ya Baraza la
Wawakilishi, wengine wamestaafu, hawautaki Muungano. Tume inawafahamu
wanaotaka Tume ya Katiba iwe na ajenda ya kuvunja Muungano. Muungano
huu, ulimfukuza Aboud Jumbe madarakani, kiongozi mkubwa tu, mi nawaambia
mambo mengine siri. Jumbe alitoka kwenye mkutano wa CCM, kaja pale nje
akakuta gari lake lingine siyo la Makamu. Leo, (anamtaja kiongozi huyo)
anasema tulifanya makosa kuungana, anajiunga na Jumbe, anaanza kufanana
na Uamsho,” alisema Butiku.
Butiku aliifananisha Katiba Mpya nzuri kuwa sawa
na asali akieleza kuwa inahitaji umakini wakati wa kuiandaa, akifafanua
kuwa unapoandaa asali lazima uwe makini vinginevyo unaweza kuambulia
kushambuliwa na nyuki.
“Wajumbe msipokuwa wa kweli, badala yake watu
wakaumwa na nyuki, mtatulaumu. Ukweli wanaufahamu wote ili waweze
kuamua? Tumekubaliana kwenye Tume tuambiane ukweli ili tupate asali.”
No comments:
Post a Comment