Dar es Salaam: Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji
Joseph Warioba amesema iwapo Mfumo wa Serikali Tatu utaridhiwa na
wananchi ni lazima mambo yaliyo ndani ya Muungano yatagawanywa ikiwa ni
pamoja na Ikulu ya Rais.
Amesema kuwa kutokana na taifa kufanya mabadiliko
ya Katiba ni lazima kuwepo mpangilio wa kugawana mambo mbalimbali
yaliyokuwa chini ya Muungano ikiwamo majengo, wafanyakazi, Ikulu, hata
vitendea kazi na kwamba utaratibu huo ni kama ule uliotumika wakati
Tanganyika na Zanzibar zilipoungana.
Kauli ya hiyo ya Jaji Warioba imekuja siku tatu
tangu Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe kueleza kuwa Tanzania
Bara itaanza mchakato wa kutunga Katiba yake Aprili mwaka 2014 na
kumalizika Desemba mwaka huohuo.
Jaji Warioba aliyasema hayo katika mahojiano
maalumu na waandishi waandamizi wa Kampuni ya Mwananchi Communications
Limited (MCL), inayochapisha magazeti ya Mwananchi, Mwananchi Jumamosi,
Mwananchi Jumapili, Mwanaspoti, The Citizen na The Citizen on Sunday,
Tido Mhando ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa MCL na Theophil
Makunga, Meneja wa Uendeshaji na Biashara MCL.
Swali: Makao Makuu ya Serikali ya Muungano yatakuwa wapi?
Warioba: Ukibadili Katiba wakati wowote ni lazima kuwe na makubaliano fulani.
Unajua Serikali ya Muungano na Tanganyika ilikuwa
pamoja, sasa ukianzisha Serikali ya Tanganyika, lazima kwenye mpangilio
muanze kugawana hata wafanyakazi kwa kuwa wafanyakazi hao walikuwa ni wa
Muungano. Hapo ndiyo mtaamua wafanyakazi gani watakwenda katika
Serikali ya Tanganyika, watakaobaki katika Muungano na wale
watakaokwenda Zanzibar.
Hata katika majengo hali inakuwa hivyo hivyo,
lazima kutakuwa na majengo yaliyokuwa yakitumiwa na wizara mbalimbali na
hata Ikulu. Hapo pia lazima myagawanye na kukubaliana viongozi wa
Tanganyika watakuwa wapi na wale wa Muungano watakuwa wapi. Lakini, hata
vifaa vya kutendea kazi navyo inatakiwa mgawane kulingana na
makubaliano yenu.
Suala hili linategemea zaidi mazungumzo ya pande
zote mbili, baada ya kukamilika kwa mchakato huu kwa sababu hii
iliyopatikana sasa ni rasimu tu, ambayo itajadiliwa na wananchi kabla ya
kuanza kwa Bunge la Katiba na baadaye kuwepo kwa kura ya maoni. Wapo
watakaokuwa wakihoji kuhusu vyeo, katika hili itakuwa kama tulivyokuwa
tukiungana Tanganyika na Zanzibar, wakati huo wapo ambao walikuwa wakuu
wa mikoa na wakajikuta wameingia katika Muungano huku wakiwa na vyeo
hivyo. Kilichofanyika ni kuendelea tu na nafasi hizo mpaka
utakapofanyika utaratibu mwingine kwa njia ya mazungumzo.
Unajua jambo hili siyo jukumu la tume hii, tunaliacha kwa sasa na hatujui litakuwaje kwa sababu ni suala la mazungumzo.
Swali: Majukumu ya Rais yatakuwaje?
Warioba: Rasimu imeeleza majukumu (roles) ya Rais
kama mkuu wa nchi, ambaye anakuwa kama taasisi na sisi tulichokifanya ni
kujenga taasisi hizo, kwamba ijulikane akifanya chochote awe
ameshauriwa, isiwe yeye peke yake.
No comments:
Post a Comment