Kama utakuwa shabiki na mtazamaji mzuri wa filamu za bongo movie, jina la Lucy Francis Komba halitakuwa jipya masikioni mwako.
Msanii huyu alianza sanaa katika Kundi la Kaole,
akishiriki baadhi ya vipindi vya televisheni na baadaye kujiunga na
Kikundi cha Dar Talent, ambapo alishiriki filamu moja ya vichekesho.
Katika sanaa, Lucy ameshacheza filamu zaidi ya 50
zikiwemo nne alizocheza nje ya nchi. Filamu ya kwanza aliyocheza nyota
huyu na kuonyesha kipaji chake inafahamika kama Utata. Baadaye
alishiriki filamu ya Yolanda, Division of Love, Jeraha la Ndoa, Talaka
Wodini, Siri ya Moyo Wangu, Teke la Mama, Richmond, Swadakta na
nyinginezo.
Kwa sasa Lucy ni mwigizaji wa filamu, mwongozaji,
mtunzi wa stori na mtayarishaji wa filamu aliyefanikiwa kuvuka mipaka ya
nchi hasa Bongo Movie akichanua hadi katika nchi za Burundi, Sierra
Leone na Denmark.
Lucy kwa sasa anasubiri kuzindua filamu yake mpya aliyoichezea nchini Denmark.
”Nilienda kupumzika tu, lakini baada ya kuona wana
mwitikio mzuri na filamu zetu, ilinibidi nicheze filamu niliyoipa jina
la ‘Tanzania to Denmark’,” anasema Lucy.
Anabainisha kuwa filamu hiyo amecheza kwa gharama
zake akishirikiana na Kampuni ya Vad Production ya Denmark
inayojihusisha na uzalishaji wa filamu.
“Walinisaidia sana hadi hatua ya mwisho. Natarajia
kuizindua mwezi huu wa Juni nchini Denmark, naamini itauza sana, maana
nimecheza na wasanii maarufu wa huko,”anasema Lucy.
Aprili mwaka jana, msanii huyo alifanikiwa kwenda
nchini Ghana kwa maandalizi ya kucheza filamu yake, hata hivyo hakuweza
kufanikiwa baada ya msanii mwenzake Kanumba kufariki dunia.
“Mimi nilikuwa nimeshatangulia, nikiwa huko nikasikia amefariki ikanibidi nirudi kwanza nyumbani kwa mazishi yake,”anasema Lucy.
Kabla ya kuondoka Ghana, Lucy alibahatika kufanya
mahojiano na mastaa wa nchini Sierra Leone waliokuwa wakikusanya
washiriki wakubwa kwa lengo la kuandaa filamu itakayojitambulisha
kimataifa.
Maandalizi hayo ni maarufu kama ‘famous film
magazine in Africa’ ambayo imewashirikisha baadhi ya nyota akiwamo Van
Vicker, Ini Edo, Desmond na wengineo katika kuandaa filamu ya ‘Repackage
live’.
No comments:
Post a Comment