Thursday, February 28, 2013

Zaidi ya 1000 wajiunga CHADEMA

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kupitia kikosi kazi chake cha Vuguvugu la Mabadiliko (M4C), Kanda ya Ziwa, kimefanikiwa kuzoa zaidi ya wanachama wapya 1,000, wengi wakitokea Chama cha Mapinduzi (CCM).

Wakizungumza na Tanzania Daima jana wilayani hapa, viongozi waandamizi wa M4C Kanda ya Ziwa, Husina Amri Saidi, na Alfonce Mawazo, walisema M4C imedhamiria kujikita zaidi maeneo ya vijijini.

Walisema baadhi ya wananchi hao walipatikana katika mikutano yao iliyofanyika kisiwa cha Bumbile, kata ya Bumbile, jimbo hilo la Muleba Kaskazini ambao ni zaidi ya 200 waliojiunga na CHADEMA.

Mbali na hilo alisema zaidi ya wanachama 100 wa CCM walilazimika kurudisha kadi zao na kujiunga CHADEMA.

“Kwa kweli CHADEMA kupitia M4C tumeweza kuzoa wanachama wengi katika visiwa vya Muleba Kaskazini.

“Kisiwa cha Bumbile, kata ya Bumbile, zaidi ya wananchi 200 wamejiunga na CHADEMA kwa kununua kadi kwa hela zao.

“Lakini, wapo zaidi ya wana CCM 100 wamerudisha kadi za ‘magamba’ kisha kuvaa ‘kombati’,” alisema Husina.

Walisema wakiwa katika visiwa vya Lushonga na Mchangani zaidi ya wananchi 438 walijiunga na CHADEMA.

Akizungumzia harakati za CHADEMA katika kuelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2014 na uchaguzi mkuu ujao mwaka 2015, Kamanda wa M4C Kanda ya Ziwa, Mawazo, aliwasihi wananchi wote wa Kanda ya Ziwa na Tanzania kwa jumla kutumia nguvu ya umma kuiondoa CCM madarakani kwenye uchaguzi mkuu ujao.

No comments:

Post a Comment