Friday, February 1, 2013

Mahakama yatupa maombi kufunguliwa Kanisa Dar

MAHAKAMA Kuu Kitengo cha Ardhi Dar es Salaam, imetupilia mbali ombi  la  Bodi ya Wadhamini ya Kanisa la Moravian Jimbo la Kusini, la kutaka kufunguliwa makufuli yaliyofungwa katika Kanisa la Usharika wa Tabata, ili waweze kumsimika mchungaji mpya, ambaye ni Lawi Mwankuga.
Add caption
Uamuzi huo ulitolewa jana na Jaji Mathew Mwaimu,baada ya bodi  hiyo ya wadhami wa Kanisa la Moravian Kusini chini ya Mchungaji Clement Mwaitebele, kupitia wakili wao, Henry Chaula wa Kampuni ya Uwakili ya C&M,  kufungua kesi namba 12  ya mwaka 2013 na kuomba isikilizwe chini ya  hati ya dharura.
Kwa mujibu wa kesi hiyo, Mchungaji Gervas Mwakafwila, Mchungaji Silas Mwakibinga, Tukuswiga Mwakabur, Atuganile Mbombo, Isakwisa Ernest  na Sekela Mukisele  ambao wanatetewa na Wakili Benjamin Mwakaganda wa Kampuni ya uwakili ya  BM,  wanadaiwa  kufunga makufuli kwenye  Kanisa la Usharika wa Tabata, ili kuzuia bodi hiyo  kumsimika mchungaji mpya.
Akitoa uamuzi, Jaji Mwaimu alikataa ombi la bodi hiyo  ya wadhamini la kutaka kufunguliwa kwa makufuli yaliyokuwa yamefungwa kwenye kanisa hilo, ili kupisha kumsimika mchungaji mpya.
Pia jaji huyo aliruhusu shughuli za kawaida za kanisani hapo kuendelea  na kusisitiza kwamba kilichozuiwa ni usimikaji wa mchungaji ili kuondoa uvunjifu wa amani.
Baada ya kutoa uamuzi huo, Jaji Mwaimu aliwataka wadaiwa  kupeleka kiapo pinzani mnamo  au kabla ya Februari 5, mwaka huu ambapo kesi hiyo imepangwa kusikilizwa.
Bodi hiyo ya wadhamini wa Kanisa la Moravian Jimbo la Rungwe  ni wadaiwa  namba 4 katika kesi namba 222 iliyofunguliwa mwaka 2012 katika Mahakama Kuu, ambayo inaendelea kusikilizwa Februari 6, mwaka huu mbele ya Jaji Augustini Mwarija.
Katika kesi hiyo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Jimbo la Mashariki na Pwani ya Kanisa la Moravian Tanzania, Clement Fumbo na wenzake saba wanapinga kuondolewa madarakani na kusimamishwa kazi.
Katika kesi hiyo, Fumbo na wenzake hao saba wanaiomba Mahakama iamuru walipwe Sh500 milioni kama fidia na gharama ya kesi.

No comments:

Post a Comment