Sunday, February 24, 2013

Muhimbili, Aga Khan kufanya operesheni ya moyo

HUDUMA za matibabu na upasuaji wa moyo zitaanza kupatikana nchini, kutokana na mipango ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na ile ya Aga Khan.
Hatua hiyo itawawezesha wagonjwa wa moyo nchini kutopelekwa kwa wingi nje ya nchi kama ilivyo sasa. Pia itaokoa mamilioni ya fedha ambazo zimekuwa zikitumika kugharimia tiba hiyo nje ya nchi.
Mkurugenzi wa Huduma za Afya wa Hospitali za Aga Khan Tanzania, Dk Jaffer Dharsee akiwasilisha taarifa kuhusu ongezeko la magonjwa ya moyo nchini katika kongamano la wataalamu wa magonjwa hayo alisema, jitihada kubwa zinafanywa ili kuhakikisha tiba ya moyo inaanza kutolewa nchini.
Alisema Hospitali ya Muhimbili inakusudia kuanza kutoa tiba hiyo katika kipindi cha miezi miwili ijayo baada ya ujenzi wa taasisi yake kukamilika, wakati Hospitali ya Aga Khan itaanza kutoa matibabu hayo mwakani. Kongamano hilo lilifanyika mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Dar es Salaam.
Hatua ya kuwapo kwa tiba za moyo nchini, itawezesha gharama za tiba kupungua kwa asilimia 57.1, ikilinganishwa na gharama za tiba hizo nje ya nchi.
Dk Dharsee alisema hapa nchini gharama za tiba zitakuwa Dola za Marekani 1,500 sawa na Sh2.4 milioni tofauti na Dola 3,500 (Sh5.6 milioni) zinazotumika kumpeleka mgonjwa kwa ajili ya upasuaji nchi za nje kama India.
Alisema gharama hiyo inatokana na kuwapo kwa gharama kubwa zinazohitajika kuandaa maabara hiyo ambayo ina thamani ya Dola 200 milioni (Sh320 bilioni) bila kuingiza gharama za wataalamu wa kuiendesha na kuhudumia wagonjwa.
Muhimbili
Habari ambazo gazeti hili lilizipata zinasema kwamba Taasisi ya Tiba ya Moyo Muhimbili itaanza kazi zake rasmi katika muda wa miezi miwili kuanzia sasa, baada ya kukamilika kwa jengo la taasisi hiyo, kuanzisha maabara maalumu ya upasuaji na matibabu ya moyo kukamilika.
Ujenzi wa jengo hilo ulianza miaka mitatu iliyopita kwa msaada wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China, iliyotoa Sh16.22 bilioni wakati Serikali ya Tanzania ilichangia Sh6 bilioni.
Mei 2008 Hospitali ya Muhimbili ilianzisha Kitengo cha Tiba ya Moyo na Figo, ambacho kwa mujibu wa Ofisa Uhusiano wa hospitali hiyo, Aminieli Aligaesha alisema kwamba kimeshatoa matibabu kwa zaidi ya wagonjwa 300 tangu kuanzishwa kwake.
 Aga Khan

Kwa upande wa Aga Khan, Dk Dharsee alisema hospitali yake imewekeza kiasi cha Dola za Marekani 4.6 milioni (Sh7.36 bilioni) kuandaa wataalamu wa kuwahudumia wagonjwa wa matatizo ya moyo.
Alisema licha ya maandalizi ya kuleta huduma za upasuaji nchini, hospitali yake imeanza kutoa huduma za kliniki bure kwa vipimo na tiba ndogo ndogo kila Jumatano na Alhamisi.
“Wastani wa wagonjwa 10 wanaofika hospitalini kwetu tumegundua, wanne wana ugonjwa wa moyo,” alisema Dk Dharsee.
Alisema mitindo ya maisha isiyofaa kama uvutaji wa sigara, ulaji wa vyakula usiozingatia afya, ulevi na uzembe wa kutofanya mazoezi mara kwa mara ndiyo vimechochea kwa kiasi kubwa ongezeko la magonjwa ya moyo.
“Hivi sasa takriban asilimia 20 ya watu waishio mijini wanaongezeka uzito kwa kiwango kikubwa jambo ambalo linatishia ongezeko la magonjwa ya moyo kama shinikizo la damu na kupooza,” alisema Dk Dharsee.
“Mwaka 2002 kulikuwa na vifo ya takriban watu 46,000 kutokana na matatizo ya moyo na idadi hiyo inategemewa kuongezeka mpaka 63,000 ifikapo 2015 na 85,400 hapo 2031.
Aliongeza kuwa magonjwa hayo kunaiongezea Serikali mzigo pamoja na kuathiri uchumi wa familia kwa kuwa mwaka 2005 pekee inakadiriwa kuwa Tanzania ilipoteza Dola 100 milioni kwa ajili ya kutibu magonjwa ya kisukari, kupooza na shinikizo la damu.

No comments:

Post a Comment