Friday, February 1, 2013

OSCAR KAMBONA: Shujaa aliyegeuka adui wa taifa lake

WIKI iliyopita niliwaletea makala ya muasisi wa chama cha TAA, TANU na baadaye CCM ambaye alikuwa mpigania uhuru wa Tanganyika iliyozaa Tanzania, marehemu Lawi Nangwanda Sijaona.
Makala ile imeleta hoja nyingi kutoka kwa wasomaji ambao wameomba kuandikwa kwa Watanzania wengine waliolitumikia taifa kwa uaminifu na kuwa mashuhuri katika nyanja kadhaa za siasa, michezo, utamaduni na utawala lakini wamesahaulika.
Hivyo kwa nia ya kutimiza matakwa yao na kuendeleza makala hii, leo ninawaletea historia ya mwanasiasa Oscar Kambona.
Oscar Kambona ni miongoni mwa viongozi mahiri na shupavu waliowahi kuwa gumzo ndani na nje ya Tanzania, kutokana na uongozi wake, hekima na busara.
Ndiye Mtanzania wa kwanza kuwa waziri aliyeongoza wizara mbili kwa wakati mmoja. Ndiye Mtanzania pekee anayeaminika kusimama kidete na kufanikiwa kulidhibiti jeshi lililoasi mwaka 1964.
Hata hivyo, pamoja na umahiri huo, lakini kubwa zaidi kutokuwa na tamaa ya kutumia nafasi ya uasi wa jeshi kushika madaraka ya nchi.
Pamoja na hayo mchango wake hauthaminiwi kabisa. Tofauti na viongozi wengine wa siasa au hata utamaduni, mpaka sasa hakuna barabara yenye ukumbusho wa jina la mwanasiasa huyu aliyefariki akiwa katika matibabu mjini London, Juni 1997 na mwili wake kurudishwa Tanzania kwa mazishi.
Oscar Kambona alizaliwa mwaka 1925, katika kijiji cha Kwambe kilichoko mwambao mwa Ziwa Nyasa, karibu na Mbamba-Bay, wilaya ya Mbinga, mkoani wa Ruvuma.
Alikuwa ni mtoto wa Kasisi David Kambona ambaye alikuwa miongoni mwa Waafrika wa kwanza kupata upadri katika kanisa la Anglikana la Tanganyika, na kwa mama Miriam Kambona.
Akiwa mdogo, baba yake alikuwa akimweleza kuhusu ndoto zake juu ya uhuru wa nchi yake, hivyo kumfanya Oscar kujawa na hamu ya kuitumikia nchi yake.
Msingi wa elimu yake aliupata nyumbani kwao, chini ya mwembe (ambao bado uko mpaka sasa), katika kijiji cha Kwambe, kwa kuwatumia wazazi wake wote wawili na mjomba wake, ambao wote walikuwa walimu.
Alipelekwa shule ya kati ya Mt. Barnabas, Liuli na baadaye Shule ya Sekondari ya Alliance (sasa Shule ya Sekondari Mazengo), ambako alilipiwa ada na askofu Mzungu wa Anglikana kwa vile baba yake hakuweza kumudu kulipa ada ya pauni 30 kwa mwaka. Inasimuliwa kuwa kilichomvutia Mzungu huyo kukubali kumlipia Oscar ada ni baada ya kusali sala ya Baba Yetu Uliye Mbinguni kwa Kizungu.
Alichaguliwa kwenda ‘Tabora Boys Senior Government School ambako ndiko alikokutana na Mwalimu Julius Nyerere kwa mara ya kwanza. Wakati huo Nyerere alikuwa anafundisha katika shule ya Kikatoliki ya St Marys.
Kukutana tena na Nyerere
Ilikuwa mwaka 1954, kwenye mkutano wa kitaifa wa walimu, ndipo Oscar Kambona ambaye naye alikuwa amemaliza shule na kufundisha katika shule ya Alliance, alikutana tena na Nyerere na kujadili mambo mbalimbali ikiwemo harakati za chama cha TANU.
Oscar alishawishika kuitumikia TANU ambayo ilikuwa imeanzishwa muda si mrefu, bila malipo baada ya Mwalimu Nyerere kumweleza kuwa asingeweza kuajiriwa ndani ya chama kwa vile haikuwa na fedha.
Huo ulikuwa uamuzi mzito na mgumu mno, hasa kwa mtu kukubali kuachia nafasi ya ualimu ambayo alikuwa akilipwa vizuri na kufanya kazi bila malipo tena za chama ambacho ndiyo kwanza kilikuwa kikianza harakati za ukombozi.
Kwa miezi takriban sita, Oscar Kambona alifanya kazi ngumu ya kuzunguka sehemu mbalimbali za nchi na kuonana na machifu na wazee wa vijiji ili kusajili wanachama.
Kwa kipindi hicho huku akitumia fedha kidogo alizokuwa amejiwekea akiba yake, alifanikiwa kusajili wanachama 10,000 na haikuwa ajabu kuwa baada ya mwaka mmoja alikuwa amepata wanachama hai 100,000.
Ili kutunza fedha za chama, Kambona alifungua akaunti ya kwanza ya TANU na kisha kwenda Butiama kumshawishi Mwalimu Nyerere achukue uongozi wa chama moja kwa moja kama mtendaji mkuu.
Mwaka 1957, Kambona alikwenda kusomea sheria katika Chuo cha Middle Temple, nchini Uingereza kwa ufadhili wa Gavana.
Akiwa London Kambona alikuwa kiongozi wa chama cha wanafunzi wa Tanganyika na mwenyekiti wa tawi la TANU la London.
Kukutana na watu mashuhuri
Mwaka 1958, Kambona alipata fursa ya kukutana kwa mara ya kwanza na watu mashuhuri akiwemo George Padmore, mwanaharakati wa umoja wa wa Waafrika duniani, ambaye alimshawishi ahudhurie mkutano wa Waafrika wote (All Africa’s Peoples Conference), uliofanyika nchini Ghana muda mfupi baada ya kupata Uhuru.
Kambona alisafiri mpaka Ghana, wakati huo akiwa bado anaendelea na masomo yake nchini Uingereza na huko alipata nafasi ya kukutana na mwanaharakati mwingine maarufu wa siasa za Afrika, Kwame Nkrumah.
Utangazaji wake BBC
Kambona ndiye Mwafrika wa kwanza kutangaza taarifa ya habari kwa lugha ya Kiswahili, katika Idhaa ya Kiswahili ya BBC, ambayo sasa inajulikana kama (BBC Swahili).
Inadaiwa kuwa alikuwa akipenda sana uandishi wa habari kwenye vyombo vya kimataifa.
Katika kuhakikisha anapigania uhuru na mafanikio ya TANU, Kambona akiwa anaendelea na masomo yake nchini Uingereza, alikutana na Mwalimu Nyerere kila alipoenda nchini humo na kupanga mikakati ya kudai uhuru.
Kambona alifunga ndoa na Flora Moriyo na harusi ilifungwa katika kanisa la Mt. Paul, London, na Nyerere ndiye alikuwa msimamizi.
Kurudi Tanganyika
Mwaka 1959, Kambona alirudi Tanganyika na kuendeleza harakati za kudai uhuru kupitia TANU, huku wakiweka bayana madai ya kupewa serikali ya madaraka.
Kambona kwa kushirikiana na wenzake akiwamo Nyerere, waliweka mikakati mbalimbali huku wakiwa tayari kuanzisha mapambano kama ilivyokuwa kwa Mau Mau ya Kenya.
Katika uchaguzi wa kwanza TANU ilishinda viti vyote isipokuwa kimoja na kuunda Serikali ya Mambo ya Ndani chini ya Mwalimu Nyerere ambaye alikuwa Waziri Kiongozi wa kwanza.
Kambona aliteuliwa kuwa Waziri wa Elimu na baadaye alishika nyadhifa za Waziri wa Mambo ya Ndani, Mambo ya Nchi za Nje na Ulinzi na Tawala za Mikoa.
Katika nyadhifa hizo, Kambona pia alikuwa mwenyekiti wa kwanza wa Kamati ya Ukombozi ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika na Mwenyekiti wa Utayarishaji wa OAU ambayo sasa ni AU.
Kuunganisha bara na visiwani
Mwaka 1964, Kambona alifanya kazi kubwa katika kuunganisha Zanzibar na Tanganyika, akiwa pamoja na Rais Nyerere na Karume. Hii ilikuwa ni baada ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Januari 20, 1964, wanajeshi wa kikosi cha Calito waliasi. Kambona akiwa waziri wa Ulinzi, alisimama kidete kusuluhisha na msemaji mkuu upande wa serikali huku viongozi wakuu Mwalimu Nyerere na makamu wake, Rashid Kawawa, ikisemekana wakiwa wamekimbilia mafichoni Kigamboni walikokaa kwa siku tatu za majadiliano mazito mpaka machafuko yalipoisha.
Moja ya nukuu za Kambona katika mahojiano na gazeti la Daily Telegraph la London, alisema, “Baada ya kuwatuliza wanajeshi nilikwenda kuwatafuta viongozi wengine na kuwarudisha mjini kwa kutumia Land Rover yangu.”
Kambona alisifiwa sana na Mwalimu Nyerere kwa hekima na busara yake hadi kufanikiwa kumaliza uasi huo kwa kutumia nafasi yake ya uwaziri wa ulinzi. Wapo walioanza kuvumisha kuwa huenda kwa uaminifu wake, angeshika nafasi ya urais baada ya Nyerere kumaliza muda wake.
Ilikuwaje akawa adui wa serikali? Endelea toleo lijalo…
imeandaliwa na Andrew Chale

No comments:

Post a Comment