Akizungumza na Mwananchi jana Profesa J alisema
hajajiunga na Chadema ili kugombea ubunge mwaka 2015, isipokuwa kwa
dhumuni la kutaka kuongeza nguvu katika chama hicho akiwa kama kijana.
“Kujiunga na siasa si dhambi na haina maana kwamba
nina mpango wa kugombea jimbo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Sihitaji kugombea hata udiwani ila ni kwa dhumuni la kutaka kuongeza
nguvu katika chama ili kuyafikia malengo,” alisema.
Alisema yeye ni mfuasi wa Chadema tangu mwaka 2005
na amekuwa karibu na chama kwa nyakati nyingi lakini kwa sasa ameamua
kuingia rasmi katika chama kama chachu katika kuongeza harakati kwa
vijana.
“Nimeingia ili nisaidie hiki chama kuikomboa
Tanzania kwani kwa muda mrefu niliokaa katika chama hiki nimegundua kuwa
wamedhamiria kumkomboa msanii, kijana wa kawaida na wakubwa kwa wadogo
hivyo nadhani nipo sahihi katika uamuzi wangu.”
“Natambua mimi ni mwanamuziki, sawa nina mashabiki
wengi lakini haina maana kwamba sina haki ya kuchagua chama ninachoona
mimi kinanifaa, lakini siwezi kusita kufanya kazi sehemu yoyote au
wakati wowote chama kikinitaka nifanye kwa wakati husika,” alisema
Profesa J.
Profesa J juzi alijiunga rasmi na chama hicho
baada ya kukabidhiwa kadi ya Chadema mjini Dodoma na Mbunge wa Mbeya
Mjini, Joseph Mbilinyi akiwa sambamba na msanii mwingine wa hiphop Kulwa
Kinega maarufu kama K wa Mapacha ambaye alikabidhiwa kadi hiyo na
Mbunge wa Ubungo John Mnyika.