Tuesday, August 20, 2013

Viongozi wamtuhumu Mwigulu Nchemba kushirikiana na polisi kutisha wananchi.


0
Share


Singida. Polisi wametanda  eneo la mkutano  wa Baraza la Katiba lililoandaliwa na Chadema, Wilaya ya Iramba.
Mkutano huo ulifanyika juzi katika Uwanja wa Soko la Zamani, ambako ni nyumbani kwa Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba. Baada ya kuwasili kwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa, askari walionekana kutanda kila kona ya uwanja huo.
Baadhi ya askari walikuwa wameshikilia mabomu ya machozi na marungu huku wakiwa wamevalia kofia ngumu,  lakini muda mfupi gari lililosheheni Polisi wa Kutuliza Ghasia (FFU) liliwasili  wanjani hapo na kuegeshwa pembeni mwa mkutano.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Mabere Marando,   alikuwa wa kwanza kupanda jukwaani na kukemea kitendo hicho.
“Ndugu zangu polisi mnatumika vibaya jinsi mlivyokaa hapa mkiwa mmevalia kofia zenu na mabomu kama vile mnataka kupambana na wahalifu, ni kitendo kibaya,” alisema Marando na kuongeza:
“Huu mkutano umeruhusiwa  kisheria na Tume na nyie hamna mamlaka ya kuuzuia,  ila nadhani haya ni maagizo kutoka kwa Mbunge Mwigulu Nchemba kama tulivyokuwa tumeelewa kabla ya kufika. “Naye Dk Slaa aliwataadharisha polisi kuacha tabia ya kufanya kazi zao kwa maelekezo ya watu, bila kufuata taaluma zao.
“Kila siku tunawalalamikia polisi kuwa chanzo cha vurugu, huu ni ushahidi tosha mmezunguka jukwaa langu lote huku wananchi ambao ni walengwa mmewasogeza mbali,” alisema Dk Slaa na kuongeza:
“Sikuja hapa kuongea na nyie, nimewafuata wananchi naomba mtoke mkae mbali ili watu wangu wasogee karibu na hiyo ni amri.”
Kitendo ambacho kilipokelewa kwa shangwe na wananchi kwa kushangilia na kuweza kusogea karibu ya jukwaa.

No comments:

Post a Comment