Sunday, April 7, 2013

Mwananchi yazoa tuzo za umahiri

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Seif Sharif Hamad (kushoto) akimkabidhi mfano wa hundi ya dola 4,000 za Marekani mshindi wa  jumla wa Tuzo ya Uandishi Bora, mwandishi wa gazeti la The Citizen, Lucas Liganga, wakati wa hafla ya utoaji wa tuzo hizo iliyoandaliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) Dar es Salaam, juzi usiku. Picha  na  Emmanuel Herman 
Dar es Salaam: Waandishi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) inayochapa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti wameibuka tena kidedea kwenye tuzo  za umahiri wa Uandishi wa Habari Tanzania (EJAT) kwa mwaka 2012, baada ya kushinda tuzo 13, ikiwamo ya mshindi wa jumla.
Sherehe za utoaji wa tuzo hizo ilifanyika jana katika Ukumbi wa Diamond Jubilee na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwamo Makamu wa Kwanza wa Rais, Seif Sharif Hamad ambaye alimwakilisha Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein.
Mshindi wa jumla kwa mwaka 2012 ni Lucas Liganga wa gazeti la The Citizen, ambaye ameifanya MCL kunyakua tuzo hiyo kwa miaka miwili mfululizo ambapo mwaka 2011 tuzo hiyo ilichukuliwa na Neville Meena wa gazeti la Mwananchi.
Washindi walipewa zawadi za magodoro, televisheni, Ipad na vyeti, huku mshindi wa jumla akipewa dola 4,000 za kujiendeleza kimasomo.
MCL iliingiza fainali waandishi 14 kati ya 66 walioteuliwa kuwania tuzo hizo ambao ni pamoja na Samweli Mwamkinga, Florence Majani, Polycarp Machira, Tom Musoba, Elias Msuya, Leon Bahati, Lucas Liganga, Shija Felician, Fredy Azzah, Joseph Zablon, Zephania Ubwani, Tumaini Msowoya, Anthony Mayunga na Edward Qorro.
Mbali na kutoa mshindi wa jumla, waandishi sita wa magazeti hayo walikuwa ndio wagombea pekee wa tuzo mbili za habari bora ya Uchumi na Biashara na Majanga, huku Azzah akishinda tuzo ya habari bora ya Virusi vya Ukimwi (VVU) ambapo alikuwa peke yake na alichaguliwa mara mbili kuwania tuzo hiyo.
Waandishi wa MCL walioshinda na tuzo zao katika mabano ni Edward Qorro (Uchumi na Biashara), Lucas Liganga (Mazingira na Malaria), Fredy Azzah (Ukimwi na Elimu), Anthony Mayunga (Utawala Bora).
Wengine ni Florence Majani (Sayansi na Teknolojia na Afya ya Uzazi), Samwel Mwakibinga (Mchora katuni bora), Zephania Ubwani (Kilimo), Polycarp Machira (Majanga), Shija Felician (Tuzo ya wazi).
Katika tuzo ya jumla MCL iliingiza waandishi watatu kati ya waandishi wanane waliochaguliwa kuwania tuzo hizo ambao ni Lucas Liganga, Fredy Azzah na Florence Majani.
Katika utoaji wa tuzo hizo, MCL ilifuatiwa na Shirika la Utangazaji (TBC) ambalo lilizoa tuzo nane, Afya Redio (6) na Kilimanjaro Film Institute (5).
Tuzo ya Uchumi na Biashara kwa upande wa televisheni ilichukuliwa na John Lewanga wa TBC, tuzo ya michezo na utamaduni kwa upande wa magazeti ilichukuliwa na Abdul Mohammed wa gazeti la The African, Abdallah Majura wa ABM FM alishinda tuzo hiyo kwa upande wa redio.
Tuzo ya mazingira upande wa redio ilichukuliwa na Idd Juma Yusuf wa Afya Redio, tuzo ya afya upande wa magazeti ilichukuliwa na Beatrice Shayo wa Nipashe na upande wa redio ilichukuliwa na Gervas Hubile wa TBC-Taifa.
Tuzo za Ukimwi na VVU upande wa redio ilikwenda kwa Andrew Kiwanyi wa Kilimanjaro Film Institute.
Tuzo ya habari za watoto upande wa magazeti ilichukuliwa na Shadrack Sagati wa Habari Leo, upande wa Televisheni alichukua Daniel Kaminyoge wa Kilimanjaro Film Institute, upande wa redio ilichukuliwa na Mwamini Andrew wa TBC.
Utawala bora upande wa Televisheni ilichukuliwa na Jamal Hashim Said wa TBC, upande wa Redio ilichukuliwa na Noel Thompson wa Afya Redio.
Tuzo za habari za jinsia kwa upande wa magazeti ilichukuliwa na Husna Mohammed wa Zanzibar Leo, upande wa Televisheni tuzo hiyo ilichukuliwa na Bernard Mwaituka Televisheni Iringa.
Tuzo ya Sayansi na Teknolojia upande wa  televisheni ilichukuliwa na Rose Kibaja wa TBC na upande wa redio ilichukuliwa na Abel Onesmo wa Clouds FM.
Upande wa tuzo za habari za Majanga kwa upande wa redio alichukua Noel Thompson wa Afya Redio, habari za malaria kwa upande wa Televisheni alichukua Dotto Mnyadi wa TBC na upande wa redio ilichukuliwa na Faraja Sendegeya wa Afya Redio.

No comments:

Post a Comment