Sunday, December 2, 2012

Marekani yapinga uamuzi wa kujenga Yerusalem

WASHINGTON, Marekani
Hillary Clinton 

NCHI ya Marekani imepinga  uamuzi wa Israel kujenga nyumba 3,000 za walowezi Mashariki mwa Jerusalem  pamoja na Ukingo wa Magharibi kwa madai kuwa  unarudisha  nyuma jitihada za amani.
Kwa mujibu wa Waziri wa nchi hiyo, Hillary Clinton alisema kuwa hatua hiyo itakuwa ikirudisha nyuma maendeleo ya nchi hiyo pamoja na jitihada ambazo zinafanywa katika kuleta amani.
"Naomba niseme  kwamba utawala huu, ni kama tawala zilizotangulia na umeweka bayana kwa Israel haiwezi kuendelea na ujenzi huo kwa kuwa  shughuli hizo zinarudisha nyuma jitihada za majadiliano ya amani," alisema Clinton.
Clinton alisema hayo  mbele ya hadhira alipokuwa akizungumza katika jukwaa lililoandaliwa na kituo cha sera za Mashariki iliyowajumuisha mawaziri  mbalimbali akiwemo Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Israel, Avigdor Lieberman  pamoja na Waziri wa Ulinzi, Ehud Barak.
Pia Clinton alisema kuwa suluhisho la kudumu la mgogoro wa Gaza  lingekuwa  ni miongoni mwa  mipango mizuri ya kuleta amani  kati ya Israel na Wapalestina wote.
Utawala wa Rais Barack Obama ulijaribu kuzuia shinikizo la Palestina la kutambuliwa na Umoja wa Mataifa, kwa madai kuwa hatua hiyo imekuwa ni  kizingiti kikubwa  katika amani na kwamba taifa la Palestina lingetokana kwa kuwepo na mazungumzo na Israel.
Hata hivyo, Clinton alisema kuwa pande zote  mbili zinapaswa kufanya kazi kwa pamoja ili kutafuta njia ya kusonga mbele katika mazungumzo ambayo ndiyo yataleta suluhisho la mataifa mawili.
Aliongeza kuwa pande mbili zitakapokuwa tayari kushiriki katika  mazungumzo na Rais Obama  pia atakuwa tayari kushirikiana nao kikamilifu.
Kwa upande wa  msemaji wa Bazara la Taifa la Usalama, Tommy Vietor alisema kuwa vitendo hivyo haviwezi kuleta manufaa yoyote katika meza ya mazungumzo na kuongeza kuwa  Marekani inarejea upinzani wake wa muda mrefu dhidi ya makazi ya walowezi, pamoja na ujenzi Mashariki mwa Jerusalem.
"Tunaamini vitendo hivi havileti manufaa yoyote zaidi ya kuhujumu jitihada za kurudi kwenye meza ya mazungumzo," alisema Vietor.
Taarifa za vyombo vya habari zilisema kuwa  baadhi ya ujenzi wa Israel utafanyika katika eneo linalogombaniwa lililopo katika Ukingo wa Magharibi maarufu kama E1, ambalo linapita kati ya upande wa mwisho wa Mashariki ya eneo lililotekwa la Jerusalem mashariki, na makazi ya Maaleh Adumim.
Vilevile Chama cha Ukombozi wa Palestina (PLO), kimelaani hatua hiyo na kusema ni uvamizi dhidi ya taifa hilo.
Wapalestina wanapinga kwa nguvu zote, mradi wa E1 kwa sababu unaligawanya eneo la Ukingo wa Magharibi katika vipande viwili - Kaskazini na Kusini, hatua ambayo inafanya uundwaji wa taifa la Palestina kuwa mgumu.

No comments:

Post a Comment