MBUNGE wa Ubungo (CHADEMA), John Mnyika ametoboa siri kuhusu kesi ya 
Dowans akisema kuwa serikali imetumia dola za Kimarekani milioni 29, 
sawa na zaidi ya sh bilioni 40 (sh bil. 45.7) kwa ajili ya uendeshaji 
wake.
  Kesi hiyo ya kupinga kulipa faini ya dola milioni 65 zinazodaiwa na 
kampuni hiyo, tayari imekatiwa rufaa na TANESCO na Desemba 5 mwaka huu 
itaanza kusikilizwa katika Mahakama ya Rufaa Tanzania.
  Mnyika alitoboa siri hiyo juzi jijini Mwanza, wakati alipokuwa 
akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni ya Movement for Change (M4C), ya 
chama hicho Kanda ya Ziwa, iliyofanyika Hoteli ya Gold Crest kisha 
kufanikiwa kupata jumla ya sh milioni 29.354. Ilihudhuriwa na wabunge, 
madiwani na viongozi mbalimbali wa CHADEMA.
  Mnyika ambaye pia ni Mkurugenzi wa Masuala ya Habari na Uenezi wa 
CHADEMA taifa, alibainisha kuwa Serikali ya Tanzania imeonekana kuchezea
 fedha za walipa kodi, kwani pamoja na kutumia fedha hizo zote katika 
kuendeshea kesi ya Dowans lakini bado haijamalizika.
  “Dowans wanaidai serikali yetu dola za Kimarekani milioni 65. Na 
katika uendeshaji wa kesi hii Tanzania imetumia dola milioni 29, sawa na
 zaidi ya sh bilioni 40…na kesi bado inaendelea, hii ni moja ya udhaifu 
wa serikali,” alisema Mnyika huku akishangiliwa.
  Mbali na hilo, Mnyika pia aliwageukia vigogo wanaodaiwa kuficha 
mamilioni ya fedha nchini Uswisi akisema kuwa baadhi yao ni wa Chama Cha
 Mapinduzi (CCM).
  Alisema watuhumiwa hao wa ufisadi walihongwa mamilioni hayo ya fedha 
na baadhi ya wawekezaji wanaoingia Tanzania kufanya utafiti wa uchimbaji
 madini na mafuta, na kwamba wanafahamu idadi ya fedha hizo na wamiliki 
wake.
  Katika hotuba yake, Mnyika aliyekuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo 
wa M4C, ambaye pia aliambatana na mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA taifa,
 Godbless Lema, alisema kwamba vigogo hao wa CCM wamehongwa fedha nyingi
 na baadhi ya wawekezaji wanaomiliki makampuni hayo ya utafiti wa mafuta
 na madini.
  “Ushahidi upo, mamilioni waliyoficha Uswisi wamehongwa na baadhi ya 
matajiri wenye makampuni yanayofanya utafiti wa kuchimba madini na 
mafuta hapa nchini kwetu Tanzania. Itafika siku tutawataja kwa majina,” 
alisema mbunge huyo wa Ubungo, ambaye hakufafanua zaidi ya hapo.
  Aliitaka pia Serikali ya CCM chini ya Rais Jakaya Kikwete kuacha 
kuziba pamba masikioni katika hilo, bali ifanye uchunguzi wake wa haraka
 kisha iwakamate na kuwafungulia kesi mahakamani watuhumiwa wote wa 
ufisadi huo wa kutisha.
  Pamoja na hilo, Mnyika alisisitiza kuwa Rais Kikwete ni kiongozi 
dhaifu, kwani ameshindwa kuwawajibisha mawaziri na watendaji wake 
wanaoonekana kushindwa kutekeleza vema majukumu yao katika kuwatumikia 
Watanzania kama walivyoapa.
  Alisema inashangaza Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kutaka 
mawaziri wahojiwe na kujieleza kwenye vikao vya chama pale wanapoonekana
 kushindwa kazi, na kuhoji sababu za Rais Kikwete kushindwa 
kuwawajibisha viongozi na watendaji wake hao hadi kazi hiyo ifanywe na 
chama.
  Kufuatia hali hiyo, Mnyika aliwasihi Watanzania wote kuunganisha nguvu
 ya pamoja na CHADEMA ili kuusaka ukombozi wa nchi hii ifikapo mwaka 
2015 kwa kuiondoa madarakani CCM.
  Katika uzinduzi huo wa M4C, Mnyika pamoja na mbunge wa Musoma mjini 
mkoani Mara, Vincent Nyerere walichangia kiasi cha sh milioni mbili kwa 
kila mmoja, huku Mbunge wa Nyamagana, Ezekiel Wenje na Lema kila mmoja 
akichangia sh milioni moja.
  Baadhi ya wajumbe wengine waliochangia na fedha zao kwenye mabano ni 
Meya wa Musoma, Alex Kisurura (sh milioni moja), Naibu Meya wa Musoma, 
James Bwire (sh 800,000), na mbunge wa Ilemela jijini Mwanza, Highness 
Kiwia ambaye alichangia sh milioni moja.
 
 
 
 

 
No comments:
Post a Comment