Friday, November 9, 2012

WALIOKUTWA NA HATIA REPORT YA GWILIZI HAWA HAPA

SPIKA wa Bunge, Anne Makinda jana alitolea uamuzi Ripoti ya Kamati Ndogo chini ya Mbunge wa Mlalo, Hassan Ngwilizi akiwasafisha wabunge waliotuhumiwa kwa rushwa akisema tuhuma zilizotolewa dhidi yao zimethibitika kuwa ni za uongo.
Katika uamuzi wake aliousoma bungeni jana, Spika ‘aliwakaanga’ Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu wake, Eliakim Maswi huku akitoa onyo kali kwa wabunge walitoa tuhuma kwa wabunge wenzao akisema wanatakiwa kuwa makini wakati wanapochangia bungeni.
Alisema kamati hiyo ndogo ya Haki, Kinga, Madaraka ya Bunge ambayo iliongozwa Ngwilizi ilifanya uchunguzi wa kina kuhusu tuhuma hizo na kugundua kuwa hazikuwa na ushahidi.
Alisema kamati hiyo iliundwa kutokana na michango mbalimbali iliyotolewa na baadhi ya wabunge wakati wakichangia Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini Julai 27, hadi 28, mwaka huu bungeni.
Alisema tuhuma hizo pia ziliibuliwa kwa maandishi na Maswi ambaye alimwandikia barua Katibu wa Bunge.
Spika alisema katika barua yake, Maswi alisema baadhi ya wabunge wa iliyokuwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini walikuwa wanakwenda ofisini kwake kuomba rushwa ili watetee wizara hiyo inapowalisha taarifa mbalimbali kwenye kamati.
Tuhuma nyingine zilikuwa baadhi ya wabunge wa kamati hiyo kuwa na mgongano wa kimasilahi katika kutekeleza majukumu yao ya kibunge ya kusimamia wizara hiyo kwa vile wanafanya biashara na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

Nyingine zilikuwa baadhi ya wabunge kujihusisha na vitendo vya rushwa kwa kupokea fedha kutoka katika kampuni za mafuta kwa lengo la kuzitetea kupinga uamuzi wa Maswi wa kutoa zabuni ya ununuzi wa mafuta mazito ya kuendeshea mitambo ya IPTL na Puma.
Mbali ya Katibu Mkuu huyo kutoa tuhuma hizo, nyingine za kujihusisha na rushwa zilitolewa na wabunge mbalimbali zikielekezwa kwa wabunge wa kamati hiyo.
Makinda alisema kutokana na uzito wa tuhuma hizo aliamua kuunda kamati ya kuchunguza jambo hilo sambamba na kuivunja Kamati ya Nishati na Madini.

Wabunge ambao walituhumiwa na Maswi ni Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Sarah Msafiri ambaye alidaiwa kumwomba Sh50 milioni ili azigawe kwa wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini kwa lengo la kuitetea.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Seleman Zedi alituhumiwa na Maswi kutaka awalipe wajumbe wa kamati yake Sh2 milioni kila mmoja ili awatulize wasiendelee kumshambulia kutokana na utendaji wake waliokuwa wakiulalamikia.

Pia Katibu Mkuu Maswi aliwatuhumu Wabunge wa Viti Maalumu (CCM), Munde Tambwe na Sarah Msafiri na Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka kwamba walimwambia kwamba lazima aachie nafasi kwa kuwajibika kutokana na utendaji wake usioridhisha.

Wabunge ambao walitoa tuhuma kwa wabunge wenzao wakati wakichangia na ambao walihojiwa na Kamati ya Ngwilizi ni Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), Ali Kesi;, John Mnyika (Ubungo-Chadema), Joseph Selasini (Rombo-Chadema), Kangi Lugola (Mwibara-CCM) na Mbunge wa Singida Kaskazini (Chadema), Tundu Lissu ambaye aliitisha mkutano wa waandishi wa habari na kuwatuhumu wabunge wa kamati hiyo kujihusisha na rushwa.

Akitoa uamuzi wake, Spika alisema baada ya kuhojiwa na Kamati ya Ngwilizi, Maswi alishindwa kutoa ushahidi kuthibitisha tuhuma zake kwa wabunge hao.
Alisema hata wabunge wote waliotoa tuhuma kwa wabunge wa kamati hiyo, walishindwa kuthibitisha tuhuma hizo huku wengine wakisema habari za kusikia.
Alisema kutokana na hali hiyo anawasafisha wabunge waliotuhumiwa.

Baadaye Spika Makinda alisema pamoja na kuwasafisha wajumbe hao, ameivunja moja kwa moja Kamati ya Nishati na Madini na kwamba ataunda mpya katika Bunge lijalo.
Alisema kuwa itakuwa vigumu kwa wabunge hao kuendelea kufanya kazi na watendaji wa wizara hiyo na kwamba wabunge hao amewapangia katika kamati nyingine.

Waliotuhumiwa wanena
Akizungumzia hatua hiyo ya Spika, Zedi aliyekuwa mwenyekiti wa kamati hiyo, alisema anashukuru kuwa ukweli umedhihirika. Alisema ingawa alikuwa akijua kuwa tuhuma hizo zilikuwa za uongo, aliamua kuichia kamati ifanye kazi yake na sasa umma umepata ukweli.
Hata hivyo, alisema hana kinyongo na wabunge wenzake waliomtuhumu kujihusisha na rushwa na kwamba amekubaliana na ushauri wa Spika wa kuwasamehe.

Kwa upande wake, Msafiri alisema anashukuru kwamba Watanzania wameujua ukweli kuhusu tuhuma alizokuwa amepewa. Alisema kuwa tuhuma dhidi yake ambazo alikuwa ametuhumiwa na Maswi ni za uongo.

Hata hivyo, Mnyika kwa upande wake alisema hakubaliani na uamuzi wa Spika kuhusu jambo hilo na kusema kwamba atakata rufaa.

“Sijakubaliana na uamuzi wa leo wa Spika kuhusu tuhuma za rushwa dhidi ya wabunge na hatima ya Kamati ya Nishati na Madini. Nitakata rufaa. Ripoti yote ya Ngwilizi inapaswa iwekwe hadharani.”

No comments:

Post a Comment