Monday, November 12, 2012

NMB yawazawadia wanafunzi 66

BENKI ya NMB, jana imewazawadia wanafunzi wawili wa Chuo Kikuu Dodoma (UDOM), Chacha Nyange Nchamcho na Kelvin Gabone, kila mmoja zawadi ya I Pad, katika promosheni ya Ki-COLLEGE Zaidi inayoendeshwa na benki hiyo.
Promosheni hiyo inayohusisha wanafunzi wenye akaunti ya NMB Student, ilifanyika makao makuu ya benki hiyo jijini Dar es Salaam, ambapo washindi wengine wawili walijishindia simu za mkononi aina ya Samsung Galaxy.
Jumla ya washindi 66 walipatikana katika droo hiyo, ambapo 60 kati yao walijishindia zawadi za taa maalumu za kujisomea zinazotumia mionzi ya jua, fulana za NMB, jezi za Taifa Stars na ongezeko mara mbili la kaunti ‘Amana Maradufu.’
Akizungumza wakati wa promosheni ya kuwasaka na hatimaye kuwatangaza washindi hao, Meneja Masoko wa NMB, Shilla Senkoro, aliwataka wanafunzi kuendelea kufungua akaunti ya NMB Student au kuweka amana zao, ili kujishindia zawadi mbalimbali katika droo mbili zijazo.
Senkoro aliongeza kuwa, nia ya promosheni hiyo ni kurudisha sehemu ya faida yao kwa wateja, hususan wanafunzi kupitia akaunti maalumu iliyoanzishwa mwaka 2007, kutokana na ongezeko la vyuo vya elimu ya juu nchini vilivyoongeza idadi ya wateja.

No comments:

Post a Comment