Saturday, November 10, 2012

Juma Kaseja azira Msimbazi

 
NAHODHA wa mabingwa wa soka Tanzania Bara, Simba, Juma Kaseja, amesusia mazoezi ya timu yao tangu kumalizika kwa mchezo wao na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.
Kutokana na kutofanya mazoezi na wenzake muda wote huo, Kocha Mkuu, Mserbia Milovan Cirkovic, hatompanga katika mchezo wa leo dhidi ya Toto African kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Kaseja amekuwa akidai kuwa hakuwa vizuri kwa ajili ya kufanya mazoezi na wenzake kutokana na matusi aliyotukanwa na mashabiki baada ya kulala kwa mabao 2-0 siku hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga, alisema Kaseja alikataa kufanya mazoezi na hatocheza mchezo wa leo, kutokana na kutofanya mazoezi na wenzake akidai hakuwa vizuri kisaikolojia hadi leo.
Kamwaga alisema pia beki Amir Maftah naye ataukosa mchezo wa leo kutokana na kuwa majeruhi mara baada ya juzi kufanyiwa upasuaji mdogo kuondoa uvimbe uliokuwa unamsumbua kwa siku kadhaa kichwani.
“Maftah anatarajiwa kuondolewa nyuzi zake hii leo na wakati wowote anaweza kujiunga na timu ya taifa, kwani maendeleo yake ni mazuri na yanaridhisha, maana sio majeraha makubwa aliyonayo,” alisema Kamwaga.
Mbali na mechi hiyo, kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya, Prisons itaialika JKT Ruvu, huku Kagera Sugar ikiumana na Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Kaitaba wakati JKT Oljoro itamenyana na Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid na Mgambo Shooting itakuwa na kibarua kigumu kwa Azam FC kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Kamwaga alisema timu yao iko vizuri na imefanya mazoezi ya nguvu tangu ilipotoka Morogoro na wachezaji wako vizuri, ukiwatoa wachezaji hao wawili.
Aliwaomba mashabiki na wanachama wao, kujitokeza kwa wingi leo, kwani yaliyopita yameshapita na sasa waelekeze nguvu katika mechi hiyo, kwani sapoti yao itawafanya wachezaji wacheze kwa kujituma zaidi.

No comments:

Post a Comment