Saturday, November 10, 2012

(CCM), wamemchagua diwani aliyevuliwa uanachama na CHADEMA, Henry Matata kuwa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilemela jijini Mwanza.

KATIKA hali ya kushangaza, madiwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wamemchagua diwani aliyevuliwa uanachama na CHADEMA, Henry Matata kuwa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilemela jijini Mwanza.
Uchaguzi huo wa aina yake uliogubikwa na utata kama ule wa Meya wa Jiji la Arusha mwaka jana, ulifanyika huku CHADEMA wakiususia kutokana na kuwepo pingamizi mahakamani, liliowekwa na Matata akipinga kufukuzwa uanachama.
Licha ya manispaa hiyo kuwa na madiwani 14, ni madiwani sita tu, yaani wanne wa CCM, mmoja wa CUF na Matata waliokutana na kumchagua meya na naibu wake.
Meya huyo ambaye ni Diwani wa Kata ya Kitangiri, amechaguliwa siku chache tangu kumalizika kwa uchaguzi mwingine wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza ambao nao ulitawaliwa na mizengwe, na hivyo CCM kutwaa kiti hicho kilichokuwa kikiongozwa na CHADEMA kabla ya manispaa hizo kugawanywa.
Matata alifukuzwa uanachama na Kamati Kuu ya CHADEMA kisha akafungua kesi mahakamani kupinga uamuzi huo, na hukumu ya kesi hiyo bado haijatolewa.
Katika uchaguzi huo wa jana, Matata alipata kura zote sita za ndiyo kwa sababu alikuwa mgombea pekee katika nafasi hiyo, huku diwani wa Bugogwa, Dede Swila (CCM) akichaguliwa kuwa naibu meya wa manispaa hiyo.
Mkuu wa Wilaya hiyo pamoja na mwanasheria wa Jiji la Mwanza, Sarah Savela, walihudhuria uchaguzi huo batili ambao haukutimiza idadi ya wajumbe kwa mujibu wa sheria na kuufanya chini ya ulinzi mkali wa polisi wakiwemo wale wa kikosi cha FFU wakiwa na silaha nzito.
Licha ya kanuni za halmashauri kueleza bayana kuwa idadi halali ya wajumbe lazima itimie theluthi mbili (2/3), bado Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa hiyo, Zuberi Mbyana, aliruhusu uchaguzi huo kufanyika bila idadi kutimia.
Kabla ya uchaguzi huo, Mbyana alisoma barua mbili za uteuzi wa wagombea kutoka CHADEMA, ambapo barua moja ilitoka makao makuu ya chama hicho ikiwa imesainiwa na Mkurugenzi wa Masuala ya Bunge na Halmashauri, John Mrema, na kuwatambulisha diwani wa Nyamanoro, Abubakar Kapera kuwa mgombea umeya na diwani wa Kirumba, Dan Kahungu kama naibu meya.
Alisema barua nyingine ya utambulisho ilitoka ofisi ya CHADEMA Wilaya ya Ilemela, ikisainiwa na Katibu wake, John Anajus, ikiwatambulisha Matata kuwa mgombea nafasi ya umeya na Diwani wa Kata ya Ilemela, Malietha Chenyenge nafasi ya unaibu meya.
Akitoa ufafanuzi wa kisheria mbele ya madiwani hao sita, mwanasheria wa Jiji, Savela alisema, Katiba ya CHADEMA kifungu namba 7.4.10 inaupa mamlaka uongozi wa wilaya kuthibitisha mgombea.
Baada ya mwanasheria Savela kubainisha taratibu za kisheria, Mkurugenzi wa Manispaa hiyo mpya, Mbyana alisimama na kutangaza utaratibu kwa madiwani hao sita kuanza kupiga kura, ambapo Matata aliyekuwa mgombea pekee alisimama na kuomba kura kwa wajumbe.
Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo uliochukua takribani dakika 10, Mbyana alisema Matata ameshinda kwa kupata kura zote sita za ndiyo, huku Swila naye akipata kura zote katika nafasi ya unaibu meya.
Tanzania Daima ilizungumza na Savela ikitaka ufafanuzi wa kisheria juu ya idadi ya wajumbe wanaoruhusiwa, lakini alijibu kwa kifupi: "Unataka ufafanuzi wa hili ili iweje? Kaandike hivyo hivyo kwamba kolamu ya wajumbe imetimia na sheria zimefuatwa."
CHADEMA wapinga
Akizungumza na waandishi wa habari, Mrema alisema uchaguzi huo ni sawa na kikao cha harusi, kwani ulifanyika bila kufuata na kuzingatia sheria za nchi.
"Madiwani wote wa CHADEMA Wilaya ya Ilemela hawakuhudhuria uchaguzi huo. Wajumbe waliopiga kura hawakufikia idadi ya theluthi mbili, kama sheria zinavyosema. Kwa hiyo CHADEMA hatutambui uchaguzi huo,” alisema.
Mrema alisema kuwa aliwasiliana na Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa kuhusiana na hilo, na kwamba chama kitatoa tamko lake kuhusu uchaguzi sahihi wa kumpata meya kwa kufuata taratibu zote.
Mkurugenzi huyo, alimtaka Waziri Mkuu Mizengo Pinda atengue mara moja uteuzi wa Mkurugenzi wa Manispaa hiyo kwa madai kwamba amesimamia uvunjifu wa sheria za nchi.
Naye Chenyenge alikanusha vikali kuteuliwa kwake kuwa mgombea naibu meya wa manispaa hiyo, kama ilivyokuwa imeelezwa kwenye barua ya uteuzi kutoka ofisi ya CHADEMA wilaya hiyo.
Hivi karibuni, madiwani wawili wa CHADEMA, Dan Kahungu (Kirumba) na Josephat Manyerere (Nyakato), waliamuriwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza, kwenda rumande kwa madai ya kudharau amri halali ya mahakama, iliyozuia kufanyika uteuzi wa wagombea meya na naibu wake Manispaa ya Ilemela.

No comments:

Post a Comment